Afrika katika magazeti ya Ujerumani
26 Januari 2018Süddeutsche Zeitung
Gazeti la Süddeutsche limeandika kwamba serikali ya Ujerumani inapinga kuilipa fidia Namibia lakini kwa kufanya hivyo hadhi yake imeharibika duniani na hasa baada ya watu wa makabila ya Herero na Nama kuwasilisha mashtaka dhidi ya Ujerumani tarehe 5 Januari mwaka uliopita. Ujerumani yenyewe iliweka kipimo cha juu kabisa katika kubainisha mauaji ya kimbari yaliyotokea katika historia duniani, kama vile ilivyoyatambua mauji ya halaiki ya watu wa Armenia.
Gazeti hilo la Süddeutsche linakumbusha katika makala yake kwamba aliyekuwa rais wa Ujerumani Joachim Gauck ndiye aliyesema kwamba kuishughulikia historia ya uhalifu kama huo ndiyo msingi wa jamii ya kisasa na ya kidemokrasia. Gazeti hilo linasema mpaka leo Ujerumani inakataa kuyatambua muaji ya Waherero yaliyofanywa na wakoloni wa Kijerumani katika karne iliyopita. Na linauliza kwa nini panahitajika mazungumzo ili kuyatambua mauaji hayo wakati ilipohusu yale ya Waarmenia bunge la Ujerumani liliyatambua bila ya mazungumzo na Uturuki? Lakini tofauti na Ujerumani.
Frankfurter Allgemeine
Ufaransa imeikubali dhima yake ya ukoloni barani Afrika. Gazeti la Frankfurter Allgemeine linaeleza katika kurasa zake kwamba katika hotuba aliyoitoa kwa wanafunzi wa chuo kikuu cha Ouagadougou, nchini Burkina Faso rais wa Ufaransa Emmanuel Macron aliishangaza dunia jinsi alivyokiri kwa uwazi juu ya uhalifu uliotendwa na wakoloni wa Kifaransa barani Afrika. Katika hotuba yake Marcron alisema ni jambo lisiloeleweka kwa nini sanaa na turathi za Afrika zionyeshwe katika mji wa Paris na mingine ya baranai Ulaya ? Kwa nini zisionyeshwe katika miji ya Lagos, Dakar au Cotonou?
Gazeti hilo la Frankfurter Allgemeine linafahamisha kwamba rais Macron anataka hatua zichukuliwe ili, mnamo kipindi cha miaka mitano ijayo sanaa na turathi za utamaduni wa Afrika zirudishwe kwa Waafrika wenyewe.
Hata hivyo gazeti la Frankfurter Allgemeine linasema, bila ya kuwekwa taratibu za kimataifa zoezi hilo halitaweza kutekelezwa. Gazeti hilo linatilia maanani kwamba rais wa Ufaransa Macron amechukua hatua ya kwanza muhimu, lakini hilo siyo suluhisho. Amekitonesha kidonda tu.
Süddeutsche Zeitung
Jee rais mpya wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa ni mtetezi wa mageuzi au ni mtetezi wa kungwi wake Robert Mugabe? Swali hilo linaulizwa katika makala nyingine ya gazeti la Süddeutsche mnamo wiki hii.
Zimbabwe sasa inaonekana kana kwamba ni nchi nyingine kabisa, tofauti ni jinsi ilivyokuwa hadi mnamo miezi ya hivi karibuni.Takriban kila siku vyombo vya habari vinaripoti juu ya tuhuma zaufisadi zinazowakabili maafisa wa serikali ya chama cha ZANU PF, aidha kila siku rais mpya wa nchi hiyo Emmarson Mnangagwa anazungumzia juu ya mipango juu ya kuijenga Zimbabwe mpya. Vyombo vya habari pia vinaripoti juu ya mipango ya kuufufua uchumi na juu ya kuitishwa haraka, uchaguzi huru na wa haki baada ya miaka 37 ya utawala wa Robert Mugabe.
Hata hivyo gazeti hilo la Süddeutsche linasema viongozi waliopo madarakani nchini Zimbabwe ni wale wale wanaotoka kwenye zizi moja. Gazeti hilo linakumbusha kwamba rais Mnangagwa alimtumikia Mugabe katika nyadhifa za uwaziri na makamu wa rais. Yeye ndiye aliyefanya kazi ya kuondoa uchafu na kuuficha kwa niaba ya Mugabe.
Gazeti la Süddeutsche linasema Mnangagwa anataka kuleta mageuzi bila ya kugeuka na kuushughulikia uhalifu uliotendwa na kungwi wake - Mugabe na bila ya kondokana na itikadi za kizamani.
die tageszeitung
Gazeti la die tageszeitung linazungumzia juu ya kifo cha Roy Bennett kilichosabishwa na ajali ya helikopta iliyotokea nchini Marekani. Gazeti hilo linasema kifo cha Roy Bennet, aliyekuwa mwasisi mmojawapo wa chama cha upinzani nchini Zimbabwe, MDC, kinaongeza mtihani kwa wapinzani nchini humo. Marehemu huyo aliyekuwa mzungu, alisimama kidete kuupinga udikteta wa Mugabe.
Roy Bennet amefariki wakati ambapo chama cha MDC hakimo katika hali nzuri. Kiongozi wake, Morgan Tsvangirai hana afya nzuri, na wakati ambapo rais mpya Mnangagwa bado hajaonyesha dalili za kuleta mabadiliko ya kweli.Gazeti hilo limemnukuu Tsvangirai akisema kuwa Roy Bennet ameacha pengo lisilozibika katika chama cha MDC.
Mwandishi: Zainab Aziz/Deutsche Zeitungen
Mhariri:Yusuf Saumu