1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Janga

Afrika Kusini yajiandaa kwa siku 21 za vizuwizi

Rashid Chilumba26 Machi 2020

Mataifa ya Afrika yameendelea kutangaza hatua pana za kudhibiti kusambaa virusi vya Corona wakati idadi ya visa vya maambukizi ikiongezeka barani humo. Afrika Kusini inajiandaa kwa vizuwizi vya siku 21 kuanzia Ijumaa.

https://p.dw.com/p/3a3gE
Corona-Krise Südafrika Pretoria Vorratskäufe in Supermarkt
Picha: AFP/P. Magakoe

Afrika Kusini ambalo ndilo taifa lenye visa vingi vya maambukizi ya corona barani Afrika imetangaza hatua kali kuelekea Ijumaa, siku ambayo nchi hiyo itaanza kutekeleza marufuku ya matembezi na kuwalazimisha watu kusalia nyumbani.

Waziri anayeshughulia idara ya polisi nchini humo amesema wakati wa kipindi cha wiki tatu raia wa Afrika kusini  watazuiwa kufanya mazoezi mbali na maakazi yao, kutembeza wanyama na amewataka wa Afrika Kusini kuepuka kunywa pombe ndani ya muda huo.

Wanajeshi na polisi wa nchi hiyo ndiyo wamepewa jukumu la kusimamaia marufuku ya watu kutembea na maeneo yote ya kuingia Afrika Kusini ikiwemo mipaka ya ardhini, bandari na viwanja vya ndege vimefungwa.

Südafrika Präsident Cyril Ramaphosa
Rais Cyril Ramaphosa ametangaza siku 21 za kukaa ndani nchini Afrika Kusini, kuzuwia kuenea kwa virusi vya Corona.Picha: AFP/M. Spatari

Hapo jana waziri wa afya wa Afrika Kusini Zweli Mkhize alisema visa vya maambukizi nchini humo vimefikia 709 na kuongeza wanatarajia idadi hiyo kupanda jambo lililomlazimisha kutoa wito kwa raia wa nchi hiyo kuwasidia maafisa wa afya kupambana na ugonjwa wa COVID-19 kwa kusalia majumbani.

Katika taifa jirani la Lesotho, serikali imetangaza kuzifunga shughuli zote nchini humo kwa muda wa siku 21 kuanzia siku ya Jumamosi na itaruhusu huduma muhimu pekee kama afya, ulinzi, maduka ya chakula na benki kuendelea na kazi.

Kulingana na shirika la afya la Umoja wa Mataifa bara la Afrika lina zaidi ya visa 2,000 vya virusi vya Coorna na idadi ya waliokufa kutokana na janga hilo imepindukia watu 50.

Nchini Kenya na Uganda marais Uhuru Kenyata na Yoweri Museveni wametangaza hatua pana ikiwemo kuzuia matembezi, marufuku kadhaa katika matumizi ya magari ya umma na kuzifunga shughuli za kawaida kama mikahawa ya chakula na vilabu vya pombe.

Wizara ya Afya nchini Ghana imetangaza vifo vya wagonjwa wawili zaidi siku ya Jumatano huku taifa hilo la Afrika Magharibi likitangaza ongezeko la wagonjwa wapya 15 na kufanya idadi ya walio na maambukizi ya virusi vya Coorna kufikia 68.

Afrika Coronavirus Pandemie / Südafrika
Maduka yamekauka wakati watu wakifanya manunuzi ya pupa kujiandaa na vizuwizi vinavyoanza Ijumaa, Machi 27, 2020.Picha: Getty Images/AFP/F. Pesce Blazquez

Nchini Libya, serikali inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa imeripoti kisa cha kwanza cha mgonjwa wa Coorna ambaye ni mwanaume mwenye miaka 73 aliyeingia nchini Libya akitokea Tunisia baada ya kuyatembelea maeneo matakatifu  nchini Saudi Arabia.

Taifa lingine la Afrika Mgaharibi la Mali nalo lilitangaza wagonjwa wa kwanza wawili ambao ni raia wa nchi hiyo waliorejea nyumbani wakitokea Ufaransa.

Katika hatua nyingine, madaktari na wauguzi nchini Zimbabwe wameingia kwenye mgomo jana Jumatano wakisema hawana mawazo maalum ya kuwakingia dhidi ya virusi vya Corona wanapowahudhumia wale wanaoshukiwa kuambukizwa.

Taifa hilo linakabiliwa na maamndalizi duni ya kukabiliana na ugonjwa wa COVID-19 na tayari limerikodi visa vitatu vya ugonjwa huo.