Afrika katika Magazeti ya Ujerumani
12 Aprili 2024die tageszeitung
Gazeti la die tageszeitung, liliiangazia kumbukumbu ya mauaji ya kimbari ya Rwanda. Limeanza kwa kuandika kuwa wakati tayari miaka 30 imepita tangu mauaji ya halaiki ya mwaka 1994 dhidi ya Watutsi hadi sasa kuna waathiriwa milioni moja na watuhumiwa milioni mbili wa tukio hilo baya ambalo halikutarajiwa. Licha ya muda wote huo kupita, bado hatua za kisheria hazina dalili ya kukamilika.
Watu wanaotuhumiwa kuhusika na mauaji hayo wanaendelea kutafutwa hata Ujerumani. die tageszeitung linamnukuu Mkuu wa upelelezi wa idara maalumu ya kuwatafuta wanaotuhumiwa kuhusika na tukio hilo Jean Bosco Siboyintore akisema bado wanawatafuta zaidi ya watuhumiwa 1,000. Orodha ya majina ya watuhumiwa hao inaonesha pia nchi wanakoishi zikiwemo Ufaransa, Ubelgiji, Marekani, Canada na Ujerumani.
Zeit online
Zeit Online liliiangazia hatua ya watawala wa kijeshi wa Mali ya kupiga marufuku shughuli zote za kisiasa katika taifa hilo. Limeanza kwa kuandika, zaidi ya vyama 80 vya Mali vilipaza sauti kutaka ukomo wa utawala wa kijeshi na kuitishwa kwa uchaguzi. Lakini kufuatia amri ya kiongozi wa utawala wa kijeshi, sasa shughuli za vyama vya kisiasa zimepigwa marufuku.
Sababu ya kupigwa marufuku kwa shughuli hizo za kisiasa zimetajwa na msemaji wa serikali hiyo ya kijeshi kuwa ni ili kudumisha utulivu. Gazeti hili la mtandaoni limeandika kuwa, awali zaidi ya vyama 80 na mashirika ya kiraia yalitoa taarifa ya pamoja iliyotoa wito wa kutaka uchaguzi wa rais ufanyike na kuutaka utawala wa kijeshi ufike kikomo haraka iwezekanavyo.
Gazeti hilo linaongeza kuwa, hali ya usalama katika taifa hilo la Afrika ya magharibi ambalo liko chini ya utawala huo wa kijeshi inazidi kuzorota. Limeitaja hali hiyo kuwa inachochewa na migogoro ya kisiasa na kiutu inayonaoikabili nchi hiyo.
Neue Zürcher Zeitung
Neue Zürcher, wiki hii limeripoti juu ya kuanza kutumika kwa sarafu mpya nchini Zimbabwe. Sarafu hiyo itatumika kama mbadala wa noti ya dola ya Zimbabwe ya trilioni 100. Gazeti hilo limeandika, Benki kuu ya nchi hiyo ilitangaza kutumia noti mpya inayoitwa Zimbabwe Gold au kwa kifupi "ZIG" inayochukua nafasi ya dola ya Zimbabwe ambayo imepoteza robo tatu ya thamani yake tangu mwaka ulipoanza. Dola ya Zimbabwe ilianza kutumiwa mwaka 2019.
Kuanza kutumika kwa sarafu hiyo ni jitihada za hivi karibuni za nchi hiyo za kukabiliana na mfumuko mkubwa wa bei na kuimarisha uchumi ambao umekuwa ukiporomoka bila udhibiti kwa karibu miongo miwili. Gazeti hilo linakwenda mbali zaidi na kusema, serikali ya Zimbabwe inapaswa kulaumiwa kwa changamoto hiyo kwani mara kwa mara, imekuwa ikitoa shinikizo kwa benki kuu kuchapisha fedha ili kulipa madeni na kujinufaisha, utamaduni ulioanza chini ya utawala wa aliyekuwa kiongozi wa taifa hilo hayati Robert Mugabe.
Noti mpya ya Zimbabwe iliyoanza kutumika itasaidiwa na akiba ya dola na thamani ya dhahabu ili isipoteze nguvu yake kama sarafu zilizotangulia.
Gazeti la Welt online
Magazeti kadhaa ya hapa Ujerumani wiki hii yameandika kuhusu uwindaji wa tembo unaofanywa barani Afrika kama sehemu ya michezo. Gazeti la Welt online limieandika, uingizwaji wa wanyamapori wanaowindwa Afrika kama sehemu ya michezo, na kisha kutumika kwa ajili ya maonesho umekithiri nchini Ujerumani.
Bidhaa za wanyama hao zinazotajwa kuingizwa Ujerumani ni pamoja na ngozi za pundamilia, vichwa vya chui na meno ya tembo.
Zaidi gazeti hilo limeweka wazi kuwa, utalii wa uwindaji ni biashara halali, yenye faida kubwa na inayokua kwa kasi. Ni mchezo mkubwa Afrika. Linaitolea mfano Botswana ambayo serikali yake hivi karibuni ilionesha kukasirishwa na mipango ya waziri wa mazingira wa Ujerumani Steffi Lemke ya kutaka kuzuia uingizwaji wa wanyama waliowindwa kama sehemu ya michezo na kuingizwa Ujerumani kwa ajili ya maonesho.
Welt Online limemnukuu meneje mradi wa shirika la kutetea haki za wanyamapori la Pro Wildlife Mona Schweizer, ambaye katika mahojiano na gazeti hilo ameilaani vikali biashara hiyo.
Neuer Zürcher
Tukamilishe kwa kulitupia jicho gazeti la Neuer Zürcher, lililoandika kuhusu chanjo mpya ya R21/Matrix-M dhidi ya Malaria kwa njia ya sindano. Linatanabaisha kuwa, kwa miaka mingi madaktari barani Afrika wamekuwa wakiisubiri kwa shauku kubwa chanjo ya aina hii.
Hii ni kwasababu, siku hadi siku kumekuwa na vifo vingi katika wodi za watoto kwenye hospitali za nchi kama vile Guinea, Kongo, Uganda na nyinginezo. Vifo hivyo vinatokana na ugonjwa huo wa kitropiki hatari kwa watoto.
Neur Zürcher linabainisha kuwa, hivi karibuni, kundi la watafiti wa kimataifa kutoka India, Mali, Burkina Faso, Kenya na Uingereza lilichapisha ripoti katika jarida la kila wiki la utafiti wa kitabibu la "The Lancet", kuhusu ufanisi wa chanjo hiyo kwa watoto 5477 wa Afrika ya magharibi. Chanjo hiyo imetengenezwa kutoka katika chanjo iliyokwishaanza kutumika ya Mosquirix.
Ripoti iliyochapishwa na jarida hilo inasema kuwa baadhi ya watoto walipata chanjo hiyo dhidi ya Malaria mara tatu. Matokeo ni ya kuridhisha. Ufanisi wake kwa watoto wenye umri wa miezi 5-17 ambao athari za Malaria zinaweza kuwasababishia vifo ulikuwa asilimia 79.
Chanjo hiyo inaarifiwa kuwa ilizuwia visa 868 vya Malaria kati ya watoto 1,000 kwa mwaka. Bila chanjo ya aina hii, inakadiriwa kuwa mtoto mmoja kati ya kila Watoto 10 anaweza kufa kutokana na Malaria.
Vyanzo: Deutsche Zeitungen