Afrika katika magazeti ya Ujerumani
1 Septemba 2013Magazeti hayo pia yameandika juu ya kuanguka kwa vijana zaidi ya alfu 25 katika mtihani wa kuingia katika chuo kikuu.
Gazeti la "Süddeutsche Zeitung"linaizingatia hali ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Gazeti hilo limeanza makala yake kwa kusema, "dawa ya moto ni moto."Linasema kwamba kwa mara ya kwanza askari wa Umoja wa Mataifa waliowekwa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo wameingia katika mapambano na waasi. Gazeti hilo limearifu kwamba wiki iliyopita jeshi la Umoja wa Mataifa liliwasaidia wanajeshi wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo katika mapambano dhidi ya waasi wa M23.
Gazeti la"Süddeutsche" limemkariri mkuu wa uwakilishi wa Umoja wa Mataifa,Monusco nchini Kongo,Martin Kobler akithibitisha kwamba jeshi la Umoja wa Mataifa lilitoa msaada wa mizinga na helikopta kwa majeshi ya serikali ya Jamhuri ya Kidemokarasi ya Kongo.
Mambo sasa kuwa magumgu kwa waasi:
Nalo gazeti la "die tageszeitung" limechapisha mahojiano juu ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na mtaalamu kutoka taasisi ya mazingira ya Ujerumani,Bwana Andreas Manhart aliesema katika mahojiano hayo kwamba sasa mambo ni magumu kwa waasi. Katika mahojiano hayo bwana Manhart alifafanua juu ya sheria ya kudhibiti madini yanayotoka katika maeneo ya migogoro kama mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.
Bwana Manhart ameeleza zaidi,katika mahojiano na gazeti la "die tageszeitung" kuwa lengo la sheria hiyo ya Marekani inayoitwa "Dodd-Frank Act" ni kudhibiti upatikanaji na uuzaji wa madini yanayotoka katika maeneo ya mizozo kama mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ili kuchangia katika juhudi za kuleta amani.Mtaalamu huyo kutoka taasisi ya mazingira ya Ujerumani bwana Manhart ameeleza katika mahojiano kwamba makundi ya waasi ya mashariki mwa Kongo yanajigharamia kutokana na mauzo ya madini.Lakini kutokana na sheria hiyo, sasa mambo yamekuwa magumu kwao.
Sheria ya Dodd-Frank ilipitishwa na bunge la Marekani mnamo mwaka wa 2010 baada ya malalamiko ya watetea haki za binadamu nchini Marekani kwamba madini yanayotoka katika maeneo ya migogoro yanaingiza fedha zinazotumika kwa ajili ya kuendeleza migogoro.
Bustani ya Mugabe kugharimu mamilioni:
Gazeti la "Süddeutsche Zeitung" wiki hii pia limechapisha makala juu ya Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe. Rais huyo anao mpango wa kujenga bustani ya burudani thamani ya Euro zaidi ya Milioni 220 kwenye maporomko ya Victoria.
Gazeti hilo linasema inapasa kutilia maanani kuwa uchumi wa Zimbabwe ulianguka sana na kusababisha mfumuko wa bei ambao hakuwa na mithili katika historia ya hivi karibuni duniani. Sekta ya utalii pia ilianguka,kwa sababu watalii wa kimataifa walijiweka mbali na Zimbabwe, lakini siyo kwa sababu kwenye maporomoko ya Victoria hakuna maduka,klabu za burudani au sehemu za kuchezea kamari!
Gazeti la "Süddeutsche" linasema hata ikiwa mradi huo wa bustani ya burudani utakamilika,utakuwa kichekesho katika muktadha wa hali ya Zimbabwe kwa jumla.
Maalfu waanguka mtihani Liberia:
Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linaripoti juu ya vijana ,25,000 walioanguka mtihani wa kuingia chuo kikuu nchini Liberia. Gazeti la"Frankfurter Allgemeine" linatufahamisha kwamba vijana hao walifanya mtihani wa lugha ya kiingereza lakini wote walishindwa. Gazeti hilo limemnukuu waziri wa elimu akisema kuwa jamii inapaswa kuubeba mzigo unaotokana na mazingira halisi ya kijamii yaliyosababishwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe Hata hivyo gazeti limemkariri mkuu wa chuo akisema sasa inapasa kutambua hali halisi iliyopo, kwani vita vilimalizika miaka 10 iliyopita nchini Liberia .
Mwandishi:Mtullya Abdu/ Deutsche Zeitungen
Mhariri: Mohammed Khelef