Afrika katika magazeti ya Ujerumani
18 Januari 2013Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" limechapisha taarifa juu ya mgogoro wa nchini Mali. Gazeti hilo linasema katika taarifa yake kwamba Ufaransa inayaimarisha majeshi yake nchini Mali. Gazeti hilo linaarifu kwamba Ufaransa imeviteremsha virafu karibu 40 katika nchi jirani ya Ivory Coast kwa ajili ya harakati za kupambana na waasi nchini Mali.
Rais Hollande amethibitisha mapema wiki hii kuwa Ufaransa kwa jumla itawapeleka wanajeshi 2,500 nchini Mali ili kupambana na waasi.
Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" pia limeripoti kwamba Rais Hollande anakusudia kulikabidhi, haraka, jukumu la kuiongoza operesheni ya kijeshi nchini Mali kwa jeshi la pamoja la nchi za Afrika magharibi lililoidhishiwa na Umoja wa Mataifa.
Gazeti la "Süddeutsche Zeitung" pia limeandika juu ya mgogoro wa Mali kwa kutilia maanani kwamba majeshi ya nchi jirani yatajiunga na majeshi ya Ufaransa katika kupambana na waasi nchini Mali.
Gazeti la "Stuttgarter "pia limeuzingatia mgogoro wa Mali lakini kwa kuiangalia dhima ya Ujerumani.Gazeti hilo linaeleza katika maoni yake kwa nini Ujerumani inajiweka nyuma nyuma kuhusu mgogoro wa Mali.
Gazeti hilo linaeleza kwamba mnamo mwaka huu ambapo uchaguzi mkuu utafanyika nchini Ujerumani, Kansela Angela Merkel hapendelei kujiingiza katika matukio ya nchi za nje yanayoweza kumharibia katika uchaguzi.Msimamo huo unamweka Kansela Merkel katika hali ya mkingamano.
Merkel aliahidi kuwa Ujerumani itasimama pamoja na Ufaransa nchini Mali lakini kileambacho Ujerumani imekifanya hadi sasa ni kutoa ndege mbili tu za kusafirishia mizigo.
Gazeti la"Berliner Zeitung" limechapisha makala kuhusu jinsi makampuni makubwa yanavyonufaika kutokana njaa za watu. Katika makala hiyo gazeti la "Berliner Zeitung" linasema mashirika ya misaada yanayalaumu makampuni makubwa ya kimataifa kwa kudhibiti viwango vya uzalishaji wa chakula katika nchi zinazoendelea. Gazeti hilo linaeleza kwamba Kampuni ya Nestle imefikia mkataba na wakulima wadogo wadogo barani Afrika wa kuiwezesha kampuni hiyo kuyanunua mazao ya wakulima hao moja kwa moja kwa ajili ya kutengenezea maziwa.
Kampuni ya" Coca-Cola" inauza kinywaji kilichorutubishwa na madini ya kalisi yaani calcium, na kampuni ya Unilever inauza biskuti za muhogo zenye kiwango cha juu cha madini ya chuma. Gazeti la "Berliner Zeitung" linasema makampuni makubwa ya chakula na kilimo yanazidi kujiingiza katika dhima ya kupambana na utapiamlo duniani.Lakini gazeti la "Beriner Zeitung" limearifu kwamba makampuni hayo yanalaumiwa na mashirika ya misaada, kama vile la Ujerumani, "Misereor".
Gazeti la"Berliner Zeitung"limelikariri shirika hilo na lingine la kutetea ulinzi wa mazingira.Mkuu wa Shirika hilo Jürgen Maier amekaririwa na gazeti la"Berliner Zeitung"akisema "inachohitajika katika nchi zinazoendelea ni kuweka vitega uchumi sahihi."
Kashfa ya barabara
Gazeti la"Berliner Zeitung" wiki hii pia limechapisha ripoti juu ya kashfa inayohusu ujenzi wa barabara katika nchi kadhaa za Afrika kwa fedha zinazotolewa na Umoja wa Ulaya.Gazeti hilo linasema kwamba baadhi ya barabara zinadumu kwa muda wa miaka minne tu,baada ya kujengwa.Berliner Zeitung linaeleza katika taarifa yake kwamba kati ya mwaka wa 1995 na 2011,Umoja wa Ulaya umetoa kiasi cha Euro bilioni 7.kwa nchi za Afrika,za kusini mwa jangwa la Sahara,kwa ajili ya miradi ya ujenzi wa barabara. Lakini malori makubwa yanaziharibu barabara hizo.
Pamoja na hayo serikali za nchi za Afrika zinatumia fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa barabara mpya ambazo hazidumu kwa muda mrefu - baadhi kwa muda wa miaka minne tu.
Mwandishi:Mtullya Abdu./Deutsche Zeitungen.
Mhariri: Josephat Charo