1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani 26.06.2020

26 Juni 2020

Sudan sasa inayo matumaini ya kupata msaada wa kimataifa wa kuiwezesha kuanza upya hayo ni baadhi ya yaliyoandikwa juu ya Afrika katika magazeti ya Ujerumani

https://p.dw.com/p/3eOiG
Nigeria Lagos Zeitungsleser
Picha: AFP/P.U. Ekpei

Tunaanza na gazeti la die tageszeitung juu ya mkasa wa kusikitisha uliotokea katika jimbo la Kano, kaskazini mwa Nigeria. Watu126 walitumikishwa kwenye kiwanda cha mpunga kwa miezi kadhaa kwa lazima. Watu hao waliwekwa katika mazingira ya kinyama. Hawakupatiwa chakula cha kutosha wala dawa walipokuwa wagonjwa.

Wanawake na wanaume hao pia hawakuruhusiwa kuzitembelea familia zao. Gazeti la die tageszeitung linasema kiwanda hicho sasa kimefungwa baada ya idara husika za serikali ya Nigeria kupewa habari. Mameneja watano wamekamatwa. Gazeti linasema jambo la kutia wasi wasi ni kwamba watu hao walikuwa wanafanya kazi wakiwa wamekaribiana bila ya barakoa.

Hadi Jumatano iliyopita watu zaidi ya 21,000 walikuwa wameambukizwa virusi vya corona nchini Nigeria. Gazeti linafahamisha kwamba wafanyakazi kwenye kiwanda hicho cha mpunga waliambiwa wafanye kazi ya ziada mnamo mwezi wa Februari kufidia muda wa kufungwa kwa kiwanda hicho kutokana na maambukizi ya virusi vya corona.

Gazeti la Der Tagesspiegel linatupeleka Sudan. Linasema baada ya harakati za kuleta mapinduzi vijana wa nchi hiyo sasa wanaweza kuwa na matumaini. Sudan sasa inayo matumaini ya kupata msaada wa kuanza upya.

Linasema ni jambo la nadra kwa Umoja wa Ulaya, Marekani, Umoja wa Afrika na nchi za Ghuba kusimama pamoja kwa ajili ya kuujenga mustakabal wa nchi yenye migogoro kama Sudan. Wadau mbalimbali wa kimataifa wanaliunga mkono baraza la mpito la raia na wanajeshi lililoundwa mwaka uliopita nchini Sudan. Ujerumani pia ni miongoni mwa nchi zinazotaka kuona maendeleo imara ya Sudan.

Hata hivyo gazeti la Tagesspiegel linatilia maanani kwamba haitakuwa rahisi kwa Sudan kuujenga upya uchumi wake kwa haraka sababu ni kwamba nchi hiyo bado imelemewa na vikwazo vya Marekani. Sudan imehusishwa na mashambulio ya kigaidi yaliyofanywa kwenye balozi za Marekani nchini Kenya na Tanzania.

Kutokana na hayo Marekani imeiweka Sudan katika orodha ya nchi za kigaidi. Marekani inafikiria kuiondoa Sudan kwenye orodha hiyo, lakini gazeti la Der Tagesspiegel linasema mchakato huo utachukua muda.

Gazeti la Neue Zürcher linazungumzia juu ya uchaguzi wa marudio nchini Malawi mapema wiki hii. Baada ya rais wa hadi sasa Peter Mutharika kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa kwanza, watu waliandamana kupinga ushindi wake. Mshindani wake kasisi Lazarus Chakwera aliwasilisha malalamiko kupinga matokeo hayo. Hesabu za kura zililikuwa za kufinyanga. Gazeti la Neue Zürcher linasema hilo si jambo la nadra barani Afrika!

Jambo la nadra, linasema gazeti hilo ni uamuzi uliotolewa na mahakama kuubatilisha ushindi wa rais Mutharika. Neue Zürcher linatilia maanani kwamba uamuzi kama huo ulipitishwa na mahakama ya nchini Kenya mnamo mwaka 2017. Ushindi wa Uhuru Kenyatta ulibatilishwa na mahakama. Gazeti hilo linasema jambo la kulitilia maanani ni kwamba mara nyingi hakuna uhuru wa mahakama kwenye nchi hizo.

Gazeti la Die Zeit liazungumzia juu ya baa la nzige katika Afrika Mashriki. Linasema kwa muda wa miezi kadhaa wadudu hao wamekuwa wanateketeza mashamba kwenye sehemu hiyo. Die Zeit linaeleza kuwa wavamizi hao wanaotokea kwenye nchi za jangwa wanahatarisha msingi wa maisha ya watu kutokana na kuteketeza mashamba. Gazeti hilo linaeleza kuwa makundi ya nzige yaliingia Kenya kutokea nchi jirani. Kenya inapambana na wadudu hao kwa kutumia ndege, mabomba ya kupulizia na hata fimbo!

Gazeti hilo linatilia maanani kwamba hatari ni kubwa kwa sababu kila baada ya miezi mitatu idadi ya nzige inaongezeka mara 20! wanajazana katika eneo la kilometa moja za mraba na kuteketeza mimea sawa na chakula kinacholiwa na binadamu 35,000 kwa siku.

Gazeti la Die Zeit limeinukulu ripoti ya kimataifa inayoonyesha kwamba watu zaidi ya milioni 25 kwenye eneo la Afrika mashariki hawana uhakika wa kupata chakula cha kutosha. Gazeti hilo linasema zaidi ya asilimia 80 ya watu katika nchi za Afrika Mashariki wanategemea kilimo. Ikiwa mashamba yao yatateketezwa na nzige maafa makubwa yatatokea.