1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ashraf Ghani kuwaachia huru wafungwa elfu 2 wa Taliban.

25 Mei 2020

Rais wa Afghanistan Ashraf Ghani ameanzisha mchakato wa kuwaachia huru takriban wafungwa elfu 2 wa Taliban kama ''ishara ya nia njema'' kufuatia hatua ya Taliban kutangaza usitishaji wapigano kwa muda wa siku tatu .

https://p.dw.com/p/3cis0
Aschraf Ghani
Picha: Reuters/M. Ismail

Katika ujumbe kupitia ukurasa wa twitter, msemaji wa rais Ghani Sediq Sediqqi alithibitisha hatua hiyo ya rais ya kuwaachia huru wafungwa hao wa Taliban. Ghani pia alisema kuwa serikali yake iko tayari kufanya mazungumzo ya amani na Taliban.Mapema Jumapili, Rais Ghani alisema kuwa ataharakisha hatua ya kuwaachia huru wafungwa hao wa Taliban. Raia wa Afghanistan walikaribisha hatua hiyo ya kusitisha mapigano na kuwasihi Talibani waachane kabisaa na mapigano.

Amir Jan raia wa taifa hilo amesema kuwa alisposikia kuhusu hatua ya kusitisha mapigano, kile alichoweza kusema ni kuwa huu ni wakati wa furaha kwa raia wote katika historia ya Afghanistan baada ya hatua ya mwisho ya kusitisha mapigano mwaka 2018 na kwamba wataliban pia ni raia wa Afghanistan.

Afghanistan Kabul | Taliban werden aus dem Bagram Gefängnis entlassen
Wafungwa wa Taliban walioachiwa huru mwezi Aprili 11, 2020Picha: Reuters/National Security Council of Afg

Mkataba kati ya Marekani na Taliban uliotiwa saini mwezi Februari, uliainisha kuwa serikali ya Afghanistan itawaachia huru wafungwa hadi elfu 5 wa Taliban huku kundi hilo la waasi likiwaachia huru takriban maafisa elfu 1 wa usalama wa Afghanistan. Hatua hiyo ya kubadilishana wafungwa inaonekana kuwa  njia ya kujenga imani kabla ya mazungumzo ya amani yaliosubiriwa kwa muda mrefu kati ya serikali ya Afghanistan na kundi la Taliban.

Kabla ya tangazo hilo la jana, serikali ya Afghanistan tayari ilikuwa imeawaachia huru takriban wafungwa elfu 1 wa Taliban huku waasi hao wakiwaachia huru takriban maafisa 300 wa ulinzi wa Afghanistan. Wakati huo huo,  maafisa wa serikali nchini humo wamesema kuwa watu kumi waliuawa katika tukio la ufyetulianaji risasi kati ya viongozi wawili wa makundi ya wanamgambo waliokuwa wamejihami katika mkoa wa Takhar Kaskazini mwa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa msemaji wa gavana katika mkoa huo Jawad Hijiri, watu watano pia walijeruhiwa wakati wa tukio hilo katika wilaya ya Kalafgan. Hijiri ameongeza kuwa sababu ya tukio hilo bado haijabainishwa lakini akasema kuwa viongozi hao wawili wamekuwa wapinzani wa muda mrefu.

Maafisa hao wa serikali wamesema kuwa baadhi ya viongozi wa makundi ya wanamgambo yanayoendesha shughuli zao nje ya jeshi rasmi la serikali ya Afghanistan wamekuwa chanzo cha ukosefu wa udhibiti na shughuli za uhalifu katika mkoa huo kwa miaka mingi.