1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

29 Septemba 2017

Wiki hii magazeti hayo yameandika juu ya wakimbizi wa Sudan Kusini waliopo nchini Uganda, upinzani mkali nchini Afrika Kusini dhidi ya kampuni ya teksi ya Uber na juu ya mabaki ya ukoloni wa Wajerumani barani Afrika.

https://p.dw.com/p/2kxKo
Uganda Bürgerkrieg und Hunger im Südsudan treiben Menschen zur Flucht
Picha: Getty Images/D. Kitwood

Gazeti la Kölner Stadt-Anzeiger wiki hii linaanza kwa kusimulia kisa cha mwanamke mmoja Sena Sadia aliyekimbia vita pamoja na wanawe. Mwanamke huyo amesimulia vipi kundi la wapiganaji walivyovamia kijiji chao na kukitia moto mumewe akapigwa risasi na yeye mwenyewe akalazimika kukimbia na kuingia Uganda kupitia njia ya mpakani. Mwanamke huyo hakuweza kunusuru chochote isipokuwa nguo alizovaa yeye na wanawe. Pamoja na yote hayo Sena Sadia anajikuta akiishi katika kambi ya wakimbizi akijaribu kuwatafutia wanawe chochote cha kuwafanya waendelee kuishi. Uganda kwa sasa inawahifadhi wakimbizi milioni 1 na laki 3 kutoka Sudan Kusini waliokimbia vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini mwao. Wakimbizi hao wanasaidiwa pia na shirika la misaada la Malteser  International kutoka mji wa Ujerumani wa Cologne. Sudan Kusini ilijipatia uhuru wake mnamo mwaka wa 2011 baada ya vita  vya muda mrefu na Sudan lakini baada ya kujipatia uhuru wake vita vya wenyewe kwa wenyewe vilizuka.  Jukumu la kuwahudumia wakimbizi hao linalotimizwa na Uganda linatambuliwa na jumuiya ya kimataifa. Shirika la misaada kutoka mji wa  Cologne la Malteser International linaisaidia Uganda katika ugavi wa maji na huduma za usafi  tangu  mwaka  wa 2013.

Der Tagesspiegel 

Gazeti hilo limendika  juu  ya  upinzani mkali dhidi ya  kampuni ya usafirishaji  Uber   iliyoanzishwa  nchini  Marekani  mnamo  mwaka wa 2009. Teksi  za kampuni  hiyo zinatoa  huduma  za  bei nafuu sana  na zimeutanuza  wigo  wake  wa  huduma hadi  nchini  Afrika Kusini. Lakini  kampuni  hiyo  inakabiliwa  na upinzani  mkali  kutoka kwa madereva  wa teksi  wa  nchi  hiyo. Juhudi  za ubunifu wenye lengo la kuleta maendeleo   zinapingwa  kwa mabavu  ya  kutumia mapanga na marungu. Kwenye mitaa  ya jiji  la Johannesburg, madereva wa kampuni  ya Uber wanaotumia tekinolojia  za kisasa, wanakabiliana  na  madereva  wa  teksi za  kawaida  wanaohofia kupoteza  ajira  zao  kutokana  na ushindani  unaosababishwa  na nauli za chini zinazotozwa na kampuni ya Uber. Mnamo mwaka huu teksi za Uber zilivamiwa kwa  ukatili  mkubwa mara zaidi ya mia tatu katika  jimbo la Gauteng na katika miji ya Johannesburg na Pretoria. Chama tawala cha ANC kimeelezea wasi wasi  mkubwa juu ya matukio hayo ya kikatili. Katika wiki za hivi karibuni matukio ya kikatili yaliendelea hadi  kufikia kiasi  cha  kuhatarisha  amani.  Waziri  Mkuu  wa  jimbo  la Gauteng  David  Makhura  amepitisha sheria  inayowataka  madereva  wa  teksi  za Uber wajiandikishe na waombe leseni ili waweze kuendesha  shughuli  zao katika  miji  ya Afrika  Kusini. Waziri  mkuu huyo  amechukua  hatua  hiyo ili  kuzuia mauaji.

Ukoloni wa Wajerumani

Gazeti la Die Welt linaeleza juu ya historia ya ukoloni wa Wajerumani ambayo ni fupi. Hakuna sehemu yoyote  barani Afrika iliyotawaliwa na Ujerumani kwa muda wa zaidi ya miaka 30. Hata hivyo katika muda  huo mfupi Wajerumani walitawala eneo ambalo lilikuwa la tatu  kwa ukubwa. Wajerumani bado hawajayasahau makoloni ya  Afrika kutokana na sababu kadhaa. Kwanza koloni lao la zamani ambalo leo ni Namibia, ndiyo nchi pekee ambako Wajerumani bado wanaendelea  kuishi  tangu enzi ya vizazi vilivyohamia wakati wa ukoloni. Wajerumani wameacha alama zao. Baadhi ya mitaa nchini Namibia bado ina majina  ya Wajerumani kama vile ya Gustav Nachtgall au Hermann Wissman hao walikuwa watafiti maarufu wa Kijerumani wa mambo ya Jiografia. Na nchini Tanzania meli ya SS Liemba bado inayakata maji kwenye ziwa Tanganyika. Meli hiyo ilipelekwa Tanganyika na Wajerumani wakati walipoitawala nchi hiyo.  

Mwandishi: Zainab Aziz/Deutsche Zeitung

Mhariri: Yusuf Saumu