1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

18 Mei 2018

Wiki hii makala katika magazeti ya Ujerumani yameandika kwa undani juu ya njama za Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza za kujiandalia mkakati wa kubakia madarakani pia kuhusu mapambano dhidi ya Malaria.

https://p.dw.com/p/2xxt9
Burundi Pierre Nkurunziza, Präsident
Picha: picture-alliance/AP Photo/B. Mugiraneza

Frankfurter Allgemeine

Makala ya gazeti la Frankfurter Allgemeine, linalotuambia kwamba mzuka umerudi tena nchini Burundi likiwa na maana ya kuzuka utatanishi wa kisiasa.yanamtaja rais wanchi hiyo Pierre Nkurunziza kwamba anakusudia kuendelea kuwamo madarakani hadi mwaka 2034. gazeti hilo linasema tangu miezi miwili iliyopita Rais Nkurunziza anaitwa Imboneza Yamaho kwa lugha ya Kirundi, yaani kiongozi wa milele.

Kiongozi huyo mweye umri wa miaka 54 ameandaa kura ya maoni kwa lengo la kuibadilisha katiba ya nchi yake na hivyo kumwezesha kushika hatamu za uongozi kwa miaka mingi mingine. Lakini kutokana na hali ya kisiasa ya nchini Burundi, ni vigumu kuwa kura hiyo ya maoni imefanyika kwa haki na huru.

die tageszeitung

Gazeti la die tageszeitung limemnukuu mwanaharakati wa haki za binadamu Pierre - Claver Mbonimpa akisema kuwa wananchi hawauwani wenyewe kwa wenyewe nchini Burundi, bali wanauawa na mawakala wa serikali. Na juu ya kura ya maoni Pierre Claver Mbonimpa anayeishi nchini Ubelgiji ameliambia gazeti la die tageszeitung kwamba kura hiyo ya maoni ni maafa kwa watu wa Burundi. Hadi hivi karibuni waliweza kupiga hatua ya kuelekea kwenye demokrasia, lakini sasa Burundi imerudi nyuma na Rais Nkurunziza anataka kuujeresha utawala wa kifalme nchini humo.

Mbonimpa amesema watu wanafikiri lipo tatizo la ukabila nchini Burundi lakini hayo si sahihi, kwa sababu idadi kubwa ya watu waliopinga muhula wa tatu wa Nkurunziza walikuwa ni rafiki zake wa chama cha CNDD-FDD. Mwanaharakati huyo wa haki za binadamu, Pierre-Claver Mbonimpa ameliambia gazeti la die tageszeitung kwamba kura hiyo ya maoni juu ya kubadilisha katiba ya nchi inaweza kusababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Burundi.

Berliner Zeitung

Gazeti la Berliner Zeitung ambalo wiki hii linatupeleka katika Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.Linatuarifu juu ya kuripuka tena kwa maradhi ya Ebola nchini humo gazeti hilo linatilia maanani kwamba shirika la afya duniani WHO limeingiwa wasiwasi juu ya mripuko wa maradhi hayo.

Kwa mujibu wa taarifa, watu wawili waliokuwa na maambukizi ya virusi vya ugonjwa huo waliwasili katika mji mkuu wa jimbo la Ikweta, wa Mbandaka wenye wakaazi zaidi ya milioni moja. Hata hivyo gazeti hilo linafahamisha kuwa shirika la afya la Umoja wa Mataifa safari hii limechukua hatua za haraka na kuwapeleka wataalamu zaidi ya 40 katika Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo tofauti na hali iliyotokea katika nchi za Afrika Magharibi miaka minne iliyopita.

Süddeutsche Zeitung

Nalo gazeti la Süddeutsche wiki hii linatupa taarifa juu ya juhudi za kupambana na maradhi ya Malaria barani Afrika kwa kutumia kifaa kipya. Gazeti hilo linaeleza kifaa hicho kipya kinaweza kubainisha iwapo mtu ana Malaria bila ya kulazimika kutoa damu. Mtaalamu aliyekitengeneza chombo hicho, Vinet Coetzee kutoka chuo kikuu cha Pretoria, nchini Afrika kusini, alikitambulisha kwenye kongamano la wataalamu lililofanyika mjini Kigali hivi karibuni. Chombo hicho kinachoitwa Spectrophotometer kinatumika kwa kukiweka kwenye kiganja cha mtu na kupima nguvu ya mwanga unaotoka katika mwili. Gazeti la Süddeutsche linatujulisha kuwa kifaa hicho kinafanya kazi kwa ufanisi mkubwa, kwa sababu kinabainisha katika muda wa nukta moja tu iwapo mtu ana vijidudu vya Malaria na bila ya mtu kutobolewa kwa ajili ya kutoa damu.

Der Tagesspiegel

Bara la Afrika pia linazalisha utamu wa chokleti unaoonjwa takriban na kila mtu katika mji wa Munich, kusini mwa Ujerumani. Lakini Afrika haisafirishi chokleti bali inasafirisha buni. Gazeti la Der Tagesspiegel linatupasha zaidi juu ya mjasiriamali kijana kutoka mji huo wa Munich, Hendrik Reimers aliwaza kwamba nchi za Afrika zingenufaika zaidi kwa kuuza chokleti kwenye soko la Ujerumani badala ya kuuza buni tu. Na ili kulitekeleza wazo lake Reimers, alianzisha kampuni inayoitwa "Fairafric" na alipata washirika kutoka nchini Ghana.

Ghana inasafirisha tani nusu milioni za Kakao kila mwaka badala ya chokleti lakini sasa kampuni ya Fairafric inauza nchini Ujerumani bidhaa zilizotengenezwa nchini Ghana. Kijana huyo Reimer amesema Ghana inapata zaidi ya Euro 10,000 kwa kila tani ya chokleti! badala ya Euro 2,000 tu kwa kila tani ya Kakao.

Mwandishi: Zainab Aziz/Deutsche Zeitungen

Mhariri: Grace Patricia Kabogo