1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya: Uchaguzi bila wapigakura

27 Oktoba 2017

Magazeti ya Ujerumani wiki hii yameangazia uchaguzi nchini Kenya, migogoro DRC na Sudan Kusini na kuuawa kwa wanajeshi wa Marekani nchini Niger.

https://p.dw.com/p/2mch2
Kenia Wahlen Wähler Wahl-Büro
Picha: picture-alliance/AP Photo/S.Abdul Azim

Kwa mara ya pili mwaka huu, Wakenya waliombwa kushiriki katika uchaguzi kumchagua rais wao atakaewaongoza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo. Mahakama ya juu kabisa nchini humo, katika hukumu ya kihistoria ilioitoa mwezi Septemba, ilibatilisha matokeo ya uchaguzi wa rais wa Agosti nane, baada ya kuridhika na hoja za upande wa upinzani kwamba uchaguzi huo ulikiuka katiba.

Likiwa na kichwa cha habari kisemacho, "Uchaguzi bila wapigakura", gazeti la NEUES DEUTSCHLAND lilizungumzia wito uliotolewa na kinara wa upinzani Raila Odinga kwa wafuasi wake kutoshiriki uchaguzi mpya, akisisitiza kuwa masharti waliotoa ya kufanyika kwa mageuzi ndani ya tume ya uchaguzi hayakutelekezwa.

Nalo gazeti la Südedeutsche Zaitung liliielezea hatua ya upinzani kususia uchaguzi mpya wa rais kama hujuma, likilinganisha muitikio wa asilimia 80 katika uchaguzi wa awali, na picha zilizosambaa za uchaguzi wa marudio.

Kenia Kisumu Proteste
Wafuasi wa muungano wa NASA mjini Kisumu, Kenya, wakichoma moto matairi kupinga kufanyika kwa uchaguzi wa marudio katika mji huo.Picha: picture-alliance/dpa

Gazeti la Süddeutsche limeelezea taswira ya uchaguzi wa Alhamisi kuwa nyingine kabisaa, ambapo mtu angeweza kuwaona wasimamizi wakiwa wamekaa tu kwenye vituo vya kupigia kura na wengine hawakujitokeza kabisaa hasa kwenye ngome za upinzani - kwa sababu za kuhofia maisha yao.

Ni uchaguzi ambao Wakenya wengi wameuona kutokuwa na maana, limesema Süddeutsche Zeitung.

Mbiu ya UN katika taifa lililochafuka

Die tageszeitung wiki hii limeandika juu ya hali mbaya inayoikabili mikoa minne katika Jamhuri ya Kidemokrais ya Kongo, ambako watu milioni 1.7 wamepoteza makaazi yao kutokana na vita vya wanamgambo na ukatili wa vikosi vya jeshi la serikali.

Kutokana na hali ya kutisha inayowakabili wakaazi wa mikoa hiyo, Umoja wa Mataifa umetoa wito wa kutangazwa kwa tahadhari ya juu kabisaa ya kibinadamu, ambayo imezoeleweka kwa mataifa kama Syria. Die tageszeitung linaripoti juu ya mateso na vurugu vilivyosambaa.

Likimnukuu Msemaji wa shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR, die tageszeitung linasema hakuna nchi yoyote duniani ambako watu wengi wanalaazimishwa kupoteza makazi yao kama ilivyo katika Jamhuri ya Kidemorasi ya Kongo.

Kulingana na msemaji huyo, idadi ya watu waliolaazimika kuondoka kwenye makaazi yao tangu mwaka 2015 imefikia karibu milioni mbili, na katika miezi mitatu iliopita pekee, watu 428, 000 wameyapa kisogo makaazi yao. Sababu ya yote hayo, alisema, ni kuenea kwa shughuli za wapiganaji na vile vile migogoro ya kikabila na kisiasa.

Kongo Afrika Massaker Mann sitzt vor einer ausgebrannten Hütte
Mkaazi wa Beni, Mashariki mwa Kongo akisikitika baada ya makaazi yake kuteketezwa kwa moto.Picha: Getty Images/K.Maliro

 

Vita vilivyosahaulika

Nalo gazeti la Die Welt, limeangazia vita vilivyosahaulika nchini Sudan Kusini, ambako vikosi vya serikali na waasi wanapambana vikali. Tayari vita hivyo vimegharimu maisha ya maelfu ya watu, mamilioni wanakimbia, na wafanyakazi wa misaada wanafanyakazi katika mazingira yasioweza kuelezeka, linaandika gazeti hilo.

Die Welt linasimulia kisa cha Blessing (siyo jina lake halisi), mama mjamzito alietembea kwa siku tano mfululizo, huku akiwa amebeba mtoto mwingine mgongoni, na watoto wengine wawili akiwashikilia mikono. Sauti za nyayo za miguu zinafunikwa na milio ya risasi, wakati mwingine kwa mbali na wakati mwingine kwa karibu. Huko alikotoka, aliacha kaka yake na majirani wawili wameuawa katika mapigano kati ya vikosi vya serikali na waasi.

Mbele yake, mwishoni mwa barabara ya vumbi, pengine ndiyo utakuwa mwisho wake pia. Pengine maisha yake yataokoka. Mwaka mmoja baadae, bado hajui hatma yake itakuwaje. Maisha yake yamesimamia katika kambi ya wakimbizi, katika kingo za mji mkuu wa sudan Kusini Juba.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, karibu watu milioni 3.87 walilaazimika kuyakimbia makaazi yao nchini sudan Kusini, wengi wao wakiwa wakulima wadogowadogo waliacha mashamba yao, hii ikimaanisha na maisha yao pia. Mgogoro wa Sudan Kusini unaathiri kanda nzima, linaandika Die Welt.

Rebellen in Südsudan
Waasi wa Sudan Kusini SPLAE-IO wakisimama baada ya kufanya shambulizi dhidi ya vikosi vya serikali, nje ya mji wa Kaya, katika mpaka wa nchi hiyo na Uganda.Picha: Reuters/G. Tomasevic

Mkimbizi wa milioni moja alisajiliwa nchini Uganda. Mamia kwa maelfu wamehamia Sudan, Kenya, DRC na Ethiopia. Furaha ya uhuru mwaka 2011, wakati taifa hilo changa kabisaa duniani lilipoazimisha kuundwa kwake baada ya mgogoro wa muda mrefu na Sudan, ilitoweka haraka, limesema Die Welt.

Msaada wa siri wa kijeshi Afrika

Nchini Niger, wiki hii ushiriki wa siri wa jeshi la Marekani ulifichuka baada ya maafisa wa kikosi maalumu cha jeshi la nchi hiyo kuuawa katika operesheni dhidi ya wanamgambo wa itikadi kali za Kiislamu katika eneo la Sahel.

Gazeti la Neue Zürcher limeandika kuwa vifo vya wanajeshi hao wanne vilitoa mwanga kuhusu uwepo wa kijeshi wa Marekani katika kanda ya Sahel.

Hadharani, ushiriki wa Marekani katika mapambano dhidi ya ugaidi barani Afrika haukuwa unajulikana.Lakini kufuatia vifo hivyo, na vurugu zinazoendelea kuuzonga utawala wa rais Donald Trump, masuala yameibuka kuhusu jukumu la Marekani katika eneo hilo.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/Die Welt, Neue Zürcher Zeitung, die tageszeitung, Süddeutsche Zeitung, Neues Detschland

Mhariri: Daniel Gakuba