Afrika Kusini yafunga ofisi zake za ubalozi Nigeria
5 Septemba 2019Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Afrika Kusini, Lunga Ngqengelele amesema baada ya kupokea taarifa na vitisho kutoka kwa baadhi ya Wanigeria, wameamua kuzifunga kwa muda ofisi hizo zilizoko Abuja na Lagos, huku wakiifatilia kwa makini hali ya mambo inavyoendelea. Lunga amesema ofisi hizo zilifungwa Jumatano kwa lengo la kuwalinda wafanyakazi wake na zitafunguliwa tena pindi watakapoona kuna umuhimu wa kufanya hivyo.
Amebainisha kuwa uamuzi wa kusitisha shughuli zake za kibalozi kwenye miji hiyo miwili, umechukuliwa baada ya kundi la watu kujaribu kuumavia ubalozi mdogo wa Lagos. Afrika Kusini na Nigeria jana ziliimarisha usalama baada ya mashambulizi ya Johannesburg dhidi ya raia wa kigeni kusababisha ulipizaji kisasi kwa wafanyabiashara wa Afrika Kusini kwenye miji kadhaa ya Nigeria.
Wakati huo huo, serikali ya Tanzania ambayo ni mwenyekiti wa Jumuia ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika, SADC imeelezea kusikitishwa na mashambulizi hayo na imetoa msimamo wake wa kuunga mkono hatua iliyochukuliwa na Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa aliyelaani vikali mashambulizi hayo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania Palamagamba Kabudi, amesema Tanzania inaendelea kuwa na mawasiliano ya karibu na Afrika Kusini.
Mvutano wa kidiplomasia umeongezeka kati ya Nigeria na Afrika Kusini, huku Nigeria ikitangaza kuwa itaususia Kongamano la Kiuchumi Duniani kuhusu Afrika linalofanyika mjini Cape Town, Afrika Kusini ambalo lilikuwa lihudhuriwe na Makamu wa Rais wa Nigeria, Yemi Osinbajo pamoja na viongozi wengine kadhaa wa Afrika.
Siku ya Jumanne, Nigeria ilimuita balozi wa Afrika Kusini nchini humo kwa mazungumzo na ilisema Rais Muhammadu Buhari alitarajiwa kupeleka mjumbe kwa Rais Ramaphosa, kuelezea kusikitishwa kwake na mashambulizi hayo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, Naledi Pandor amesema maafisa wa Nigeria na Afrika Kusini wamekuwa kwenye mawasiliano ya mara kwa mara wakijaribu kuituliza hali ya mambo. Aidha, amebainisha kwamba hakuna sheria ya kuwalipa fidia walioharibiwa mali zao kutokana na mashambulizi hayo.
Ama kwa upande mwingine, Afrika Kusini imeifunga kampuni yake ya huduma za simu, MTN pamoja na duka lake kubwa la bidhaa mbalimbali la Shoprite nchini Nigeria, kutokana na mashambulizi hayo yanayozilenga biashara za nchi hiyo.
(AFP, Reuters)