1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

13 Julai 2018

Fursa ya kihistoria iliyojitokeza baada ya viongozi wa Ethiopia na Eritrea kupeana mikono na kukumbatiana inaashiria mwisho wa uhasama baina ya nchi zao katika hatua ya kurejesha uhusiano baina ya nchi hizo mbili.

https://p.dw.com/p/31OQH
Eritrea Treffen Abiy Ahmed und Isaias Afwerk  in Asmara
Picha: picture-alliance/dpa/ERITV

Süddeutsche Zeitung

Mkutano uliofanyika katika mji mkuu wa Eritrea, Asmara baina ya waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed na mwenyeji wake rais Isias Afwerki umefungua fursa ya kihistoria. Mkutano huo haukuwa wa gumzo tupu bali umeleta mabadiliko ya kweli katika uhusiano baina ya Ethiopia na Eritrea. Nchi hizo haraka zimekubaliana kufunguliana ofisi za kibalozi, kuanzisha mawasilinao ya simu na safari za ndege baina yao.

Gazeti la Süddeutsche linasema hatua hizo zimechukuliwa kwa mwendo wa kasi na linasema, baada ya Ethiopia na Eritrea kufikia mapatano ya amani, bara la Ulaya linapaswa kutumia uwezo wake ili kuzisaidia nchi hizo.

die tageszeitung

Gazeti la die tageszeitung linatilia maanani kuwa mabadiliko makubwa yametokea nchini Ethiopia baada ya waziri mkuu mpya Abiy Ahmed kuingia madarakani. Gazeti hilo linaeleza kwamba baada ya utawala wa kidhalimu sasa yapo matumaini nchini Ethiopia miongoni mwa watu wake milioni 100. Maalfu ya wafungwa wa kisiasa wameachiwa na maafisa wa idara za usalama waliokuwa na mitazamo mikali wamestaafishwa.

Äthiopien Präsident  Isaias Afwerki und Premierminister Abiy Ahmed in Asmera
KUshoto: Waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed na kulia ni rais wa Eritrea Isaias AfwerkiPicha: Yemane G. Meskel/Minister of Information

Hata hivyo die tagezeitung linakumbusha kwamba mnamo mwezi uliopita lilifanyika shambulio la gurunedi kwenye mkutano wa hadhara mjini Addis Ababa ambapo waziri mkuu mpya Abiy Ahmed alikuwapo.Yeye alinusurika lakini watu wawili waliuawa gazeti hilo linasema shambulio hilo linaonyesha wazi kuwa katika serikali yake bado wapo watu wasiotaka kuona mabadiliko.

Berliner Zeitung

Nalo gazeti la Berliner Zeitung wiki hii linaturudisha Sudan Kusini. Linasema nchi hiyo imeendelea kuwa katika hali mbaya tangu ijipatie uhuru mnamo mwaka 2011. Gazeti hilo limeandika kwamba asilimia 95 ya watu walioshiriki katika kura ya maoni waliunga mkono hoja ya Sudan Kusini ijitenge na Sudan, lakini mnamo mwaka 2013 moto ulianza kuwaka katika nchi hiyo changa kabisa barani Afrika.

Gazeti la Berliner linaeleza kwamba vita vya wenyewe kwa wenyewe vilianza baina ya watu waliopiga kura ya kuchagua kujitenga na upande wa Kaskazini. Sudan kusini ni nchi yenye makabila makubwa na madogo jumla ya 60.

Wakati mwingine ni vigumu kutambua ni nani anapigana na upande upi? Robo ya watu wa Sudan Kusini wamegeuka wakimbizi wa ndani na nje. Kilimo kimesambaratika katika maeneo mengi ya nchi kwa sababu wakulima hawathubutu kwenda mashambani. Gazeti hilo linasema Sudan Kusini inaendelea kuzama katika dhiki na sasa maisha ya watu wengi yanategemea hisani ya mashirika ya misaada kutoka nje.

Mwananchi wa Sudan Kusini akiwa amebeba bendera ya taifa hilo changa
Mwananchi wa Sudan Kusini akiwa amebeba bendera ya taifa hilo changaPicha: picture alliance/dpa/M. Messara

Frankfurter Allgemeine

Makala ya gazeti la Frankfurter Allgemeine wiki hii inazingatia hali ya kiuchumi barani Afrika. Linasema ustawi wa uchumi unaleta neema kwa watu wachache na kwamba ufukara unaendelea kuwa wa kiwango kikubwa.

Gazeti hilo la Frankfurter Allgemeine limenukuu ripoti za Halmashauri ya Umoja wa Afrika na shirika la ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo,(OECD) zilizobainisha kwamba kasi ya ustawi wa uchumi barani Afrika haitoshi kupunguza idadi ya watu wanaoishi katika utata ingawa ripoti hiyo inasema hatua thabiti zimepigwa katika nchi za Afrika Mashariki ambako zaidi ya humusi moja ya watu wamejikwamua na kuondokana na umasikini uliokithiri.

Utajiri wa mifugo
Utajiri wa mifugoPicha: picture-alliance/F. May

Gazeti hilo linasema ni kweli kwamba umasikini wa kuziba viraka umepungua kutoka asilimia 49 hadi asilimia 36 lakini bado Waafrika milioni 400 wanaishi katika umasikini mbaya sana. Kijana anayefanya kazi barani Afrika kwa wastani ana kipato kisichozidi dola 2 kwa siku. Gazeti la Frankfurter Allgemeine limeeleza kwamba mnamo mwaka 2016 ustawi wa uchumi ulikwama katika nchi nyingi za Afrika kutokana na bei za malighafi kuanguka kwenye soko la dunia.

Gazeti hilo limewanukuu wataalamu waliotoa ripoti hiyo wakitoa ushauri kwa nchi za Afrika wa kuchukua hatua ili kuacha kutegemea kuuza malighafi na bidhaa za kilimo tu. Nchi hizo pia zinapaswa kujaribu kupunguza tofauti za mapato baina ya wananchi wao ili kuondoa umasikini mbaya.

Mwandishi: Zainab Aziz/Deutschen Zeitungen

Mhariri: Mohammed Khelef