1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Abdu Said Mtullya4 Oktoba 2013

Wiki hii magezeti ya Ujerumani yameandika juu ya maafa yaliyotokea karibu na kisiwa cha Italia cha Lampedusa,mashambulio ya magaidi wa al-Shabaab jijini Nairobi na juu ya tuzo iliyotolewa kwa mtawa wa Kongo.

https://p.dw.com/p/19txT
Mamia ya wakimbizi wafa maji karibu na kisiwa cha Italia cha Lampedusa
Mamia ya wakimbizi wafa maji karibu na kisiwa cha Italia cha LampedusaPicha: picture-alliance/dpa

Mamia ya wakimbizi kutoka Afrika wamekufa maji baada ya mashua yao kuzama kwenye bahari ya Mediterania. Watu hao walikuwa njiani kulekea barani Ulaya ili kutafuta maisha bora. Juu ya maafa hayo gazeti la die tageszeitung limeandika maoni kusema kwamba mzigo wote wa lawama juu ya maafa hayo unastahili kubebwa na nchi za Umoja wa Ulaya.

Gazeti hilo linasema nchi zote za Umoja wa Ulaya zimejiwajibisha kuwapa hifadhi ya ukimbizi watu wanaoandamwa. Lakini ni vigumu kwa watu hao kuitumia haki hiyo. Linasena idadi kubwa ya watu waliokufa maji karibu na kisiwa cha Italia cha Lampedusa walitoka katika nchi zenye migogoro.Ndiyo kusema walistahiki kupata hifadhi ya ukimbizi barani Ulaya .Lakini njia ya kufikia kwenye haki hiyo imefungwa kwa sababu mipaka ya nchi za Ulaya inalindwa na askari.

Pamoja na hayo gazeti linasema mipaka hiyo inalindwa na sheria ya kuwaadhibu watu kama wavuvi au manahodha wa meli za mizigo wanaojaribu kuwasaidia watu wanaofikwa na matatizo baharini.Gazeti la "die tageszeitung" linaeleza katika maoni yake kwamba yeyote anaejaribu kuwasaidia wakimbizi anajitia katika hatari ya kufunguliwa mashtaka ya kufanya biashara ya kuwauza watu.Gazeti hilo linasema wale wanaojaribu kuwasaidia watu waliomo hatarini baharini hawapaswi kuandamwa na sheria. Gazeti la "die tageszeitung" limezitaka nchi za Umoja wa Ulaya ziifungue milango yao kwa watu wanaotafuta hifadhi ,la sivyo vifo vitaendelea.

"Idara za Kenya zilitahadharishwa"

Gazeti la "Berliner Zeitung" limechapisha makala juu ya mkasa wa kuvamiwa kwa jengo la biashara na magaidi wa al-Shabaab katika jiji la Nairobi.Katika makala hiyo gazeti la "Berliner "limezikariri taarifa zinazosema kuwa idara husika za Kenya zilitahadharishwa juu ya hatari ya kutokea mashambulio ya kigaidi katika sehemu kadhaa. Gazeti hilo pia limeeleza kuwa uchunguzi uliofanywa na wandishi habari mbalimbali umeonyesha kuwa magaidi wa al-Shabaab walikodisha duka moja katika sehemu ya biashara, miezi mitatu kabla ya kufanya mashambulio.

Mtawa Angelique Namaika

Mtawa Angelique Namaika,ametunukiwa tuzo ya mwaka huu ya Nansen ya shirika la Umoja wa Mataifa linalowashughulikia wakimbizi UNHCR Gazeti la "die tageszeitung" Gazeti limeandika habari hizo na limetilia maanani kwamba mtawa huyo Namaika ametunukiwa nishani hiyo kutokana na juhudi zake za kuwasaidia wanawake walionyanyaswa nchini mwake. Mtawa huyo anakiongoza kituo kilichopo kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo,cha kuwasaidia wanawake na wasichana kurejea tena katika jamii, baada ya kutendewa uhalifu ,kama vile wa kubakwa au kushambuliwa na makundi ya waasi.

Gazeti la "die tageszeitung" limesema kwamba pamoja na kuwasaidia wanawake hao kuondokana na majeraha ya rohoni sista Angelique Namaika anawasaidia akina mama hao kujipatia ujuzi wa kazi za mikono.

Mbio za marathoni

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" limeandika juu ya mwanariadha Wilson Kipsang alievunja rekodi ya dunia katika mbio za marathoni mjini Berlin. Mwanariadha huyo wa Kenya alitumia muda wa saa 2 dadika tatu na sekunde 23. Ushindi huo umemweka katika jamii ya wanariadha mashuhuri wa Kenya kama Paul Targat ambae miaka 10 iliyopita pia alivunja rekodi ya dunia katika mbio za marathoni mjini Berlin. Gazeti la " Frankfruter Allgemeine" limeandika katika makala yake kwamba "Wilson Kipsang amesema anamshukuru Targat kwa mafanikio yake kwani Targat ni kocha wake wa michezo na wa maisha.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen:

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman