Afrika katika magazeti ya Ujerumani
29 Mei 2012Tuanzie lakini Somalia ambako gazeti la mjini Berlin,Die Tageszeitung linazungumzia juu ya vitisho vilivyotolewa na maharamia wa kisomali dhidi ya wanamaji wa kikosi cha Atalanta cha Umoja wa Ulaya baada ya helikopta za kikosi hicho kuhujumu kwa mara ya kwanza vituo vya maharamia hao ndani nchini Somalia.Die Tageszeitung limemnukuu mkuu wa maharamia Abdi Yare akiliambia shirika la habari la Ufaransa-AFP,"watajibisha vikali" pindi wanajeshi wa Atalanta wataendelea kuhujumu maeneo ya mwambao. Gazeti la die Tageszeitung limemnukuu pia mkuu wa maharamia Bile Hussein akilalamika na kusema vikosi vya Atalanta vimezivunja mashua zao tisaa.
Nalo gazeti la Die Zeit limezungumzia jinsi polisi ya Kenya inavyomsaka raia mmoja wa kijerumani aliyesilimu.Anatuhumiwa kuhusika na visa vya ugaidi.Familia yake nchini Ujerumani imeingiwa na hamu kupita kiasi kuhusiana na madai hayo."Andy uko wapi?" Ndio kichwa cha maneno cha ripoti ya Die Zeit.Andy ni jina la mkato la Andreas Ahmed M. mwenye umri wa miaka 40.Anatuhumiwa na polisi ya Kenya kushiriki katika shambulio la Nairobi April 29 iliyopita ambapo watu wawili waliuwawa.Anatuhumiwa pia kuwa mfuasi wa kundi la wanamgambo wa kiislam wa Somalia, Al Shabab wanaoshirikiana na Al Qaida.Picha yake imesambazwa katika mtandao wa Internet.Gazeti la Die Zeit linazungumzia jinsi Familia ya Andreas Ahmed M walivyoingiwa na majonzi na simanzi tangu walipoyasikia madai hayo.Die Zeit linasema hali kama hiyo inazikumba familia kadhaa ambazo watoto wao baada ya kusilimu,wamekuwa wakiondoka nyumbani bila ya kuaga na kuhamia mahala kusikojulikana ambako mara nyengine wanajiunga pengine na makundi ya wanamgambo,makundi ya kigaidi na kadhalika.
Gazeti la Die Tageszeitung linazungumzia kuhusu ripoti ya Shirika la haki za binaadam Human Rights Watch kuhusu visa vya kikatili wanavyofanyiwa wahamiaji wa jamahuri ya kidemokrasi ya Kongo wanaoshikiliwa katika vituo vya Angola kwa lengo la kuwarejesha nyumbani.Katika jela zilizojazana watu nchini Angola,wakinamama na wasichana kila siku wananajisiwa,wanateswa na kupigwa.Wanavumulia vituko hivyo vya kinyama vinavyofanywa na polisi na wanajeshi wa Angola kwasababu ya woga wa kufa na njaa au kuuliwa.Die Tageszeitung linazungumzia mwito uliotolewa na shirika hilo la haki za binaadam-Human Rights Watch kutaka wahalifu wafikishwe mahakamani.Ripoti ya Human Rights Watch imewanukuu wahanga wa kambi hiyo ya Condueji huko Dundo wakisema wanajeshi walikuwa wakija kwa makundi makundi,watu watatu au hata wanne-na kuwanajisi .Watoto wamekuwa wakishuhudia madhila hayo na kila wakati wakihanikiza kwa vilio.Serikali ya Angola daima imekuwa ikikanusha ripoti za kunajisiwa wakinamama na wasichana katika vituo hivyo.Rais Edouardo Dos Santos amewahi kuahidi sheria za kimataifa zitaheshimiwa katika utaratibu wa kuwarejesha makwao wahamiaji-hali lakini ni nyengine kabisa linamaliza kuandika gazeti la Die Tageszeitung.
Na hatimae lilikuwa gazeti la Frankfurter Allgemeine Zeitung lililozungumzia kuhusu vurugu zilizotokea katika kasri la rais nchini Mali ambapo rais wa mpito Dioncounda Traore alipigwa mpaka kuzimia na watu walioivamia ofisi yake.Kuna wanaoamini mashambulio hayo yamefanywa na wafuasi wa utawala wa kijeshi ambao hawajafurahishwa na makubaliano yaliyofikiwa pamoja na jumuia ya ushriikiano ya Afrika Magharibi ECOWAS ya kuwataka wanajeshi warejee kambini na spika wa bunge Dioncounda Traore aendelee na kipindi cha mpito hadi uchaguzi utakapoitishwa.Tangu makubaliano hayo yalipofikiwa watawala wa kijeshi wanaoongozwa na kepteni Sanogo wamekuwa wakitoa masharti mepya na matumaini ya kupatiwa ufumbuzi wa amani mzozo wa Mali yanazidi kufifia, linamaliza kuandika gazeti la Frankfurter Allgemeine.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Pressedatenbank
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman