1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Abdu Said Mtullya14 Septemba 2012

Magazeti ya Ujerumani juu ya Rais mpya wa Somalia, mgogoro wa migodi Afrika Kusini na kesi ya mauaji inayomkabili raia wa Nigeria nchini Ukraine.

https://p.dw.com/p/169L9
Rais mpya wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud
Rais mpya wa Somalia - Hassan Sheikh MohamudPicha: picture-alliance/dpa

Gazeti la "Süddeutsche" liemandika juu ya Rais mpya wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud kwa kusema "Wasomali wamesherehekea kwa kufyatua risasi hewani kuchaguliwa Rais wao mpya, Hassan Sheikh Mohamud. Gazeti la "Süddeutsche" linatilia maanani katika makala yake kwamba ushindi wa Sheikh Mohamud katika uchaguzi wa Rais uliwashangaza watu, kwani yeye siye alietarajiwa kushinda." Hassan Sheikh Mohamud alishinda katika duru ya pili ya uchaguzi kwa kura 190 na kumwacha nyuma kabisa aliekuwa Rais wa kipindi cha mpito, Sharif Sheikh Ahmed, alieambulia kura 79. Gazeti la "Suddeutsche" linasema Rais mpya wa Somalia Sheikh Mohamud ni ishara ya zama mpya nchini Somalia.

Gazeti hilo linaeleza kuwa Rais huyo mpya ndiye mtu ambae wasomali wanamhitaji sana kwani mpaka sasa jina lake halijaingia doa la madai ya rushwa, na wala hahusiani na wababe wa kivita. Hata hivyo Hassan Sheikh Mohamuda hakuwa an mwanzo mzuri kwani gazeti la "Berliner Zeitung" limeandika taarifa juu ya jaribio la kumuua Rais huyo.

Gazeti hilo limearifu: "Siku moja tu baada ya kuanza kazi Rais Hassan Sheikh Mohamud aliponea chupu chupu baada ya jaribio la kumuua lililofanywa na wapiganaji wa al - Shabaabu kushindikana. Washambuliaji wa kujitoa mhanga zaidi ya watatu walijaribu kujipenyeza katika hoteli ya al-Jazeerah iliyopo karibu na uwanja wa ndege ambako Rais huyo anakaa. Taarira ya "Berliner Zeitung" inaeleza kuwa mshambuliaji mmoja alijirupua wakati Rais mpya wa Somalia alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari pamoja na Waziri wa mambo ya nje wa Kenya, Sam Ongeri. Wote wawili walinusurika. Gazeti la "Berliner Zeitung" limekariri habari zinazosema kuwa wapiganaji wa al-shabaab wamedai kuhusika na shambulio hilo.

Gazeti la "Financial Times Deutschland" pia limeandika juu ya Rais mpya wa Somalia kwa kumwita Rais huyo kuwa Obama wa Somalia. Gazeti hilo limemnukuu mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, Augustine Mahiga, akisema: Rais mpya anawakailisha kipindi cha mabadaliko- na hakuna mwengine kama yeye. Kuchaguliwa kwake kutaanzisha enzi mpya"

Harakati za wafanyakazi wa migodi nchi Afrika Kusini zinaendelea na hakuna matumaini ya kupatikana suluhisho hivi karibuni. Hizo ni habari zilizoandikwa na gazeti la "Frankfurter Allgemeine" Gazeti hilo linaarifu:
"Harakati za wafanyakazi wa migodi nchini Afrika kusini zinaenea nchini kote. Wafanyakazi hao wanadai nyongeza za mishahara. Mazungumzo baina ya wawakilishi wa wafanyakazi na wamiliki wa migodi hayajaleta matunda. La kutilia maanani ni kwamba pana mvutano baina ya vyama vya wafanyakazi."

Gazeti la "Süddeutsche" wiki hii limeripoti juu ya kesi ya mauaji inayomkabili raia mmoja wa Nigeria nchini Ukraine. Gazeti hilo linatupasha: kwamba mwanafunzi kutoka Nigeria, Olaolu Sunkanmi, ametiwa ndani tokea nusu mwaka akikabiliwa na mashtaka ya kuua bila ya kudhamiria. Mwendesha mashtaka wa serikali anadai kuwa mwanafunzi huyo aliwashambulia vijana wa Ukraine kwa kutumia chupa iliyovunjika. Gazeti la Süddeutsche "limewakariri wanaharakati wa mashirika ya haki za binadamu wakisema kwamba hakuna mshtaki alieumizwa kiasi cha kuhatarisha maisha yake. Gazeti la "Suddeutsche" limewanukuu watetezi wa haki za binadamu wakisema kuwa kesi hiyo ni bandia na inaonyesha maonevu yaliopo katika mfumo wa sheria nchini Ukraine. Wanaharakati wanaotetea haki za binadamu wamesema kuwa kesi inayomkabili kijana huyo kutoka Nigeria imepangwa ili kuwanufaisha vijana wa Ukraine wanaodai kuwa walishambuliwa na Mwafrika huyo.

Gazeti la "Südeutsche" linasema katika taarifa yake kwamba kijana mmoja miongoni mwa wanaodai kushambuliwa na Mnageria huyo anadai fidia ya Euro 10,000.

Mwandishi:Mtullya abdu:Deutsche Zeitungen/

Mhariri: Miraji Othman