1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ebola

Abdu Said Mtullya31 Agosti 2014

Wiki hii magazeti ya Ujerumani yameandika juu ya matumaini ya kumshinda adui Ebola, na juu ya hatari inayotokana na uhaba wa maji katika nchi zinazoendelea ikiwa pamoja na barani Afrika.

https://p.dw.com/p/1D4KB
Mapambano dhidi ya Ebola
Mapambano dhidi ya EbolaPicha: picture-alliance/dpa

Gazeti la "Berliner Zeitung" limeandika juu ya maradhi ya Ebola yanayozidi kuenea barani Afrika. Gazeti hilo linatahadharisha kwamba kasi ya kuenea maradhi hayo hakijulikani kwa uhakika.

Gazeti hilo linasema kana kwamba vifo vya watu zaidi ya1500 katika nchi za Afrika magharibi kutokana na Ebola havitoshi,ugonjwa huo sasa umeingia katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Gazeti hilo linaarifu kwamba mpaka sasa watu 70 wameshakufa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Gazeti la "Berliner " linatilia maanani kwamba hii ni mara ya saba kwa maradhi ya Ebola kutokea katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Mara ya kwanza ugonjwa huo ulizuka mnamo mwaka wa 1976 nchini humo.

Matumaini ya kumshinda adui Ebola

Gazeti la "Neues Deutschland" limeandika juu ya matumaini ya kupatikana tiba ya Ebola kutoka Japan. Gazeti hilo linatuambia kwamba yawezekana Japan ikawa na dawa ya kuyatibu maradhi hayo.

Linaeleza kuwa dawa ya kuyatibu mafua makali inayoitwa Avigan kutoka Japan imeshatumika kwa ajii ya kuwatibu wanyama na imesaidia. Pamoja na hayo dawa hiyo ipo ya kutosha. Hata hiyvo gazeti la "Neues Deutschland" linasema kuwa uwezo wa dawa ya Avigan kutoka Japan bado haujathibitishwa.Lakini linaarifu kuwa binadamu wanaweza kuitumia dawa hiyo bila ya matatizo yoyote

.Madhali Shirika la Afya Duniani WHO limesema kuwa ni sahihi kuzitumia dawa ambazo bado hazijajaribiwa kwa binadamu, Japan imesema ipo tayari kuzitoa dawa hizo kwa Shirika hilo na kwa kila nchi itakayotoa maombi.

Tumbaku: dawa ya Ebola

Na kutoka mji wa Halle mashariki mwa Ujerumani, gazeti la "Super Illu" limeleta taarifa ya matumaini juu ya kupambana na maradhi ya Ebola.Kwa mujibu wa gazeti hilo kampuni ya Icon Genetics ya mji huo imegundua kwamba huenda tumbaku ikawa dawa ya kuyatibu maradhi ya Ebola. Gazeti la "Superr Illu" linatufahamisha kwamba Kampuni ya Icon Genetics kutoka mji wa Halle ina ustadi wa kutengeneza dawa kutokana na mimea.

Na tumbaku ndiyo msingi wa dawa ya ZMapp.Dawa hiyo inayotengenezwa nchini Marekani bado imo katika hatua za majaribio lakini tayari imeshayaokoa maisha ya Wamarekani wawili waliokuwa wameambukizwa maradhi ya Ebola.

Na hali za watu wengine watatu sasa ni nzuri baada ya kutibiwa na dawa hiyo ya ZMapp.Na kwa hivyo, gazeti la "Super Illu" linasema matumaini yamo katika tumbaku inayopandwa na kampuni hiyo ya Icon Genetics ya mjini Halle mashariki mwa Ujerumani.

Uhaba wa maji ni hatari

Maji yanazidi kuwa haba duniani na hasa katika nchi zinazondelea ikiwa pamoja na barani Afrika. Hizo ni habari zilizoandikwa na gazeti la biashara la "Handelsblatt" Gazeti hilo limeripoti kwamba Shirika la hifadhi ya mazingira WWF limetahadharisha juu ya hali hiyo inayosababisha mivutano kati ya jamii mbalimbali.

Gazeti la "Handelsblatt" linatufahamisha zaidi kwamba serikali ya jimbo la India la Uttar Pradesh imetoa agizo la kuifunga mitambo ya maji baada ya wakulima kulalamika kwamba maji yanazidi kuwa haba.Sababu ni kwamba Kampuni ya Cocacola inatumia kiasi kikubwa sana cha maji. Kwa mujibu wa taarifa ya gazeti la "Handelsblatt " uhaba wa maji unafanya baishara iwe ngumu.

Gazeti la "Handelsblatt" limeikariri ripoti ya Shirika la hifadhi ya mazingira na wanyama pori WWF ikisema kuwa nchi kama Afrika ya Kusini ni eneo lenye uhaba mkubwa wa maji. Siyo tu kwamba maji ni haba nchini humo bali ni ya kiwango duni. Gazeti la "Handelsblatt" limeikariri ripoti ya shirika la WWF ikisema kuwa uhaba wa maji unasababishwa na ufujaji wa makampuni makubwa kama Cocacola katika matumizi ya raslimali hiyo.

Mwandishi:Mtullya abdu./Deutsche Zeitungen.

Mhariri:Yusuf Saumu