Afrika kama mbia wa kiuchumi
18 Mei 2012Wajasirimali wa Ujerumani wanaopendelea kushirikiana na Afrika wameungana katika chama cha uhusiano baina ya Ujerumani na Afrika. Idadi ya wanachama wa chama hicho inazidi kuongezeka, na sasa imefikia mia saba. Miongoni mwa wanachama hao ni kampuni kubwa za kimataifa, kama Siemens na ThyssenKrupp. Mwenyekiti wa chama cha uhusiano baina ya Afrika na Ujerumani, Stefan Liebig, amelalamika kwamba kampuni zisizokuwa na habari za kutosha juu ya Afrika zinaliepuka bara hilo kutokana na kulinasibisha na migogoro. Mbali hilo, ushindani sasa umekuwa mkali zaidi kuliko ilivyokuwa hapo awali kutokana na shuhguli za China, Brazil na India barani Afrika. Kutokana na ushindani huo wajasirimali wa Ujerumani wanahitaji mikakati mipya. Hayo ameshauri mwenyekiti huyo Liebig. „Anachokisikia mtu barani Afrika kote ni kwamba teknolojia na bidhaa za Ujerumani zinathaminiwa sana. Lakini pia inapasa kusema kwamba bidhaa za Ujerumani aghalabu ni ghali."
Kinachotakiwa: Bidhaa za bei nafuu
Sambamba na bidhaa mahsusi kwa mahitaji ya nchi za Afrika, nchi hizo pia zinapendelea miradi ya kubalidishana taaluma. Anaepeleka teknolojia barani Afrika pia atapaswa kutoa mafunzo kwa waafrika. Mfano ni katika sekta ya nishati endelevu. Nchini Nigeria miradi hiyo inajenga msingi wa ugavi imara wa nishati, kama anavyosisitiza Waziri wa sayansi na utafiti wa Nigeria, Ita Okon Bassey, ambae hivi karibuni alifanya ziara nchini Ujerumani: „Ama kwa hakika tunajaribu kuanzisha ushirikiano nchini Ujerumani na mashirika ambayo hasa ya uhusiano na chuo kikuu cha Stuttgart na vyuo vingine vya Ujerumani. Nafikiri hayo yanajenga mazingira yanaowawezesha washirika wa Nigeria kuja Ujerumani na kujifunza tekinolojia."
Kinachodhamiriwa: Uzalishaji ndani ya nchi yenyewe
Nchi za Afrika hasa zinasisitiza juu ya kushughulikia ndani ya bara hilo, sehemu kubwa ya sekta ya kuongeza thamani ya bidhaa. Hayo yana maana kuwa kazi zitafanywa na waafrika wenyewe, katika sekta ya zana ufundi na kushuhgulikia mali ghafi. Kampuni ya Ujerumani, Siemens, imejipanga kuona utaratibu huo ukiongezeka kati ya asilimia 80 na 90 nchini Ghana, Nigeria na Angola.
Sambamba na nishati endelevu nchi za Afrika pia zinakodolea macho ufundi ambao hata nchini Ujerumani hakuna anaeutaka tena. Katika ziara yake ya hivi karibuni nchini Ujerumani, waziri wa nishati wa Nigeria aliifafanua mipango ya nchi yake ya nishati ya nyuklia. Pia katika sekta hiyo Ujerumani ni mshirika anaethaminiwa, amesema waziri huyo.
Mwandishi: Mösch, Thomas.
Tafsiri: Mtullya, Abdu
Mhariri: Othman, Miraji