1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika kusini waungana katika sala kumkumbuka Mandela

8 Desemba 2013

Waafrika kusini watajikusanya leo Jumapili(08.12.2013)makanisani, misikitini, na masinagogi katika kumbukumbu ya Nelson Mandela, ambaye ujumbe wake wa amani na maridhiano ulivuka mipaka ya ukabila na dini.

https://p.dw.com/p/1AUv9
Nelson Mandela aus dem Krankenhaus entlassen
Nelson Mandela wakati wa uhai wakePicha: Reuters/Mike Hutchings

Siku hiyo itakayoadhimishwa nchini kote ya sala inaadhimisha mwanzo wa wiki nzima ya mazishi ya kitaifa kwa mtu ambaye aliweza kuunda Afrika kusini mpya isiyokuwa na kibaguzi, yenye makabila mbali mbali dhidi ya mabaki ya enzi wa ubaguzi ambao alipambana kuung'oa.

Rais wa marekani Barack Obama na mkewe Michelle watahudhuria sala ya kumbukumbu mjini Johannesburg siku ya Jumanne, amesema afisa wa Ikulu ya Marekani ya White House, mmoja kati ya idadi kubwa inayoongezeka na viongozi wa dunia ambao wanatarajiwa kwenda nchini Afrika kusini kutoa heshima zao za mwisho kwa shujaa huyo aliyepambana dhidi ya ubaguzi wa rangi.

Stimmen und Reaktionen zum Tod Nelson Mandelas
Rais Jacob ZumaPicha: Reuters

Kumbukumbu

Kumbukumbu hiyo itafikia kilele pale Mandela atakapozikwa Desemba 15 mwaka huu katika kijiji cha Qunu, kijiji ambacho alikulia. Rais Jacob Zuma amesisitiza kuwa sala hiyo itakayofanyika leo ifanyike bila huzuni na kwamba itakuwa ni kusherehekea kile alichokiacha Mandela ambaye alifariki siku ya Alhamis baada ya kuugua kwa muda mrefu, akiwa na umri wa miaka 95.

"Tunapaswa , wakati tukiomboleza , pia kuimba kwa sauti ya juu kabisa , kucheza na kila kitu tutakachofanya, kusherehekea maisha ya mtu huyo mwanamapinduzi," amesema Zuma.

Rais Zuma alitarajiwa kuhudhuria sala katika kanisa la Methodist katika eneo linalokaliwa zaidi ya Wazungu mjini Johannesburg, wakati rais wa zamani Thabo Mbeki atajiunga na sala hiyo katika sinagogi mjini humo.

Kundi kubwa la waumini pia linatarajiwa katika kanisa kubwa nchini humo la Kikatoliki katika moja ya maeneo yanayoishi Waafrika pekee mjini Soweto.

Sala hizo zitafanyika pia mjini London , ambako askofu mkuu wa Canterbury Justin Welby , kiongozi wa kiroho wa Waanglikani milioni 80 duniani kote , ataongoza sala ya kumbukumbu. Afya ya Mandela ilikuwa inaporomoka mno katika wakati fulani, hata hivyo kifo chake kimekuja kwa mshituko mkubwa kwa Waafrika kusini ambao uhusiano wao kwake , rais wa kwanza mweusi katika nchi hiyo ulikuwa haumithiliki na wa karibu mno.

Taarifa ya kifo

Tangu pale taarifa za kifo chake zilipotolewa , makaazi yake mjini Johannesburg yamekuwa kama mahali pa hija, ambao maelfu ya watu walimiminika katika eneo hilo kutoa rambi rambi zao.

Trauer um Nelson Mandela
Maua kama ishara ya kumuenzi mzee MandelaPicha: Reuters

Hali kwa nyakati tofauti imekuwa ya majonzi na sherehe, baadhi ya watu wakiweka maua kama rambi rambi zao, wengine wakicheza na kuimba kwa heshima ya mtu huyo ambae wanamapenzi nae ya karibu na kumtambua kama Madiba.

"Kwangu mimi sio siku ya huzuni. Ni siku ya matumaini, kwetu sisi kuweza kuamua hatima yetu," amesema muuza bidhaa Khabile Mgangame.

Familia ya Mandela imefananisha kutoweka huko kwa mpendwa wao kuwa ni kama mateso ya kutengwa wakati wa muda mrefu wa kifungo katika jela ya kisiwa cha Robben.

Nguzo imeondoka

"Nguzo ya familia haiko tena, kama alivyokuwa wakati alipotengwa na jamii kwa muda wa miaka 27 yenye maumivu makali akiwa jela," msemaji wa familia Temba matanzima amewaambia waandishi habari mjini Johannesburg siku ya Jumamosi (07.12.2013).

Kuwapo kwake kulikuwa kama mbuyu ambao unatoa kivuli chenye utulizo ambao ulikuwa unatoa ulinzi na usalama kwetu," amesema Temba akimfananisha na mti mkubwa wa mbuyu.

Stimmen und Reaktionen zum Tod Nelson Mandelas
Mshumaa ukiwaka ikiwa ni ishara ya mwanga unaomulika taifa hilo, Nelson MandelaPicha: Reuters/Siphiwe Sibeko

Siku ya Jumanne(10.12.2013) kiasi ya watu 80,000 wanatarajiwa kuhudhuria , pamoja na rais Obama wa Marekani , sala maalum katika uwanja wa mpira wa mjini Soweto ambao ulikuwa uwanja uliofanyiwa fainali ya kombe la dunia mwaka 2010.

Wakati huo huo mwili wa Mandela utawekwa hadharani ili watu waweze kutoa heshima zao za mwisho kwa siku tatu kuanzia Jumatano, ambako jeneza lake litachukuliwa katika msafara kupitia katika mitaa ya mjini Pretoria kila asubuhi ili kuwapa fursa watu wengi zaidi iwezekanavyo kuuagana mwili wake.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe

Mhariri: Amina Aboubakar