1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Abdu Said Mtullya9 Novemba 2012

Wiki hii magazeti ya Ujerumani yameandika juu ya kijiji cha Kogelo kwa bibi yake Obama.Magazeti hayo yameripoti kwamba kijiji hicho kilikuwa macho usiku wote ili kuufuatilia uchaguzi wa nchini Marekani.

https://p.dw.com/p/16gKi
Wanakijiji wa Kogelo,Kenya wakifurahi juu ya ushindi wa Rais Obama
Wanakijiji wa Kogelo ,Kenya wakifurahi juu ya ushindi wa Rais ObamaPicha: dapd

Magazeti ya Ujerumani pia yameandika juu ya Fauzia Yusuf Haji Adana, mwanamke wa kwanza kuchaguliwa kuwa waziri wa mambo ya nje wa Somalia. Na gazeti la " die tageszeitung" linatupia macho mgogoro uliotokea kwenye mpaka baina ya Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo na Rwanda.

Gazeti la "Der Tagesspiegel"lilifuatilia jinsi watu wa kijiji hicho walivyokesha ili kujua yaliyokuwa yanajiri katika uchaguzi wa rais nchini Marekani. Gazeti hilo limeandika kuwa Bibi yake Obama katika kijiji cha Kogelo alisherehekea kuchaguliwa tena kwa mjuu wake, Barack nchini Marekani. Takriban nusu ya wanakajiji hawakulala usiku wa kuamkia jumatano ili kuufuatilia uchaguzi wa rais nchini Marekani.Bibi wa kambo wa Obama, Sarah alizungukwa na majirani akiwa anaangalia televisheni.

Gazeti la "Der Tagespiegel" limekariri taarifa ya gazeti la Kenya ,Daily Nation likiripoti kuwa Bibi,Sarah alikuwa na uhakika juu ya ushindi wa mjukuu wake Obama. Gazeti la "Der Tagesspiegel" pia limeripoti kwamba karibu na kijiji cha Kogelo walizaliwa mapacha katika siku ya uchaguzi. Mzazi wao Millicent Owuor amewapa mapacha wake majina ya Barack Obama na Mitt Romney.Kijiji cha Kogelo kilichopo ,magharibi mwa Kenya ndipo alipozaliwa baba yake Obama.

Gazeti la "die tageszeitung limechapisha wasifu wa mwanamke wa kwanza kuteuliwa kuwa Waziri wa mambo ya nje wa Somalia,Fauzia Yusuf Haji Adan. Katika medani ya kimataifa mama huyo analiandika jina lake kwa kutumia tahijia tofauti na zile anazotumia nchini Somalia. Lakini gazeti la "die tageszeitung" linasema hayo siyo muhimu.Jambo la kutilia maanani ni kwamba kuanzia sasa jumuiya ya kimataifa itapaswa kulizoea jina la Fauzia Yusuf Haji Adan.Gazeti la "die tageszeitung" linatilia maanani katika makala yake kwamba, mwanamke hajawahi kuiongoza wizara ya mambo ya nje nchini Somalia. Gazeti hilo pia limetilia maanani kwamba mama huyo pia atakuwa makamu wa Waziri Mkuu katika baraza la mawaziri la Somalia. Fauzia Yusuf aliishi katika hifadhi ya kisiasa nchini Uingereza kuanzia mwaka wa 1995 ambako alianzisha kikundi cha wakimbizi cha kujisaidia wenyewe. Lakini gazeti la "die tageszeitung linasema ,mara kwa mara mwanasiasa huyo alikuwa anarejea nyumbani.

Gazeti la "die tageszeitung wiki hii pia limechapisha habari juu ya mzozo uliotokea kwenye mpaka baina ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na Rwanda. Gazeti hilo linaarifu kwamba mzozo uliotokea kwenye mpaka baina ya Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo umechochea zaidi mvutano uliopo baina ya nchi mbili hizo.

Gazeti hilo limearifu katika makala yake kwamba askari mmoja wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo aliuliwa na wanajeshi wa Rwanda wiki iliyopita. Gazeti la "die tageszeitung" limemnukuu msemaji wa jeshi la Rwanda Joseph Nzabamwita akisema kwamba askari wawili wa jeshi la Kongo walivuka mpaka na kuingia Rwanda kufanya ujasusi. Baada ya kuarifiwa na wanakijiji, askari wa Rwanda walipelekwa katika sehemu husika ,ambapo palitokea mapambano.

Lakini gazeti la die tageszeitung limemkariri mkuu wa polisi wa mpakani katika Kivu ya Kaskazini akikanusha kauli ya msemaji wa jeshi la Rwanda. Msemaji huyo, Ethienne Kasala ameliambia gazeti la "die tageszeitung" kwamba askari wa Kongo waliondoka kwenye kituo chao ili kuenda kununua maziwa katika eneo la mpakani, kwa sababu wanafanya hivyo wakati wote. Na msemaji wa jeshi la Kongo katika Kivu ya kaskazini,Olivier Hamuli ameliambia gazeti la "die tageszeitung " kwamba askari wao aliuliwa ndani ya mpaka wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo .

Mwandishi:Mtullya abdu.Deutsche Zeitungen:

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman