Afrika Katika Magazeti ya Ujerumani
31 Agosti 2012.
Gazeti la "die tageszeitung" linazungumzia hatua muhimu sana iliyopigwa na watu wa Somalia mnamo wiki hii. Gazeti hilo limeandika katika makala yake, kwamaba wabunge wa Somalia wamemchagua Spika wao, Bwana Mohammed Osman Jawari aliekuwa waziri hapo awali.
Kuchaguliwa kwa Spika huyo wa Bunge ni hatua ya kwanza ya kuelekea katika kuunda serikali itakayofanya kazi nchini Somalia. Tokea mwaka wa 1991 nchi hiyo haijawa na serikali yoyote .Ni vita tu vya wenyewe kwa wenyewe tokea wakati huo. Gazeti la "die tageszeitung" linatilia maanani kwamba kuchaguliwa kwa Spika wa Bunge nchini Somalia maana yake ni kwamba sasa tarehe ya uchaguzi wa Rais itapangwa.
Gazeti la "die tageszeitung" pia limeandika juu ya matukio ya mjini Mombasa nchini Kenya. Chini ya kichwa cha habari "Waislamu wa Mombasa wamekasirishwa sana baada ya kuuawa kwa kiongozi wa kidini-Sheikh Aboud Rogo.", gazeti hilo limearifu kuwa kifo cha Sheikh aliekuwa na itikadi kali na aliekuwa anatuhumiwa kuwa gaidi, kimesababisha ghasia kubwa katika mji wa Mombasa. Linasema na hadi kufikia jumatano iliyopita watu watano walikuwa wamekufa kutokana na ghasia hizo. Maalfu ya wafuasi wa Sheikh Aboud Rogo waliandamana barabarani na wengine waliyashambulia makanisa.
Gazeti la "die tageszeitung" limemkariri Waziri Mkuu wa Kenya Raila Odinga akisema kwamba Sheikh Aboud Rogo aliuliwa na maadui wa Kenya,wanaolenga shabaha ya kuwagombanisha Wakristo na Waislamu wa nchi hiyo.
Gazeti la "die tageszeitung" linakumbusha katika makala yake kwamba Sheikh Aboud Rogo siyo mtu wa kwanza kuuawa nchini Kenya ,aliekuwa anatuhumiwa kuwa gaidi. Gazeti hilo linasema mnamo mwezi wa Aprili, mtuhumiwa mwengine wa ugaidi ,Samir Hashim Khan aliuawa.
Sheikh Aboud Rogo aliuawa alasiri ya jumatatu iliyopita ndani ya gari alipokuwa njiani kuelekea hospitali yeye pamoja na familia yake.Gazeti la "die tageszeitung" limeripoti kwamba watu wake wanatuhumu kwamba waliomuua walikuwa mawakala wa serikali.
Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" wiki hii limeandika juu ya umuhimu wa pampu katika kukidhi mahitaji ya maji kwa wakulima. Gazeti hilo linaarifu kattika makala yake kuwa mamilioni ya wakulima wanayamwagilia mashamba yoa kwa kutumia ndoo au madebe, lakini gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linasema uchunguzi umeonyesha kuwa kwa ,kutumia vifaa vya kisasa wakulima wataweza kuongeza mavuno yao. Gazeti hilo limeripoti juu ya uchunguzi uliofanywa na shirika la mradi wa maji-"Water Solutions Project." Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" limeinukuu ripoti ya uchunguzi huo ikisema: kuwa maji ni haba katika sehemu nyingi duniani.Na hata pale ambako yanapatikana, wakulima wadogo wadogo hawana uwezekano wa kuyatumia katika kiwango cha kuwaletea faida. Kutokana na hali hiyo, maisha ya mamiioni barani Afrika yanazidi kuwa mabaya, hali ambayo inaweza kuepukwa.
Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linasema baada ya uchunguzi uliochukua muda wa miaka minne,wataalamu walioshiriki katika uchunguzi huo wametoa mwito wa kuwasaidia wakulima katika njia za kuyatumia maji kwa ufanisi , kwa mfano kwa kutumia pampu zinazoendeshwa na mashine ili kusukuma maji wakati wa kuyamwagilia mashamba. Katika mwito wao wataalamu wamesema matumizi ya pampu yanaweza kuongeza mavuno kwa asilimia hadi 300. Katika taarifa yake gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linasema ikiwa maji yatapatikana kwa uhakika kwenye mashamba ya wakulima wadogo wadogo katika nchi za Afrika kusini ya jangwa la Sahara, watu Milioni 369 watanufaika na kiasi cha dola Bilioni 20 kitaingizwa kila mwaka.
Mwandishi:Mtullya abdu/Deutsche Zeitungen/
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman