Afrika katika magazeti ya Ujerumani
9 Desemba 2022die tageszeitung
Gazeti la die tageszeitung ambalo limeandika juu ya msukosuko unaomkabili rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa. Linasema rais huyo yumo katika kizungumkuti cha mgogoro. Gazeti linasema chama chake kinachotawala kimegawika, uchumi wa nchi umo katika hali mbaya, vurumai inazidi nchini na sasa kashfa zinamzunguka.
Gazeti hilo linaeleza kuwa uchunguzi uliofanyika wiki iliyopita umeonyesha kuwa huenda alikiuka katiba ya nchi. Mkasa unaohusika ni wizi wa dola milioni nne za kimarekani zilizokuwamo kwenye shamba lake binafsi. Mkasa huo ulitokea miaka miwili iliyopita. Gazeti la die tageszeitung linaeleza kuwa rais Ramaphosa hakutoa taarifa juu ya kumiliki fedha hizo kama anavyotakiwa kufanya kwa mujibu wa sheria.
Gazeti hilo pia linatilia maanani kwamba hakuna ripoti iliyotolewa polisi juu ya wizi huo na badala yake wanaotuhumiwa kuwa wezi ndiyo waliotekwa nyara. Kwa mujibu wa taarifa wevi hao walihongwa fedha ili wanyamaze. Watuhumiwa hao walikamatwa nchini Namibia na kurudishwa nchini Afrika Kusini. Gazeti la die tagezeitung linasema matatatizo yanayomkabili rais Ramaphosa bado hayajaondoka.
Handelsblatt
Gazeti la Handelsblatt linazungumzia juu ya ziara ya waziri wa uchumi wa Ujerumani Robert Habeck aliyofanya barani Afrika katika juhudi za kutafuta masoko mengine ya nishati. Gazeti la Handelsblatt linauliza jee bara la Afrika linaweza kuisaidia Ujerumani kuondokana na kuzitegemea Urusi na China? Gazeti linaeleza kuwa lengo la ziara ya waziri Habeck ni kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na anakusudia kujenga msingi wa uhusiano na nchi za Afrika ili kuiwezesha Ujerumani kupunguza kuzitegemea China na Urusi kwa mahitaji yake ya malighafi.
Gazeti linafahamisha kwamba katika ziara yake waziri Habeck ameenda pamoja na mameneja wa biashara. Gazeti la Handelsblatt limemnukulu mwenyekiti wa baraza la biashara la Ujerumani akisema kuwa Afrika ni barala la fursa na kwamba bara hilo linaendelea haraka kuliko sehemu nyingine nyingi za dunia.
Kituo cha kwanza cha ziara ya waziri wa Ujerumani kilikuwa Namibia. Gazeti la Handelsblatt linasema Ujerumani inakusudia kushirikiana na Namibia katika uzalishaji wa nishati endelevu katika sekta ya nguvu ya maji. Mradi kabambe wa nishati inayotokana na nguvu ya maji ni ishara ya matumiaini makubwa katika uhusiano baina ya Ujerumani na Namibia.
Hata hivyo gazeti linatilia maanani kwamba wapo watu wenye mashaka juu ya miradi hiyo kwa sababu wamekumbusha kwamba miradi ya hapo awali barani Afrika ilishindikana. Sababu ni kwamba miradi hiyo ilikuwa ya gharama kubwa. Mbali na hayo gazeti linasema bado pana changamoto kubwa barani Afrika kuhusu utekelezaji. Gazeti linasema ziara ya waziri Habeck ni muhimu lakini haitatatua matatizo ya Ujerumani haraka.
Der Tagesspiegel
Gazeti la Der Tagesspiegel linasema virusi vya Omikron vilivyogunduliwa nchini Afrika Kusini vimewashangaza wataalamu wa mambo ya afya. Gazeti hilo linasema virusi hivyo vilienea haraka mnamo kipindi cha muda mfupi na kujibadilisha mara kwa mara. Gazeti la Der Tagesspiegel linaeleza kuwa virusi vya Omikron vilikuwapo kwa muda mrefu bila ya kugundulika barani Afrika. Gazeti hilo linaarifu kuwa watafiti walibainisha kwamba watu 25 walikuwa wameambukizwa virusi vya Omikron kabla ya kugundulika nchini Afrika kusini.
Gazeti linakumbusha kwamba Ujerumani ilitoa agizo kwa wananchi wake la kuepuka safari za kwenda Afrika Kusini. Linasema hatua hiyo iliathiri uchumi wa Afrika Kusini. Limemnukulu profesa wa magonjwa ya kuambukiza Erika Sander, akisema kwamba Afrika Kusini ilistahili kusaidiwa na siyo kutengwa.
Frankfurter Allgemeine
Gazeti la Frankfurter Allgemeine linasema vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Angola havijasahauliwa. Gazeti hilo linasema miaka 20 iliyopita yalikuwapo matumaini ya vita hiyvo kumalizika. Chama cha UNITA kimekuwa kinapambana na majeshi ya serikali inayoongozwa na chama cha MPLA. Gazeti linaeleza kuwa pande mbili hizo zinapigania madaraka na utajiri wa nchi, na hasa mafuta na almasi.
Gazeti la Frankfurter Allgemeine linakumbusha kwamba baada ya kiongozi wa UNITA, Jonas Savimbi kuuliwa amani ilirejea nchini Angola. Hata hivyo gazeti linasema athari za vita hivyo bado zinaonekana hadi leo. Pia linatilia maanani kwamba walionufaika na amani ni wachache waliojitajirisha. Kwa mfano ukoo wa rais wa hapo awali Jose Eduardo dos Santos. Hata hivyo vijana wanasema hakuna anayetamani siku za vita. Rika changa la vijana wa Unita linasema halitaki kumwaga damu na halijioni kuwa kuwa rika la waasi.
Vyanzo: Deutsche Zeitungen