1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Abdu Said Mtullya11 Machi 2013

Wiki hii magazeti ya Ujerumani yameandika juu ya mpasuko katika kundi la waasi la M23, na juu ya taarifa za kuuawa kwa kiongozi wa al -Qaeda nchini Mali.

https://p.dw.com/p/17uiF
Wanajeshi wa Ufaransa nchini Mali
Wanajeshi wa Ufaransa nchini MaliPicha: Getty Images

Gazeti la"die tageszeitung"limeandika juu ya mpasuko uliotokea katika kundi la waasi wa M23.Gazeti hilo linasema katika makala yake kwamba waasi hao walipambana na kuuana wenyewe kwa wenyewe.

Gazeti hilo linakumbusha kwamba mnamo mwezi wa Juni mwaka jana waasi wa M23 waliuteka mji wa Bunagana mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Waasi hao waliweka utaratibu wao wa utawala katika sehemu hiyo.Lakini sasa utawala huo unaelekea kusambaratika.

Gazeti la"die tageszeitung" limearifu katika makala yake kwamba mkuu wa tawi la kijeshi,Sultani Makenga amemtimua mkuu wa tawi la kisiasa Jean Marie Runige .Sababu ni kwamba Runige anashirikiana na kiongozi wa waasi wa hapo awali Bosco Ntaganda anaesakwa na Mahakama Kuu ya Kimataifa ya mjini The Hague ICC

Kiongozi wa Al-Qaeda auawa.

Gazeti la"Frankfurter Allgemeine" limechapisha makala yenye kichwa cha habari kinachosema" Belmokhtar auawa. Huyo ni kiongozi wa mtandao wa Al-Qaeda katika Afrika ya Kaskazini. Gazeti hilo limeripoti kuwa jeshi la Chad limearifu kwamba viongozi wawili muhimu wa mtandao wa Al-Qaeda katika Afrika ya Kaskazini wameuawa nchini Mali.Viongozi hao ni Abdelhamid Abu Zaid na Mokhtar Belmokthar. Belmokhtar alihusika na kutekwa nyara kwa wafanyakazi kwenye kiwanda cha uzalishaji gesi nchini Algeria mnamo mwezi wa januari. Wafanyakazi 40 ambao walikuwa raia wa nje waliuawa. Hata hivyo gazeti la "Frankfurter Allgemeine" limeeleza kuwa habari juu ya kuuawa kwa magaidi hao wawili bado hazijathibitishwa kwa uhakika.

Gazeti la "Die Zeit" pia linauzungumzia mgogoro wa nchini Mali.Linasema katika makala yake kwamba mgogoro huo utachukua muda mrefu.Linaeleza katika makala hiyo kwamba mashikamano baina ya Ufaransa na waasi wa Kitaureg unakwamisha juhudi za kuleta maridhiano ya kitaifa nchini Mali.

Gazeti la "Die Zeit" linaeleza kuwa majeshi ya Ufaransa yanashirikiana na waasi wa kitaureg wa MNLA katika jimbo la Kidal kaskazini mwa Mali ambako mapambano makali yanatokea.Gazeti la "Die Zeit" linaeleza kuwa wapiganaji wa kitaureg wanayajua vizuri mandhari ya kaskazini mwa Mali kwa hiyo wao ni msaada mkubwa kwa majeshi ya Ufaransa. Lakini gazeti la "Die Zeit" linasema ushirikiano baina ya majeshi ya Ufaransa na waasi wa kitaureg walioiteka Mali ya kaskazini mwanzoni kabisa,siyo jambo sahili.

Gazeti hilo linakumbusha kwamba wapiganaji hao wa kitaureg walitenda uhalifu kaskazini mwa Mali.Hali hiyo inazifanya juhudi za kuleta maridhiano ya kitaifa ziwe ngumu nchini Mali.

Siku njema za Afrika zaja:


Murugenzi la shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia maendeleo ya viwanda Philippe Scholtes amesema kuwa sekta ya biashara ya kilimo inaweza kuwaondoa Waafrika wengi kutoka kwenye umasikini.Hizo ni habari zilizoandikwa na gazeti la "Neues Deutchland"wiki hii. Gazeti hilo limemkariri Mkurugenzi wa UNIDO Bwana Scholtes akisema kwamba Hadi mwanzoni mwa karne hii,hapakuwa na vitega uchumi katika sekta ya biashara ya kilimo Lakini amesema katika muda wa miaka mitatu iliyopita ,wajasiramali wameweka vitega uchumi thamani ya mabilioni ya dola.

Sekta hiyo ya biashara ya kilimo inaweza kuondoa umasikini barani Afrika. Mkurugenzi wa UNIDO Scholtes ameliambia gazeti la "Neues Deutschland" kwamba bara la Afrika limepata ustawi mkubwa kutokana na maliasilia kama mafuta na madini. Hata hivyo amesema utajiri unaotokana na maliasilia hizo unaingia katika mifuko ya wachache.Lakini gharama za maisha zinapopanda, ni wote wanaothirika katika jamii. Mkuregenzi huyo ameliambia gazeti la"Neues Deutschland"kwamba sekta ya biashara ya kilimo itawanufaisha wengi barani Afrika, kwa bidhaa zitaongezewa thamani kabla ya kuuzwa nje.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri:Yusuf Saumu