1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yazuia shughuli za benki za "Hawala"

12 Aprili 2015

Magazeti ya Ujerumani yameandika juu ya hatua iliyochukuliwa na serikali ya Kenya kuzuia miamala ya fedha ya taasisi zinazotuhumiwa kuhusika na ugaidi.Pia yameandika juu ya mfano wa demokrasia barani Afrika

https://p.dw.com/p/1F6bZ
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta
Rais wa Kenya Uhuru KenyattaPicha: picture-alliance/dpa/ZUMA Press

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linasema serikali ya Kenya imeamua kuizuia miamala ya fedha ya taasisi zinazotuhumiwa kuhusika na ugaidi baada ya mashambulio yaliyofanywa na magaidi wa al-Shabaab kwenye chuo kikuu cha Garissa kaskazini mashariki mwa Kenya. Watu zaidi ya 140 waliuawa kutokana na mashambulio hayo.

Gazeti hilo linaeleza kwamba hatua iliyochukuliwa na serikali ya Kenya kuzifunga shughuli za kutuma fedha baina ya Kenya na Somalia ni pigo kubwa kwa watu nchini Somalia. Gazeti hilo limeeleza kuwa taasisi hizo ni zile zinazoitumia Kenya kama makao kwa ajili ya kuendeshea shughuli zao ndani ya Somalia.

Taasisi za "Hawala"


Gazeti la "Frakfurter Allgemeine" linasema kwa watu wengi nchini Somalia njia pekee ya kupatia fedha ni kutuma fedha kupitia taasisi taasisi za "Hawala". Mtumaji anapeleka fedha tasilimu kwenye taasisi hizo nchini Kenya na mpokeaji anazichukua nchini Somalia. Gazeti hilo limeeleza kwamba mfumo wa mabenki rasmi haufanyi kazi kwa kiwango kinachohitajika nchini Somalia.

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" limezikariri taarifa za mashirika ya kimataifa yanayokadiria kwamba dola Bilioni 1.6 zinapelekwa nchini Somalia kila mwaka kwa njia ya benki za "Hawala"

Mafunzo juu ya demokrasia kutoka Nigeria

Gazeti la "Die Zeit" linasema Nigeria imetoa mafunzo barani Afrika kwa kufanya uchaguzi wa amani na kuleta mabadiliko ya uongozi bila ya mushkeli wowote.

Gazeti hilo linaeleza kwamba Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria amefanya kitu ambacho si cha kawaida barani Afrika. Amekubali kushindwa katika uchaguzi na alimpongeza mshindani wake Muhammadu Buhari alieshinda uchaguzi.

Gazeti la "Die Zeit" linasema huo ni ujumbe kwa bara lote la Afrika na hasa kwa viongozi kama Robert Mugabe,wa Zimbabwe, Yoweri Museveni wa Uganda na Jose Edoardo dos Santos wa Angola. Gazeti la "Die Zeit" linasema viongozi hao waliokaa madarakani kwa muda mrefu kwa kutumia hila za namna mbalimbali hawawezi kuupuuza ujumbe huo kutoka Nigeria.

Maiti zaidi ya 400 zagunduliwa katika kaburi moja

Gazeti la "die tageszeitung" limezikariri habari juu ya kugunduliwa kaburi lililokuwa na maiti 425 karibu na Kinshasa, mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Gazeti hilo limefahamisha kwamba maiti 421 zilizikwa katika kaburi moja katika wilaya ya Maluku ya mji wa kinshasa. Maiti 300 zilikuwa za vijusi na watoto wachanga waliozaliwa wafu. Serikali ya Kongo imesema haina kitu cha kuficha juu ya maiti hizo, ili kakanusha uvumi kwamba maiti hizo ni za wapinzani wa serikali waliouliwa.

China yajiimarisha katika mambo ya habari barani Afrika

Gazeti la "Der Tagesspiegel" wiki hii limeandika juu ya juhudi za China za kujiiimarisha katika madhari ya vyombo vya habari barani Afrika. Gazeti hilo linasema China inaibadilisha sura ya vyombo vya habari barani Afrika.

Gazeti la "Der Tagesspiegel" linaeleza kwamba mkakati wa China ulianza mnamo mwaka wa 2008 baada ya mashindano ya michezo ya Olimpiki mjini Beijing. Tokea wakati huo shirika la habari la China "Xinhua" limeshafungua ofisi 30 za waandishi habari wake 60 barani Afrika.

Gazeti la "Der Tagesspiegel" linafahamisha kuwa fahari ya China katika tasnia ya vyombo vya habari, barani Afrika ni televisheni ya serikali inayoitwa, CCTV Africa. Mnamo mwaka 2011 shirika hilo la televisheni lilifungua ofisi kubwa sana mjini Nairobi. Kwa mujibu wa hilo serikali za nchi za Africa na China zinakubaliana kwamba jukumu la vyombo vya habari ni kuripoti juu ya mafanikio ya jamii.

Mwandishi:Mtullya Abdu.Deutsche Zeitungen.

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman