1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Abdu Said Mtullya22 Julai 2012

Magazeti ya Ujerumani karibu yote yameandika kwa mapana na marefu juu ya kuchaguliwa Nkosazana Dlamini-Zuma kuwa Rais mpya wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika

https://p.dw.com/p/15cto
Rais mpya wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika
Rais mpya wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika,Nkosazana Dlamini-ZumaPicha: Reuters

Magazeti ya Ujerumani pia yameandika juu ya mgogoro wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, na juu ya madai yaliyotolewa dhidi ya Rais wa Somalia Ahmed Sharif kwamba anasharikiana na wahalifu.

Juu ya Rais mpya wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika gazeti la "Die Welt linasema katika makala yake kwamba mwanamke anataka kulisogeza bara la Afrika mbele. Mwanamke huyo ni Nkosazana Dlamini- Zuma aliechaguliwa kuwa Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Afrika.

Gazeti la "Die Welt"limeeleza zaidi juu ya mwanasiasa huyo."Kwa mara ya kwanza katika historia yake, Umoja wa Afrika unaongozwa na mwanamke , Nkosazana Dlamini - Zuma aliekuwa waziri wa mambo ya ndani wa Afrika Kusini. Gazeti "Die Welt" linasema kuchaguliwa mwanamke huyo kuuongoza Umoja wa Afrika ni hatua iliyovunja mwiko. Siyo tu kwa sababu mwanamke amechaguliwa, bali kwa sababu anatoka katika nchi inayozingatiwa kuwa taifa kubwa- Afrika Kusini. Kwa mujibu wa sheria ya pembeni, ambayo haijaandikwa popote, wadhifa huo haupaswi kushikwa na mtu anaetoka katika nchi zinazozingatiwa kuwa kubwa, kama vile Afrika Kusini na Nigeria."

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" pia limeandika juu ya Dlamini - Zuma, na linasema Rais mpya wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika ni mwanasiasa maarufu sana barani Afrika, lakini katika upande mwingine anayo tabia ya kutoa macho ya ukali. Anatafautiana na Rais wa hapo awali-Jean Ping kutoka Gabon."

Dlamini- Zuma anataka kuona matokeo ya juhudi wakati Jean Ping aliendekeza sana itifaki. Hata hivyo, gazeti la "Die Welt" linakumbusha kwamba mwanasiasa huyo atakabiliwa na changamoto kadhaa katika wadhifa wake. Moja wapo ni mgogoro wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Na gazeti la "die Tageszeitung" linauzungumzia mgogoro huo kwa kusema: inapasa kukizingatia kiini cha mgogoro. Huo ni ujumbe kwa serikali za nchi zlizoamua kupeleka majeshi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi Kongo ili kupambana na makundi ya waasi."

Katika makala yake gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linauzungumzia mkutano wa kilele wa viongozi wa nchi za Umoja wa Afrika. Lakini gazeti hilo linautilia maanani mkutano wa marais wa Sudan na Sudan ya Kusini.

Gazeti hilo linasema kwa mara ya kwanza baada ya zaidi ya nusu mwaka, Marais Omar al -Bashir wa Sudan na Salva Kiir wa Sudan ya Kusini walikutana mjini Addis Ababa pembeni ya kikao cha viongozi wa Umoja wa Afrika. Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" limeikariri taarifa ya mjumbe mmoja wa Sudan ya Kusini akisema kuwa mazungumzo hayo yalifanyika katika mazingira ya kirafiki.

Lakini mazingira siyo ya kirafiki nyumbani kwa Omar al -Bashiri. Gazeti la "Die Zeit" linayasema hayo katika makala yake. Linaeleza kuwa mamlaka ya Rais Omar al-Bashir yanaanza kuyumba kutokana na hali mbaya ya kiuchumi. Gazeti la "Die Zeit" linaeleza sababu ya kuyumba kwa mamlaka ya rais huyo. Sudan itakuwa na pengo kubwa katika bajeti yake mnamo mwaka huu, kufikia kiasi cha dola bilioni 2.5

Sababu ya pengo hilo ni kwamba asilimia 80 ya bajeti inatengwa kwa ajili ya matumizi ya kijeshi na kwa ajili ya idara ya usalama. Serikali imelazimika kubana matumizi, hali inayosababisha maandamano ya mara kwa mara

Gazeti la "die tageszeitung" limechapisha madai kwamba Rais Sheikh Sharif Ahmed wa Somalia anashirikiana na wahalifu. Madai hayo ni juu ya hati ya kusafiria iliyotolewa kwa ajili ya kiongozi wa maharamia Mohammed Abdi Hassan Afweyne. Kiongozi huyo wa maharamia alipewa pasi hiyo ya kibalozi kwa idhini ya Rais Sharif Ahmed ili kumwezesha kuitembelea familia yake nchini Malaysia.

Gazeti la "die tageszeitung limearifu katika makala yake kwamba Mohammed Afweyne alitoa hati nchini Malaysia iliyosema kuwa alikuwa kazini kupambana na uharamia. Hati hiyo ilitoka ofisi ya Rais.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen/

Mhariri: Miraji Othman