1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Abdu Said Mtullya21 Machi 2014

Magazeti ya Ujerumani wiki hii yameandika kuhusu uamuzi wa Ujerumani wa kuwapeleka wanajeshi Somalia ili kutoa mafunzo. Pia yameandika juu ya mwanaharakati anaetetea haki za mashoga nchini Kameruni.

https://p.dw.com/p/1BU4o
Askari wa kulinda amani Somalia
Askari wa kulinda amani SomaliaPicha: Bundeswehr

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" limeandika juu ya uamuzi wa baraza la mawaziri wa Ujerumani wa kuwapeleka wakufunzi wa kijeshi 20 nchini Somalia. Gazeti hilo linamefahamisha kwamba wanajeshi wa Ujerumani tayari wameshariki katika mpango wa kutoa mafunzo kwa wanajeshi wa Somalia uliotekelezwa nchini Uganda. Lakini sasa mpango huo wa mafunzo yanayotolewa katika ngazi ya Umoja wa Ulaya utatekelezwa katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu.

Lengo la mafunzo hayo ni kuwawezesha wanajeshi wa Somalia kuleta na kuuimarisha usalama wa nchi yao. Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" limearifu zaidi kwamba wanajeshi wa Ujerumani pia watatoa ushauri kwa wizara ya ulinzi ya Somalia.Hata hivyo uamuzi wa baraza la mawaziri wa Ujerumani unahitaji ridhaa ya Bunge.

Hoteli yashambuliwa

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" pia limechapisha taarifa juu ya kushambuliwa kwa hoteli katika mji wa Bulobarge mwanzoni mwa wiki hii. Kwa mujibu wa taarifa hiyo watu 14 waliuawa na wengine 24 walijeruhiwa. Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" limezikariri taarifa zilizosema kuwa wapiganaji wa al-Shabaab walilifanya shambulio hilo kwenye hoteli hiyo inayowahudumia hasa wanajeshi wa serikali na askari wa Umoja wa Afrika wanaolinda amani nchini Somalia.

Haki za mashoga

Gazeti la "die tageszeitung" limechapisha makala juu ya mwanaharakati anaezitetea haki za mashoga nchini Kameruni. Mwanaharakati huyo Alice Nkom ambae pia ni mwanasheria alitunukiwa tuzo ya haki za binadamu na Shirika la kutetea haki za binadamu, Amnesty International tawi la Ujerumani. Alice Nkom alikabidhiwa tuzo hiyo mjini Berlin Jumanne iliyopita kama ishara ya kutambua mchango wake katika harakati za kutetea haki zamashoga nchini Kemeruni.

Hata hivyo gazeti la "die tageszetung"linaeleza katika makala yake kwamba mtu yeyote anaejaribu kuwatetea watu wanaofanya mapenzi ya jinsia moja barani Afrika,aghalabu husimama peke yake kama mchawi. Gazeti hilo linasema mtu kama huyo huonekaka kuwa amesimama nje ya utamaduni wa Afrika.

Zuma matatani tena

Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini anatakiwa alipe sehemu ya kiasi cha dola Milioni 21 zilizotumiwa kwa ajili ya kuifanyia nyumba yake ukarabati .Mwendesha mashataka wa serikali amesema kwamba Rais Zuma alitumia fedha za serikali kwa ajili ya nyumba hiya . Hizo ni habari nyingine zilizochapishwa wiki hii na gazeti la "Frankfurter Allgemeine" Gazeti hilo linaarifa zaidi kwamba Rais Zuma ametumia fedha za walipa kodi kuikarabati nyumba yake katika mji wa Nkandla uliopo katika jimbo la Kwa Zulu Natal. Mji wa Nkandla ni miongoni mwa sehemu masikini sana katika jimbo la kwa Zulu ambako shughuli kubwa inayowaingizia watu kipato ni ya uvuvi.

Rais waikimbia nchi yao,Eritrea

Gazeti la "Neues Deutschland" limeripoti juu ya hali ya nchini Eritrea. Limefahamisha kwamba watu 3000 wanaikimbia nchi yao kila mwezi.

Gazeti la "Neues Deutschland" linaarifu kwamba watu wa Ertitrea wanaukimbia mkono wa chuma wa kiongozi wao Isaias Afewerki.Raia wa Eritrea wanazikimbia kambi za kazi ngumu wanazolazimishwa kuzifanya. Gazeti hilo linaeleza kwamba watu wa Eritrea waliupigania uhuru wao kwa kujitoa mhanga kwa kiasi kikubwa lakini bado hawajaupata uhuru huo.

Gazeti la "Neues Deutschland" limeripoti kwamba haki za binadamu zinakiukwa kwa kiwango kikubwa nchini Eritrea ambako hakuna katiba, wala mahakama huru. Gazeti hilo limefahamisha zaidi kwamba hakuna uchaguzi unaofanyika katika nchi hiyo iliyopo mashariki mwa Afrika na kwamba mamlaka yote yamo katika mikono ya mtu mmoja- Isaias Afewerki.

Gazeti la "Neues Deutschland"limeikariri ripoti ya Umoja wa Mataifa inayoarifu kwamba watu 3000 wanaondoka Eritrea kila mwezi ili kukwepa kulazimishwa kulitumikia jeshi.


Mwandishi: Abdu Mtullya/Deutsche Zeitungen

Mhariri: Mohammed Khelef