Gazeti la der Freitag, ambalo liliandika juu ya kulazimishwa kwa serikali ya mpito nchini Sudan na Marekani, kufanya mambo yasiyokubalika na raia wake kutokana na dhiki inayoipitia nchi hiyo. Der Freitag linasema tangu rais ambaye sasa amepinduliwa Omar al-Bashir alipoingia madarakani mwaka 1989, nchi hiyo imetengwa na sehemu nyingine za dunia kwa jina la haki za binadamu.
Vikwazo vya kiuchumi vilifuatiwa na kuorodheshwa kama taifa linalofadhili ugaidi na waranti wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC dhidi ya rais Bashir. Ilishuhudiwa namna anguko la Bashir lilivyokuwa na gharama kubwa, wakati mamia ya watu walipofariki katika makabiliano na jeshi. Madhara ya kiuchumi yalikuwa makubwa, lakini walibali? kuchukua hatari kutokana na matumaini waliyokuwa nayo.
Wakati Marekani ilipotambua mafankio ya vuguvugu la umma, hawakuamua kuijenga upya nchi hiyo mara moja. Ikiwa Khartoum ilitaka kurejeshwa tena katika mfumo wa kimataifa, basi ilipaswa kulipa gharama. Katikati mwa mwezi Oktoba, rais Donald Trump alitangaza kwamba fidia ya dola milioni 335 ingelipwa kwa wahanga na ndugu wa wahanga wa mashambulizi ya kigaidi, ambayo utawala wa zamani ulihusika nayo.
Na wakati huo huo, serikali ya mpito ikiwa imelewa, kutokana na hali ngumu ya kiuchumi, ilishinikizwa kuitambua Israel na kusawazisha uhusiano wake na taifa hilo. Hatua kama hiyo haikuwapendeza raia wa Sudan ambao hawakushauriwa juu yake.
Der Freitag linasema Marekani ililazimisha makubaliano hayo kuonesha nini inachoweza kufanya. Ukweli ni kwamba hakutakuwa na uhusiano wowote maalumu au mpana kati ya Israel na Sudan, lakini suala muhimu ni kutengeneza mazingira katika ulimwengu wa Kiarabu, yanayozishawishi nchi muhimu zaidi kuanzisha mawasiliano na Netanyahu, mfano Saudi Arabia.
Magazeti ya Die Tageszeitung na Neues Deutschland yaliandika juu ya waranti uliotolewa wa kukamatwa kwa katibu mkuu wa chama tawala nchini Afrika Kusini - ANC. Die Tageszeitung lilisema kampeni ya rais wa Afrika Kusini Cyrill Ramaphosa kupambana na rushwa katika kambi yake imefika kilele cha kuvutia. Majira ya mchana tarehe 10 mwezi, vituo vingi vya redio na televisheni vilikatisha matangazo yake ili kuripoti juu ya habari usioweza kusubiri:
Shirika la juu kabisa la usimamizi wa sheria nchini humo, NPA, lilithibitisha kwamba mtu wa pili kwa nguvu ndani ya chama cha ANC baada ya rais, katibu mkuu Ace Magashule, alipaswa kujitokeza mbele ya jaji siku ya Ijumaa kujibu tuhuma za rushwa ya mamilioni, vinginevyo angefikishwa na polisi kwa lazima.
Maghashule anadaiwa miongoni mwa mambo mengine, kuhusika na ubadhirifu wa fedha za serikali kiasi cha euro milioni 14 katika mrdi wa nyumba mwaka 2014.
Katika wiki za karibuni, wanachama 13 wandamizi wa ANC wamekamatwa pamoja na wafanyabiashara maarufu walio karibu nao. Hatua hizi zinaenda sambamba na msimamo unaochukuliwa na rais Ramaphosa, ambaye wakati anachukuwa madaraka mwishoni mwa Februari 2018, aliahidi kukomesha rushwa iliyokithiri ya mtangulizi wake Jacob Zuma na watu wake wa karibu.
Gazeti la Die Tageszeitung liliandika pia kuhusu hali ya wasiwasi iliyozuka nchini Cote d'Ivoire baada ya kuchaguliwa tena kwa rais wa taifa hilo Alasane Ouattara. Gazeti hilo liripoti kwamba hofu ya vurugu bado haijaondoka, na katika moja ya ngome za Ouattara, wakaazi wamekimbilia mafichoni. Lakini pia die Tageszeitung liliripoti juu ya hali ya usalama inayozidi kuporomoka kaskazini mwa Msumbiji.
Likiwa na kichwa cha habari kisemacho "Utorokaji hatari katika bahari ya Hindi", die Tageszeitung linasema vita vya wenyewe kwa wenyewe kaskazini mwa Msumbiji vinawalazimu maelfu ya watu kukimbilia maisha yao kuvuka bahari ya Hindi kuelekea mji wa pwani wa Pemba. Baadhi hawanusuriki safari hiyo, lakini pia kubakia nyumbani sio chaguo.
Nalo Gazeti la Frankfurter Allgemeine limeripoti juu ya hofu iliyotanda kuhusu uwezekano wa kutumbukia katika machafuko, eneo la pembe ya Afrika kutokana na mzozo kati ya serikali ya Ethiopia na mkoa wa Tigray kaskazini mwa nchi hiyo.
Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, amejaribu kutuliza hali kwa kusema kwamba mzozo huo wa kijeshi utaisha katika muda sio mrefu, akisema kuwa operesheni ya kijeshi iliyoagizwa na serikali yake ilikuwa inaendelea kama ilivyopangwa dhidi ya chama cha Ukombozi wa Watu wa Tigray, TPLF, kinachotawala mkoa huo, na kutangaza kukombolewa kwa maeneo kadhaa kutoka kwa vikosi vya mkoa huo.
Gazeti linazungumzia mzozo ulioibuka kati ya serikali ya waziri mkuu Abiy pamoja na viongozi wa mkoa huo, unaoelezwa kusababishwa na mageuzi makubwa aliyoanza kuyatekeleza Abiy baada ya kuchukuwa usukani wa serikali, ambayo watu wa Tigray, waliohodhi siasa za Ethiopia kwa muda mrefu, wanayaona kama yanawabagua.