Afrika katika magazeti ya Ujerumani
8 Februari 2019Frankfurter Allgemeine
Makala ya gazeti la Frankfurter Allgemeine inazungumzia juu ya hatua ya kutia moyo barani Afrika. Rais Faustin-Archange Touadera wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, na viongozi wa makundi 14 ya waasi walitia saini mkataba wa kuleta amani katika nchi hiyo. Mkataba huo ulitiwa saini mjini Khartoum na kushuhudiwa na rais wa Sudan Omar al-Bashir. Hata hivyo gazeti la Frankfurter Allgemeine linaeleza kwamba huo ni mkataba wa saba kutiwa saini katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, tangu mwaka 2012 na mikataba yote ya hapo awali ilisambaratika.
Yapo mashaka iwapo mkataba huo mpya utadumu kwa sababu yapo makundi fulani ya wapiganaji ambayo hayako tayari kuacha biashara ya dhahabu, almasi na mifugo inayowaletea utajiri mkubwa. Mazungumzo yaliyouleta mkataba huo wa amani katika Jamhuri ya Afrika ya Kati yalidhaminiwa na Umoja wa Mataifa kwa pamoja na Umoja wa Afrika.
Gazeti hilo la Frankfurter Allgemeine linakumbusha kwamba mgogoro wa Jamhuri ya Afrika ya Kati ulianza mnamo mwaka 2013 baada ya wanamgambo wa Seleka kutwaa mamlaka na kumtimua rais Francois Bozize lakini waasi hao walitimuliwa haraka sana na wanamgambo wa Anti-Balaka waliotuhumiwa kutenda ukatili mkubwa.
Berliner Zeitung
Gazeti la Berliner linatupeleka Afrika Kusini ambako, linasema kiwango cha ufisadi ni kikubwa zaidi kuliko ilivyodaiwa hapo awali na linatueleza zaidi kwamba Afrika Kusini imepata mshtuko mkubwa kutokana na ushahidi uliotolewa kwa muda wa siku nane na mfichua siri, Angelo Agrizzi. Mtoboa siri huyo, aliyekuwa mkurugenzi wa kampuni ya mambo ya usalama, inayoitwa Bosasa, aliufichua mfumo wa kifisadi ndani ya kampuni hiyo uliowanufaisha wanasiasa wa ngazi za juu, watumishi wa umma, viongozi wa jumuiya za wafanyakazi na maafisa wa idara kuu ya kodi nchini Afrika Kusini.
Gazeti hilo linafahamisha kwamba katika kipindi cha miaka 15 iliyopita kampuni hiyo ilijipatia tenda za serikali za thamani ya Euro zipatazo milioni 800. Na ili kujihakikishia tenda hizo kampuni hiyo iliwahonga mamilioni ya fedha watu wakubwa kwenye wizara za magereza, sheria na mambo ya ndani. Gazeti la Berliner limemnukulu mtoboa siri Angelo Agrizzi alipotoa ushahidi mbele ya tume ya uchunguzi.
Viongozi kadhaa wa chama tawala cha ANC pamoja na rais wa hapo awali Jacob Zuma pia walikuwa wanapokea rushwa kutoka kwenye kampuni hiyo ya Bosasa ya mjini Johannesburg. Mfichua siri huyo Angelo Agrizzi amenukuliwa na gazeti la Berliner akidai kwamba pia naibu wa wakili wa serikali Nomgcobo Jiba alikuwa anapokea rushwa ya kiasi cha Euro 9000 kwa mwezi ili kuficha ufisadi. Gazeti hilo linasema shina la mti wa chama tawala cha African National Congress ANC nchini Afrika kusini limezidi kuliwa na wadudu wa ufisadi.
Süddeutsche Zeitung
Gazeti la Süddeutsche linasema barani Afrika yapo mambo mengine. Linazungumzia juu ushiriki wa akina mama katika nyanja ya siasa na linaeleza kwamba idadi ya wanawake katika nafasi za juu za uongozi bado ni ndogo. Bado ni nadra kuwaona akina mama katika nafasi za wakuu wa nchi au serikali. Kwenye mikutano ya viongozi wa Afrika wanaonekana ni watu wanaojitinga suti na tai. Blauzi na magauni hayaonekani kwa wingi. Mpaka sasa ni katika nchi tano tu ambako wanawake waliwahi kushika nyadhifa za juu kabisa tangu kutokomezwa kwa ukoloni.
Hata hivyo gazetihilo la Süddeutsche linasema kuanzia miaka ya hivi karibuni limejitokeza rika jipya la wanasiasa miongoni mwa wanawake waliofanikiwa kuviruka viunzi vilivyokuwa vinawazuia na linatilia maanani kwamba nchini Ethiopia, kwenye baraza la mawaziri 20, kumi ni wanawake. Rais wa nchi hiyo pia ni mwanamke bi Sahle-Work Zewde. Nchini Rwanda asilimia 68 ya wabunge ni wanawake. Afrika imeshawahi kuwa na marais wanawake, nchini Liberia, Malawi na Mauritius na pia rais wa kipindi cha mpito katika Jamhuri ya Afrika ya kati.
Gazeti la Süddeutsche limemnukulu waziri mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed, akieleza kuwa wanawake hawanaswi haraka katika mtego wa ufisadi. Gazeti hilo pia limenukulu ripoti ya jopo la wataalamu wa baraza la masuala ya nje nchini Marekani wakieleza kuwa nchi zinakuwa na amani zaidi chini ya uongozi wa wanawake.
Mwandishi: Zainab Aziz/deutsche Zeitungen
Mhariri: Josephat Charo