Afghanistan yatia saini mkataba na Marekani
30 Septemba 2014makubaliano hayo yanamaliza mwaka mmoja wa hali ya sintofahamu juu ya hali ya baadaye ya majeshi ya kigeni yanayosaidia Waafghanistani wakati wakichukua jukumu la usalama katika nchi yao.
Viongozi wa Afghanistan, Marekani na wa NATO wameyakaribisha makubaliano hayo , ambayo yataruhusu kiasi ya wanajeshi 10,000 wa marekani kubakia nchini humo baada ya ujumbe wa mapambano wa majeshi ya kimataifa kumalizika tarehe 31 Desemba.
Rais wa zamani wa Afghanistan Hamid Karzai alikataa kutia saini licha ya vitisho vya Marekani vya kuondoa kabisa majeshi yake iwapo hakutakuwa na chombo cha kisheria kitakachowalinda wanajeshi wa Marekani.
Maafisa wa Marekani wamesema kuwa uchelewesho huo katika kutiwa saini kwa makubaliano hayo hakutaathiri mipango ya mwaka ujao.
Rais Ashraf ghani Ahmadzai , ambaye aliapishwa kushika madaraka hayo siku moja kabla, ameuambia mkusanyiko huo kuwa makubaliano yaliyotiwa saini yanaashiria hatua muhimu ya mabadiliko kuelekea katika hali bora katika uhusiano wa nchi hiyo na dunia.
"Makubaliano haya ni kwa ajili tu ya usalama na uthabiti wa Afghanistan," amesema.
"Makubaliano haya ni kwa maslahi ya taifa letu. Makubaliano ya pande mbili ya usalama yatasafisha njia kwa ajili ya Afghanistan kuchukua udhibiti," ameongeza.
Mshauri mpya aliyeteuliwa wa masuala ya usalama nchini Afghanistan , Mohammad Hanif Atmar na balozi wa Marekani James Cunningham walitia saini makubaliano hayo katika ikulu ya rais katika mji mkuu Kabul.
Makubaliano ya pili yanayoruhusu majeshi ya NATO kubakia nchini humo pia yalitiwa saini pia wakati wa sherehe hizo.
Mtendaji mkuu wa serikali Abdullah Abdullah , ambaye amepewa wadhifa ambao ni sawa na waziri mkuu baada ya kutia saini makubaliano ya kugawana madaraka na Ghani Ahmadzai , pia ameukaribisha mkataba huo wa usalama.
"Umetiwa saini baada ya tafakari ya kina," amesema na kuongeza kuwa " mkataba huo unaojulikana kama BSA si kitisho kwa majirani zetu. Utasaidia kuimarisha amani na uthabiti katika kanda hiyo."
Katibu mkuu wa NATO Anders Fogh rasmussen ameukaribisha mkataba huo , akisema unaainisha ujumbe mpya wa kundi hilo la mataifa kutoa mafunzo, ushauri na kusaidia majeshi ya Afghanistan.
"Tutaendelea kusaidia kutoa fedha kwa majeshi ya usalama ya afghanistan, taasisi zake, na kuendeleza zaidi ushirikiano wetu wa kisiasa na kiutendaji na Afghanistan kupitia ushirikiano wetu wa siku zote," amesema katika taarifa.
Wakati huo huo Waafghanistan katika jimbo muhimu kimkakati upande wa kaskazini wa mji mkuu wametishia kufanya uasi iwapo rais mpya nchini humo hataheshimu makubaliano ya kugawana madaraka na kiongozi waliyemchagua , Abdullah Abdullah.
Gavana wa jimbo la Panjshir Abdul rahman Kabiri amesema watu wanawasi wasi kuwa Abdullah anaweza kutupwa nje ya madaraka.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre
Mhariri: Josephat Charo