1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

10 Agosti 2018

Yaliyoandikwa kwenye magazeti ya Ujerumani juu ya masuala na matukio ya barani Afrika wiki hii ni pamoja na uamuzi wa rais Joseph Kabila wa kutogombea tena kiti cha urais katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

https://p.dw.com/p/32xJM
DRC Präsident Joseph Kabila
Picha: Reuters/K.Katombe

Süddeutsche Zeitung

Msemaji wa Kabila ndiye alieutangaza uamuzi wa mwanasiasa huyo Jumatano iliyopita, saa chache tu kabla ya kumalizika kwa muda wa kujiandikisha kwa wagombea. Badala yake Kabila amemteua Emmanuel Ramazan Shadary kusimama katika uchaguzi huo utakaofanyika tarehe 23 mwezi wa Desemba. Ramazan Shadary ni waziri wake wa mambo ya ndani na usalama. Hata hivyo gazeti la Süddeutsche linatufahamisha kwamba bwana Ramazan Shadary amewekwa katika orodha ya Umoja wa Ulaya ya kuwekewa vikwazo kutokana na kukiuka haki za binadamu na kutumia mkono wa chuma katika kuwaandama wapinzani.

 Neue Zürcher

 Gazeti la Neue Zürcher wiki hii linauzingatia mgogoro wa fedha ulioikumba Zimbabwe. Linasema nchi hiyo inazidi kukaukiwa fedha na linaeleza kwamba Zimbabwe ambayo tangu mwezi wa Julai inaendelea kuongozwa baada ya Robert Mugabe kuondolewa madarakani nchi hiyo sasa imo katika hali mbaya sana ya kiuchumi.

Gazeti hilo linaeleza kwamba safari hii mgogoro huo siyo wa mfumuko wa bei bali ni wa kukaukiwa fedha. Mnamo mwaka 2009 Zimbabwe iliiondoa sarafu yake ya kitaifa na kuanza kutumia dola ya Marekani kwa kufanyia miamala yote ya kifedha. Uamuzi huo ulisaidia kuzuia mfumuko wa bei kwa kiwango kikubwa, lakini sasa Zimbabwe imeshamaliza akiba ya dola za Marekani.

Zimbabwe ambayo katika miaka iliyopita ilikuwa mzalishaji chakula mkuu barani Afrika, sasa inaagiza chakula kutoka nje na kwa hivyo inalazimika kutumia fedha nyingi za kigeni. Hali hiyo imesababisha uhaba wa fedha. Gazeti hilo la Neue Zücher linasema uhaba wa fedha za kigeni unayatatiza siyo tu maisha ya kila siku ya watu wa Zimbawe bali pia unazitatiza kampuni za nje zinazofanya biashara nchini humo. Linasema matumaini ya kulitatua tatizo la Zimbabwe la kutumia dola ya Marekani yanategemea na uongozi mpya uliochaguliwa na wananchi baada ya Robert Mugabe kutimuliwa.

Frankfurter Allgemeine

Nalo Gazeti la Frankfurter Allgemeine linasema hakuna sababu ya watu kuteseka na njaa barani Afrika, linasema kuwa sehemu kubwa ya ardhi haitumiwi vizuri ili kuweza kuzalisha chakula cha kutosha. Na linaeleza kwamba katika nchi nyingi za Afrika kilimo bado hakijaleta tija kubwa. Kwa sababu wakulima wadogo wadogo hawana mitaji na ujuzi wa kisasa. Kutokana na uzalishaji mdogo wa chakula takriban thuluthi moja ya watu barani Afrika, kusini mwa jangwa la Sahara hawapati lishe ya kutosha. Kwa mujibu wa shirika la chakula duniani, FAO idadi hiyo inawakilisha watu milioni 220. Gazeti la Frankfurter Allgemeine linasema ipo sehemu kubwa ya ardhi yenye rutuba ,lakini mavuno ni hafifu.

Gazeti hilo linasema wakulima wadogo wadogo wanavuna tani moja hadi mbili tu, katika kila hekta barani Afrika, wakati barani Ulaya, Marekani na barani Asia, wakulima wanavuna wastani wa tani hadi nne katika kila hekta. Mafanikio hayo yamepatikana kutokana na kutumia mbegu bora, matumizi bora ya mbolea na kuendeleza kilimo cha umwagiliaji.

Gazeti hilo la Frankfurter Allgemeine linatilia maanani katika makala yake kuwa serikali za Afrika zinatambua kwamba pana ulazima wa kuleta usasa katika kilimo.Linasema mnamo mwaka 2003 Umoja wa Afrika ulipitisha azimio la kutenga asilimia 10 ya bajeti kwa kila nchi, kila mwaka kwa ajili ya kuendeleza kilimo lakini mpaka sasa ni nchi nne tu zilizoweza kulifikia lengo hilo.

Die Zeit

Gazeti la Die Zeit liizungumzia Rwanda kuwa ni nchi inayowapa wanawake haki sawa, kuliko nchi nyingine yoyote barani Afrika. Hata katika sekta ya filamu ni wanawake nchini Rwanda wanaohusika na kugawa majukumu katika uchezaji wa filamu yaani. Gazeti la Die Zeit limemnukulu mwigizaji na mwongozaji filamu Dida Nibagwire, akiyasema hayo.

Gazeti hilo linaeleza zaidi kwamba Rwanda ni nchi yenye watu wapatao millioni 12 ambapo wanawake wana usemi mkubwa. Asilimia 64 ya wabunge nchini humo ni akina mama na asilimia 40 wanatumikia nyadhifa mbalimbali za uwaziri. Nusu ya mahakimu kwenye mahakama kuu ya Rwanda ni wanawake. Gazeti la Die Welt linatilia maanani kwamba masuala  ya jinsia nchini Rwanda hayajadiliwi kwenye ofisi za  wizara tu, bali  yanazingatiwa katika bajeti ya nchi,elimu,kilimo na katika sekta zote za maendeleo. Bila ya akina mama hakuna kitakachofanyika! 

Mwandishi:Zainab Aziz/Deutsche Zeitungen

Mhariri:Josephat Charo