1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afisa mkuu wa jeshi auawa nchini Lebanon

12 Desemba 2007
https://p.dw.com/p/Cab2
Rais wa zamani wa Lebanon Emile Lahoud,(kulia) pamoja na Jemadari Michel Sleiman.Picha: AP

Mripuko mkubwa wa bomu uliotokea asubuhi ya leo katika mji mkuu wa Lebanon,Beirut umeua si chini ya watu 5 na kujeruhi 10 wengine.Miongoni mwa waliouawa ni Jemadari Francois El Hajj.

Yadhihirika kuwa mripuko huo wa bomu uliotikisa kitongoji cha Baabda,kusini-mashariki ya mji mkuu Beirut,ulilenga kumuuwa Jemadari Francois El Hajj aliekuwa njiani kwenda kazini katika wizara ya ulinzi.Jemadari huyo alipata umaarufu wake wakati wa vita vya majira ya joto kati ya vikosi vya serikali na kundi linalounga mkono Al-Qaeda. Mapigano hayo katika kambi ya wakimbizi ya Wapalestina ya Nahr el-Bared,kaskazini mwa Lebanon yalidumu majuma 15.

Jemadari El Hajj alitazamiwa kuchukuwa nafasi ya kamanda mkuu wa majeshi,Jemadari Michel Sleiman anaetumainiwa kuwa rais mpya wa Lebanon. Kuchaguliwa kwa Sleiman kumekwama kwa sababu ya mvutano wa kambi inayoiunga mkono Syria na ile inayoipinga.

Muandishi wa habari aliekuwepo eneo la mripuko alisema,mripuko huo ulitokea nje ya jengo la manispaa ya Baabda na kuharibu vibaya jengo hilo. Hata magari mengi yaliyoegezwa karibu na eneo la mripuko yamteketezwa.Maafisa wengi wanaamini kuwa mauaji ya Jemadari El Hajj yanahusika na vita vya kambi ya Nahr al-Bared.

Hivi sasa Lebanon inajikuta katika hali ya mvutano mkubwa.Siku ya Jumanne bunge kwa mara ya nane,liliahirisha kikao chake kumchagua mkuu wa majeshi Sleiman kama rais mpya wa Lebanon,wakati upande unaounga mkono na ule unaoipinga Syria ukisababisha mzozo mbaya kabisa tangu kumalizika vita vya wenyewe kwa wenyewe vya mwaka 1975 hadi 1990.Inahofiwa kuwa mgogoro wa hivi sasa huenda ukasababisha machafuko katika nchi iliyokumbwa na mauaji kadhaa ya kisiasa tangu miaka miwili iliyopita.Katika kipindi hicho,waliuawa wabunge na wanasiasa kadhaa wanaoipinga Syria.

Lebanon haina rais tangu Emile Lahoud kumaliza muhula wake tarehe 23 Novemba.Serikali ya mseto na upande wa upinzani zimekubaliana kumpa Jemadari Sleiman wadhifa wa urais,lakini wanashindwa kuafikiana njia ya kubadilisha katiba ili kuweza kumchagua jemadari huyo.Tatizo jingine ni muundo wa baraza jipya la mawaziri.Nchi za Kiarabu na Ulaya zina wasiwasi kuwa mzozo wa hivi sasa nchini Lebanon,huenda ukahatarisha zaidi hali utulivu nchini humo.