1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika kuboresha hali ya wakimbizi

12 Februari 2019

Mkutano wa siku mbili wa Umoja wa Afrika umekamilika Jumatatu hii mjini Addis Ababa nchini Ethiopia. Azimio muhimu lililofikiwa lilikuwa kuhakikisha nchi za bara la Afrika zinaunda sera za kuboresha huduma za wakimbizi. 

https://p.dw.com/p/3DC8z
Äthiopien Gipfeltreffen der Afrikanischen Union in Addis Abeba
Picha: Getty Images/AFP/S. Maina

Mkutano wa siku mbili wa Umoja wa Afrika umekamilika hapo jana mjini Addis Ababa nchini Ethiopia, azimio muhimu lililofikiwa likiwa kuhakikisha nchi za bara la Afrika zinaunda sera za kuwawezesha wakimbizi na watu waliolazimika kuyahama makazi yao, wapate maisha bora na huduma bora katika nchi ambazo wanaishi. 

Mwenyekiti mpya wa Umoja wa Afrika, ambaye pia ni rais wa Misri, Abdel Fattah al- Sissi ametoa wito wa juhudi za makusudi zifanyike kuzitafutia ufumbuzi changamoto za wakimbizi na wahamiaji zinazolikabili bara la Afrika. Hitimisho la mkutano huo uliohudhuriwa na wakuu wa nchi, wakuu wa serikali au wawakilishi wao, al Sissi alisema viongozi wa Afrika wametambua kuwa ni lazima kuwe na suluhisho la kudumu kwa chanzo cha watu kulazimika kuyahama makazi yao.

"Tumemaua kutengeneza nafasi zaidi za ajira kwa vijana wetu na kuwa na bara lenye ufanisi ambao utavishughulikia vyanzo vya shida ambazo bara letu linakabiliwa nazo na kuimarisha juhudi zetu za kuwasaidia wakimbizi, na waliolazimika kuyahama makazi yao kwa njia ya kukidhi mahitaji yao, pamoja na kuweka sera kusaidia kuyajenga upya mataifa yaliyoharibiwa na vita." alisema al-Sissi.

Ugaidi ni suala lililoangaziwa pia kwenye mkutano wa kilele wa AU.

Marais hao pia walijadili kuhusu njia za kukabiliana na ugaidi barani Afrika. Suala la ugaidi limeendelea kuwa changamoto katika baadhi ya maeneo barani humo, na limekuwa likisababisha kukosekana kwa hali ya utulivu kwenye maeneo hayo.

Somalia Kämpfer der Terrormiliz al-Shabaab
Wanamgambo wa Al-Shabaab wakifanya mazoezi ya kijeshi kaskazini mwa mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.Picha: picture-alliance/AP Photo/F. Abdi Warsameh

Mwenyekiti wa kamisheni ya Umoja wa Afrika, Mahammat Moussa Faki alisema, "Suala la ugaidi ni suala ambalo limekuwa changamoto kubwa zaidi barani Afrika. Tumeamua kuwa bara letu litanufaika kutoka kwa Misri katika kupambana na ugaidi. Marais wameamua wataanzisha kituo cha kuangalia ujenzi wa nchi zilizoathiriwa na vita na maendeleo. Kituo hiki kitakuwa nchini Misri na hili ni jambo muhimu katika kuzitatua shida zetu za ukosefu wa amani na usalama"

Wajumbe wa mkutano huo wa mjini Addis Ababa pia walijadili suala la vita na mzozo nchini Libya, na kufikia maamuzi ya kuandaliwa kwa mkutano utakaowahusisha wadau wote nchini humo ili kufikiwa kwa makubalino ya amani na kuwawezesha kuandaa na kufanya uchaguzi mwezi Oktoba mwaka huu.

"Tunajua kuwa vita nchini Libya vimeathairi nchi jirani. Ni shida ngumu na ina gharama nyingi. Hivi majuzi Chad imeshambuliwa na magaidi kutoka Libya. Ikiwa hali nchini Libya itaendela kama ilivyo. Kwa hivyo sasa ni wakati wa jamii ya kimataifa kuunga mkono jitihada za pamoja ya Umoja wa Afrika na Umoja wa mataifa ili kufikia malengo ya kudumisha amani nchini humo." alisema Kamishna anayeshughulikia amani na usalama katika kamisheni ya Umoja wa Afrika, balozi Ismael Chergui.

Mwenyekiti mpya wa Umoja wa Afrika, Rais wa Misri, Abdel Fattah al Sissi, amesema ataendeleza mchakato wa kufanya mageuzi katika uendeshaji wa shughuli za Umoja wa Afrika na kamisheni yake ambao mtangulizi wake Rais Paul Kagame wa Rwanda aliuanzisha mwaka uliopita alipokuwa mwenyekiti.

Mwandishi: Colleta Wanjohi DW, Addis Ababa.

Mhariri Josephat Charo.