Afrika katika magazeti ya Ujerumani
22 Desemba 2017Kwa muda wa zaidi ya nusu mwaka chama cha ANC kilikuwa kinakabiliwa na mivutano ya ndani kuhusu uongozi.Lakini mwanzoni mwa wiki iliyopita chama hicho kilimchagua kiongozi wake mpya Cyril Ramaphosa. Kuchaguliwa kwake kunazingatiwa kuwa hatua muhimu ya kwanza katika kuliwinga wingu la mfarakano lililokuwa limetanda juu ya chama cha ANC. Katika uchaguzi uliofanyika, Ramaphosa alimshinda Nkosazana Dlamini Zuma alieiwakilisha kambi ya rais Jacob Zuma, anaetarajiwa kuondoka madarakani mnamo mwaka 2019. Gazeti la Berliner Zeitung linatilia maanani kwamba,
Kinyang‘anyiro cha kumtafuta rais mpya wa chama cha ANC kilikuwa baina ya kambi ya Ramaphosa na ya Jacob Zuma na ndiyo sababu huenda Ramaphosa akabililiwa na changamoto baada ya kuahidi kuleta mageuzi ya kina ndani ya chama. Hatahivyo ushindi wa Ramaphosa unazingatiwa kuwa muhimu sana katika muktadha wa uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka 2019 nchini Afrika Kusini. Kwa mujibu wa gazeti la Berliner Zeitung, endapo Dlamini Zuma, aliekuwa mke wa Rais Zuma angelimshinda Ramaphosa chama cha ANC kingelikuwamo katika hatari kubwa ya kushindwa katika uchaguzi huo mkuu.
Handelsblatt
Gazeti la masuala ya kibiashara, Handelsblatt pia linazungumzia juu ya hali ya nchini Afrika Kusini na linasema kwamba nchi hiyo inahitaji mwanzo mpya, na linaeleza. Afrika Kusini imekuwamo katika njia mrama. Lakini baada ya kuchaguliwa kiongozi mpya wa chama tawala ANC, Ramaphosa, masoko yanaweka matumaini juu yake. Matumaini ni makubwa kwa sababu Ramaphosa ni mfanya biashara aliefanikiwa na pia ni mtu mwenye ufahamu mkubwa juu ya masuala ya wafanyakazi. Hata hivyo gazeti la Handelsblatt linatahadharisha juu ya kumzingatia Ramaphosa kuwa mtu mwenye uwezo wa kuleta miujiza.Pamoja na hayo linakumbusha kwamba mwanasiasa huyo alikuwa makamu wa rais Jacob Zuma
die tageszeitung.
Gazeti la die tageszeitung wiki hii linazungumzia juu ya uamuzi wa kihistoria uliotolewa na mahakama ya kimataifa ya kupambana na uhalifu ya mjini the Hague.Gazeti hilo linaeleza mahakama ya kimataifa ya mjini The Hague sasa inautekeleza wajibu wake kwa uthabiti wote. Taasisi hiyo ya kisheria iliamua wiki iliyopita kwamba waliokumbwa na uhalifu uliofanywa na mbabe wa kivita Thomas Lubanga nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo walipwe fidia jumla ya dola milioni 10 na mhalifu huyo. Uamuzi huo umefungua njia mpya pamoja na kuhukumiwa, wahalifu hao wanawajibishwa kutoa kifuta machozi kwa wahanga.
Mbabe wa kivita Thomas Lubanga aliekuwa kiongozi wa kundi la wanamgambo wa UPC (Union of Congolese Patriots) aliongoza vita kwenye jimbo la Ituri, kaskazini mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo kuanzia mwaka wa 2002 hadi 2003. Lubanga alitiwa hatiani na mahakama ya kimataifa kwa uhalifu wa kuwaandikisha watoto kupigana vita. Gazeti la die tageszeitung linaeleza kuwa watoto hao walidhulumiwa utoto wao kutokana na kuingizwa kwenye makundi ya wapiganaji.
Watoto hao walilazimishwa kuondoka makwao na kupelekwa vitani.Walinyanyaswa kwenye kambi za kijeshi na walidhulumiwa fursa za kwenda shule.Hata hivyo gazeti la die tageszeitung linatilia maanani kwamba uhalifu uliofanywa na watu hao walipokuwa askari watoto haukuzingatiwa na mahakama. Lakini wao ndio watakaolipwa fidia.
Gazeti la Die tageszeitung pia limeandika kuhusu biashara ya nguo kuu kuu maarufu kama mitumba, Bi Carol Nambuga anauza nguo hizo za zamani kwenye soko kubwa zaidi katika Afrika Mashariki -Soko la Owino, huko mjini Kampala. Lakini kuna hofu kwamba biashara hiyo inaelekea kufikia mwisho wake, kwa sababu Afrika inataka kuimarisha viwanda vyake vya kutengeneza nguo mpya. Die tageszeitung linasema hiyo ni fursa nzuri kwa wafanyabishara wa Ujerumani.
Gazeti hilo linasema kila uchao, maelfu ya wauzaji wa mitumba kama vile Nambuga wanaendesha kazi zao kwenye soko hilo lililo kati ya eneo la biashara za rejareja na mitaa katika barabara za mji mkongwe uliopo mjini Kampala. Zaidi ya wafanyabiashara 50,000 wanashughulika katika eno hilo lenye ukubwa wa heka saba. Wengi, wao kama alivyo Nambuga, wana meza ya mbao au vigingi wanavyotumia kutundika bidhaa zao na ambazo hutumika kama maduka.
Baadhi ya wafanyabishara hao wa mitumba hubeba bidhaa zao mabegani kama vile sidiria, mifuko, mashuka, mikanda au vitambaa kama njia moja ya kuboresha biashara zao. Eneo hilo hushamiri kwa kelele kila mmoja akiinadi bidhaa yake kwa sauti. Lakini sasa, wafanyabiashara wengi katika soko hilo la Owino na masoko mengine kama hayo katika eneo la Afrika mashariki wanaogopa kupoteza ajira zao kutokana na viongozi wa Nchi za Jumuiya ya Mashariki ya Afrika kuamua manamo mwaka jana kuondokana na uagizaji wa mitumba hadi kufikia mwaka wa 2019.
Nchi za Afrika Mashariki kama Rwanda, Uganda,Tanzania na Kenya zitakuwa zinaongeza kodi kwa kila mwaka kwa bidhaa hizo zinapoagizwa. Lengo ni kuongeza mahitaji ya nguo zinazotengenezwa ndani ya nchi zao na hivyo kuweza kufufua sekta ya nguo katika kanda hiyo. Zaidi ya yote, hatua hii inalenga kuongeza nafasi za ajira. Katika mkutano wa biashara kati ya Ujerumani na bara la Afrika uliofanyika mjini Berlin, Rais wa Uganda Yoweri Museveni aliwahimiza wafanya biashara wa Ujerumani kuwekeza katika sekta ya nguo nchini Uganda nchi hiyo ikiwa ni mzalishashaji mkubwa wa pamba katika eneo la Afrika Mashariki.
Mwandishi: Zainab Aziz/Deutsche Zeitungen
Mhariri:Yusuf Saumu