1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Abdu Said Mtullya7 Septemba 2014

Wiki hii magazeti ya Ujerumani yanatukumbusha kwamba yapo magonjwa mengine hatari barani Afrika. Magazeti hayo pia yanazungumzia juu ya athari za kampuni kubwa kuchukua ardhi ya kilimo barani Afrika

https://p.dw.com/p/1D8Ic
Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Donald Kaberuka asema biashara yaweza kuendelea licha ya Ebola
Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Donald Kaberuka asema biashara yaweza kuendelea licha ya EbolaPicha: picture-alliance/dpa/J. Relvas

Gazeti la "Neues Deutschland linatukumbusha kwamba barani Afrika yapo maradhi na matatizo mengine makubwa licha ya Ebola.Gazeti hilo linaeleza kwamba kutokana na mkazo kuwekwa juu ya maradhi ya Ebola magonjwa na matatizo mengine yanagubikwa.

Linaripoti kwamba kila siku akina mama waja wazito wanapiga hodi kuomba msaada kwenye kituo cha dharura kinachoongozwa na madaktari wasiojali mipaka katika mji mkuu wa Liberia ,Monrovia. Lakini kutokana na tahadhari juu ya ugonjwa wa Ebola kituo hicho na hospitali karibu zote zimefungwa ili kuzuia maambukizi.

Wajawazito wapuuzwa

Gazeti la "Neues Deutschland" limemnukuu mfanyakazi mmoja akisema kuwa matokeo ya kuweka mkazo mkubwa sana juu ya maradhi ya Ebola ni kupuuzwa magonjwa mengine kama vile malaria na shida za akina mama wajawazito.

Mkurugenzi wa harakati za mashirika ya kimataifa Mariono Lugli amenukuliwa na gazeti la "Neues Deutschland" akisema kuwa wanawake wengi wanajifungua majumbani mwao bila ya msaada wa wataalamu . Mkurugenzi huyo amesema watoto wengi wanakufa panapotekea matatizo.

Ebola yaathiri uchumi

Gazeti la "Der Tagesspigel" linazizingatia athari za kiuchumi zinazotokana na maradhi ya Ebola barani Afrika. Gazeti hilo linasema Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika,ADB Donald Kaberuka sasa anacho kibarua kigumu cha kujaribu kuwapa imani washirika wa biashara wa nchi za Afrika .

Bwana Kaberuka amesema kwamba washirika wa biashara wa Afrika wanaweza kuendelea kufanya biashara barani Afrika.Gazeti la "Der Tagesspiegel" linatufahamisha kuwa maadhara tayari ni makubwa katika uchumi wa nchi zilizokumbwa na maambukizi ya Ebola.

Na kutokana na hali hiyo Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Donald Kaberuka amefanya ziara katika nchi hizo wiki iliyopita.Bwana Kaberuka amenukuliwa akisema kuwa maradhi ya Ebola ni ya hatari kubwa lakini hiyo isiwe sababu ya shughuli za kiuchumi kusimama. Hata hivyo gazeti la "Tagesspiegel" limeripoti kwamba ustawi wa uchumi umepungua katika nchi zilizokumbwa na baa la Ebola.

Miradi ya kilimo ya kampuni za kimataifa ni tishio kwa wakulima wadogo wadogo

Gazeti la "die tageszeitung" limechapisha makala juu ya miradi mikubwa ya kilimo inayotekelezwa na kampuni kubwa za kimataifa barani Afrika. Gazeti hilo limeikariri ripoti ya shirika la misaada la Oxfam ikisema kuwa miradi hiyo inatishia upatikanaji wa chakula kwa wananchi katika nchi mbalimbali za Afrika.

Gazeti hilo limeripoti kwamba mfanyakazi mmoja wa shirika la misaada la Oxfam David Hachfield amesema wananchi wanaporwa ardhi yao na kutolewa kwa ajili ya kilimo cha miwa nchini Malawi.Kampuni ya ubia ya Afrika Kusini na Uingereza Illovo inalima shamba kubwa la miwa nchini humo.Wakulima wazawa wenyewe hawana tena ardhi ya kulimia.

Serikali ya Ujerumani nayo yashiriki

Gazeti la "die tageszeitung" limearifu kwamba sasa upo mtindo mpya wa miradi ya kilimo barani Afrika. Gazeti hilo linasema katika nchi kama Tanzania, Malawi na Burkina Faso serikali zinatoa sehemu kubwa za ardhi kwa kampuni za nje.Gazeti hilo limesema kampuni hizo zinasaidiwa na serikali za nchi zao katika miradi ya kuzalisha chakula barani Afrika.

Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na shirika la misaada Oxfam nchini Malawi, shughuli za makampuni hayo makubwa haziifanyi hali ya upatikanaji wa chakula iwe bora kwa wananchi, chini ya mradi unaoitwa "ubia binafsi na wa umma" unaoungwa mkono pia na serikali ya Ujerumani. Kwa mujibu wa gazeti la "die tageszeitung" Ujerumani hadi sasa imeshakubali kutoa msaada wa Euro Milioni 300 kwa nchi za Afrika zinazoshiriki katika mradi huo wa ubia na kampuni za nje.

Mwandishi:Mtullya Abdu.Deutsche Zeitungen.

Mhariri: Josephat Charo