Afrika katika magazeti ya Ujerumani
3 Januari 2014Gazeti la "die tageszeoitung limeandika juu ya mgogoro wa Sudan ya Kusini. Kattika makala yake gazeti hilo linasema sasa matumaini ya kuumaliza mgogoro huo yamo katika mikono ya viongozi wa serikali ya Sudan na ya waasi.
Gazeti hilo limeandika katika makala yake kwamba pande zinazohusika na mgogoro zimekubali kufanya mazungumzo juu ya njia za kuutatua. Lakini wakati huo huo mapigano bado yanaendelea.
Gazeti la "Süddeutsche " pia limeandika juu ya mgogoro wa Sudan ya Kusini.Gazeti hilo linatilia maanani katika makala yake kwamba waasi wapo tayari kufanya mazungumzo na serikali juu ya kusimamisha mapigano.
Yoweri Museveni atoa changamoto
Gazeti la "Süddeutsche" linasema yumkini ni kutokana na shinikizo kutoka nje kwamba kiongozi wa waasi Riek Machar amekubali kufanya mazungumzo juu ya kusimamisha mapigano. Gazeti hilo limemnukuu Rais Yoweri Museveni wa Uganda akisema kwamba nchi za Afrika Mashiriki zitakuwa tayari kuingilia kati kijeshi katika Sudan ya Kusini ikiwa waasi hatawatakubali kusimamisha mapigano.
Heshima na wajibu kwa Ufaransa
Gazeti la "Neues Deutschland" linauzungumzia mgogoro wa Jamhuri ya Afrika ya Kati katika muktadha wa kuhusika kwa Ufaransa Gazeti la "Neues Deutschland" limemnukuu Rais Francois Hollande wa Ufaransa akisema katika salamu za mwaka mpya kwa wananchi wake kwamba, ni wajibu na pia ni heshima kwa Ufaransa kuchukua hatua ili kurejesha amani katika Jahmuri ya Afrika ya Kati na kuzuia mauaji ya watoto.
Hata hivyo katika makala yake gazeti la "Neues Deutschland" linatilia maanani kuwa mpaka sasa majeshi ya Ufaransa yanashindwa kuzuia hali kwenda mrama katika Jamhuri ya Afrika ya Kati. Gazeti hilo linafahamisha kwamba Ufaransa ina askari 1,600 tu, katika nchi yenye ukubwa ,sawa na eneo la Ufaransa na Ubelgiji kwa pamoja.
"Magaidi" wazimwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo
Gazeti la "die tageszeitung" limechapisha taarifa juu ya mkasa uliotokea mjini Kinshasa wiki iliyopita. Athari za kilichotuhumiwa kuwa jaribio la kuiangusha serikali katika Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo ni kubwa zaidi kuliko ilivyoripotiwa hapo awali. Gazeti la "die tageszeitung" limeikariri taarifa ya serikali iliyosema kuwa, idadi ya wale walioitwa magaidi, waliouliwa na majeshi ya serikali ilifikia 95. Hapo awali taarifa zilisema kuwa ni 34 tu waliouawa.
Gazeti la "die tageszeitung" linatufahamisha zaidi juu ya mkasa huo kwa kuarifu kwamba watu waliokuwa na silaha jumatatu ya wiki iliyopita walikivamia kituo cha televisheni ya taifa ,pia waliuvamia uwanja wa ndege na makao makuu ya jeshi mjini Kinshasa.
Ndovu wa Afrika waangamizwa
Mwanzoni mwa mwezi wa Oktoba,ulifanyika uhalifu mkubwa katika mbuga ya taifa ya wanyama ya Hwange nchini Zimbabwe.Ndovu zaidi ya mia tatu walitiliwa sumu .Hizo ni habari zilizoripotiwa na gazeti la "Berliner Zeitung."Gazeti hilo linasema katika taarifa yake kwamba ndovu hao waliangamizwa kwa sababu ya pembe zao.
Gazeti hilo limefahamisha kwamba wanunuzi wa pembe hizo wako nje ya Afrika,na hasa China. Gazeti la "Berliner Zeitung" linasema katika taarifa yake kwamba kilichotokea Zimbabwe ni sehemu ndogo tu ya uhalifu mkubwa uliolikumba bara zima la Afrika. Limeikariri ripoti ya shirika la uhifadhi wa wanyama pori duniani WWF inayothibisha kwamba katika mwaka uliopita pekee,tembo alfu 30 waliangamizwa barani Afrika.
Mwandishi:Mtullya Abdu./Deutsche Zeitungen.
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman