1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

6 Julai 2018

Pamoja na masuala mengine magazeti ya Ujerumani wiki hii yameandika juu ya mapatano ya amani yaliyofikiwa baina ya mahasimu wakubwa nchini Sudan Kusini. Kampuni kubwa za Ujerumani kuleta matumaini Afrika.

https://p.dw.com/p/30vf4
Letztes männliches Nördliches Breitmaulnashorn der Welt gestorben
Picha: Reuters/T. Mukoya

Frankfurter Allgemeine

Rais wa Sudan Kusini Salva Kirr na hasimu wake mkubwa Riek Machar walikutana tena baada  ya miaka miwili na kutia saini mapatano hayo. Kulingana na makubaliano hayo, majeshi ya serikali na waasi wanaoongozwa na Riek Machar walipaswa kuacha mapigano katika muda wa saa72. Mkataba huo pia unaweka msingi kuzungumzia juu ya kugawana mamlaka na kuundwa kwa jeshi, polisi na idara za usalama  wa taifa.

Hata hivyo gazeti la Frankfurter Allgemeine limewanukulu, wataalamu na wawakilishi wa mashirika ya misaada wakielezea wasi wasi juu ya makubaliano hayo iwapo yatatekelezwa, gazeti hilo limkariri Jeremy Taylor wa baraza la wakimbizi la shirika la Norway akieleza kuwa makubaliano yaliyotiwa saini mjini Khartoum pia yanaweza kukiukwa kwa sababu hii si mara ya kwanza kwa rais Salva Kirr na Riek Machar kutia saini makubaliano ya kumaliza vita baina yao.

Kushoto: Riek Machar. Kulia: Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir
Kushoto: Riek Machar. Kulia: Rais wa Sudan Kusini Salva KiirPicha: picture-alliance/AP/J. Patinkin

der Freitag

Gazeti hilo linasema Umoja wa Ulaya unatafakari kujenga vituo vya kuwaweka wakimbizi katika nchi za Afrika Kaskazini. Hata hivyo linatilia maanani kwamba, hakuna nchi inayotaka kuwekewa vituo hivyo. Gazeti hilo la der Freitag linasema baada ya mkutano wa viongozi wa nchi za Umoja wa Ulaya wa wiki iliyopita, Umoja huo sasa unachunguza uwezekano wa kujenga vituo hivyo ili kuepusha vifo vya maelfu ya watu vinavyotokea baharini na ili kuweka utaratibu mzuri wa kuwawezesha wakimbizi kupata hifadhi katika nchi za Ulaya.

Hata hivyo hakuna nchi yoyote ya Afrika Kaskazini iliyoonyesha nia ya kuukubali mpango huo wa  Umoja wa Ulaya. Gazeti la der Freitag limewanukulu wawakilishi wa serikali na kibalozi wa nchi hizo  wakisema kuwa nchi zao hazitaki kuwekewa kambi za wakimbizi. Gazeti hilo linasema mpango wa nchi za Umoja wa Ulaya wa kujenga kambi hizo ni ndoto tu. Na Linakumbusha kuwa nchi za Ulaya zilizosabababisha mgogoro wa wakimbizi barani Afrika na kwingineko duniani zinataka kuukwepa wajibu wao .

Neues Deutschland

Gazeti la Neues Deutschland linatufahamisha kwamba kampuni kubwa za Ujerumani zimo katika harakati za kuleta matumaini barani Afrika. Limemkariri naibu waziri wa uchumi wa Ujerumani Matthias Machnig akisema bara la Afrika pia linatoa fursa nyingi za biashara na kwamba bara hilo siyo la kukabiliwa na changamtoto tu. Mwito huo umeitikiwa na kampuni kubwa za Ujerumani za Volkswagen, Allianz na Hapag-Lloyd. Kampuni hizo zinafanya biashara katika nchi za Afrika.

Wakuu wa tawi la Volkswagen la nchini Rwanda. Kushoto: Michaella Rugwizangoga. Kulia: Mkurugenzi mkuu Thomas Schäfer
Wakuu wa tawi la Volkswagen la nchini Rwanda. Kushoto: Michaella Rugwizangoga. Kulia: Mkurugenzi mkuu Thomas Schäfer Picha: DW/S. Schlindwein

Gazeti hilo la Neues Deutschland linafahamisha kuwa kampuni ya magari ya Volkswagen ilifungua kiwanda katika mji mkuu wa Rwanda, Kigali  kitakachokuwa na uwezo hapo baadae wa kuunganisha magari hadi 5000 kwa mwaka kwa ajili ya soko la ndani. Gazeti  hilo pia  limeripoti kwamba kuanzia  mwezi wa Aprili kampuni ya Ujerumani ya meli za kubeba makontena ilianza kutoa huduma kwenye  bandari za Mombasa na Dar es salaam kutokea Jeddah, Saudi Arabia kila wiki. Gazeti la Neues Deutschland linasema kwa kutoa huduma hiyo kampuni ya Ujerumani ya Hapag-Lloyd italiingiza eneo la Afrika Mashariki katika mtandao wa huduma inazotoa duniani kote.

Süddeutsche Zeitung

Gazeti la Süddeutsche wiki hii linatufahamisha kwamba kwa mara ya kwanza madaktari wa wanyama wamefanikiwa kuzalisha viini tete vya faru kwenye maabara. Gazeti hilo linasema hatua hiyo inaweza kuwa msingi wa kuendeleza uwepo wa wanyama hao waliomo katika hatari ya kutoweka.

Gazeti hilo linatufahamisha zaidi kwamba wataalamu walizalisha viini tete hivyo kutokana na kuchanganya mbegu za faru wa aina za kaskazini na kusini. Süddeutsche linakumbusha kuwa faru wa aina ya kaskazini wanahesabika kuwa wametoweka, wa mwisho wa aina hiyo ni yule aliyekuwa anaitwa Sudan aliyekufa nchini Kenya mnamo mwezi Machi. Sasa kwenye hifadhi yamebakia majike tu bila ya dume. Gazeti hilo linasema wataalamu wanatumai kwamba katika muda wa miaka 3 ijayo kifaru wa kwanza wa aina ya kaskazini atazaliwa. 

Mwandishi: Zainab Aziz/Deutsche Zeitungen

Mhariri: Mohammed Khelef