Afrika katika magazeti ya Ujerumani
3 Agosti 2018die tageszeitung
Matokeo ya uchaguzi yalikuwa wazi kabisa kwa sababu vyama vilivyopigania uhuru vinafahamika kuwa kichwa ngumu barani Afrika. Ni vigumu kuviondoa vyama hivyo vinapokuwamo madarakani. Licha ya uchaguzi huo wa kwanza kufanyika bila ya Robert Mugabe mshindi alijulikana tangu mwanzoni, mgombea wa chama tawala cha ZANU-PF.
Berliner Zeitung
Gazeti la Berliner Zeitung linatilia maanani kwamba risasi zilirindima katika mji mkuu, Harare baada ya matokeo ya uchaguzi kuanza kujulikana. gazeti hilo linaeleza kwamba chama cha upinzani cha Movement for Democratic Change (MDC ) kimeilaumu tume ya uchaguzi kwa kuiba kura kwa kiwango kikubwa. Hata hivyo wajumbe wa Umoja wa Ulaya walioruhusiwa kuwa waangalizi wa uchaguzi huo kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu, wamesema kwa jumla uchaguzi ulionyesha dalili za kutia moyo japo yalikuwapo mashaka ya kutiliwa maanani.
Wajumbe kutoka Umoja wa Afrika - AU na kutoka jumuiya ya maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika -SADC wamesema uchaguzi huo ulifanyika kwa haki na amani na kwamba umefungua njia ya kuendeleza demokrasia nchini Zimbabwe.
Süddeutsche Zeitung
Na katika maoni yake juu ya uchaguzi wa Zimbabwe gazeti la Süddeutsche linasema hakuna mshindi wa kweli katika uchaguzi huo bali ni Wazimbabwe wengi waliokula hasara. Gazeti hilo la Süddetusche Zeitung linafafanua kwamba uchaguzi wa Zimbabwe ulipaswa kuwa huru na wa haki lakini hali haikuwa hivyo.
Chama cha ZANU-PF kiliwashinikiza watu wampigie kura mgombea wa urais wa chama hicho Emmerson Mnangagwa aliekuwa mshirika mkubwa wa Robert Mugabe kwa miaka mingi lakini mgombea wa chama cha upinzani naye pia hakujipambanua kuwa bora kwa kujitangaza mshindi kabla ya matokeo rasmi kutolewa!
die tageszeitung
Katika makala yake nyingine wiki hii gazeti la die tageszeitung linatupeleka Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambako polisi walitumia mabomu ya kutoa machozi ili kuwatuliza wafuasi wa Jean Pierre Bemba, aliyerejea nchini humo baada ya miaka 11 nje ya nchi.
Gazeti hilo linaeleza kwamba baada ya kuachiwa huru na mahakama ya kimataifa ya mjini The Hague ICC na baada ya kutumikia kifungo cha miaka 10 jela, Bemba amerejea nyumbani.Mwanasiasa huyo aliewahi kuwa makamu wa rais, kiongozi wa upinzani, na mbabe wa kivita katika jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo anawania kiti cha urais. Kurejea kwake nchini Kongo, maana yake ni kwamba kampeni za uchaguzi zimeshaanza.
Gazeti hilo la die tageszeitung linatilia maanani kwamba Bemba anaweza kuwa mshindani mkali katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika tarehe 23 mwezi Desemba lakini kwanza anapaswa kuruka kiunzi cha sheria kinachoweza kumzuia kugombea urais kutokana na kuhusika na matukio fulani ya miaka iliyopita. Gazeti hilo linakumbusha kwamba katika uchaguzi wa rais wa mwaka 2006 ambapo alishindana na rais Joseph Kabila, Bemba alipata asilimia 42 ya kura.
der Freitag
Na sasa tunakwenda Nigeria ambako gazeti la der Freitag linatupasha kwamba wahubiri wanatumia dini kujitajirisha.Gazeti hilo limeandika katika makala yake kuhusu kuchangisha fedha kumegeuka kuwa biashara kubwa nchini Nigeria inayofanyika kwenye makanisa na jumuiya mbalimbali.
Wahubiri wanapewa hadhi kama nyota wa muziki na fedha wanazopata zinawawezesha kusafiri kwa ndege binafsi na kuishi maisha ya kifahari. Ripota wa gazeti la der Freitag aliyeshuhudia matukio kadhaa kwenye kanisa la Covenant mjini Lagos anasema alimwona kasisi Poye Ojumade jinsi alivyokuwa anawahamasisha waumini watoe fedha ili kulichangia kanisa lake.
Ripota huyo amesema aliziona bahasha zilizowekwa kwenye mabechi kwa ajili ya waumini wanaotoa viwango vikubwa vya fedha. Watu hao wanazitumbukiza fedha ndani ya bahasha hizo na wale wanaotoa fedha, kuvuka Euro 800 wanapewa vyeti.
Ushindani ni mkubwa katika biashara hiyo ya kuitumia dini. Wahubiri na wale wanaojiita mitume wanalazimika kuonyesha uwezo wa kutibu magonjwa kama vile kuwapunga watu mapepo na kuwatibu walemavu kama alivyofanya bwana Yesu! Shughuli hiyo imewatajirisha wahubiri hao kwa kiasi kikubwa.
Mchungaji mmoja David Oyedepo anasemekana kuwa na utajiri unaofikia dola milioni 150. Inapasa kutilia maanani kwamba fedha zinazotokana na michango ya kanisani hazitozwi kodi. Licha ya kujua kwamba wahubiri wanazidi kujitajirisha watu wanaendelea kutoa michango na kuwatajirisha hata zaidi!
Mwandishi: Zainab Aziz/Deutsche Zeitungen
Mhariri: Mohammed Khelef