Afghanistan baada ya uchaguzi muhimu wa rais
21 Agosti 2009Kiongozi wa kikosi kilichoendesha kampeni ya rais Hamid Karzai katika uchaguzi wa rais nchini Afghanistan amedai leo, kuwa rais huyo ameshinda uchaguzi , na kuongeza kuwa matokeo ya awali yanaonyesha hakutakuwa na haja ya uchaguzi wa duru ya pili. Lakini hata mgombea mwingine wa kiti cha urais Abdullah Abdullah nae amedai kuwa ameshinda uchaguzi huo.
Matokeo ya awali yanaonesha kuwa rais wa sasa Hamid Karzai amepata wingi wa kutosha, Deen Mohammad ameliambia shirika la habari la Reuters, licha ya kusema kuwa ni jukumu la tume ya uchaguzi kutangaza matokeo rasmi ya uchaguzi. Mohammad amesema makadirio ya ushindi huo yako chini ya msingi wa ripoti kutoka kwa karibu wachunguzi 29,000 ambao kikosi cha kampeni ya rais kimewaweka katika vituo vya kupigia kura nchi nzima.
Matokeo rasmi hayatarajiwi karibuni , hadi baada ya wiki mbili, lakini zoezi la kuhesabu kura limeanza mara tu baada ya upigaji kura kumalizika jana.
Vituo 6,200 vya kupigia kura vinatakiwa kutangaza matokeo yake hadharani , baada ya kuhesabu, ili kuepuka udanganyifu.
Msemaji wa mpinzani mkuu wa Karzai, Abdullah Abdullah , amepuuzia madai hayo ya ushindi.
Si kweli, amesema Fazi Sangcharaki, hata sisi tunasema, huenda hatuhitaji uchaguzi wa duru ya pili na Abdullah ameshinda.
Zekria Barakzai , naibu mkuu wa tume huru ya uchaguzi IEC, ametoa wito wa kuwa na subira na uvumilivu.
Maafisa wa Afghanistan pamoja na wale wa Marekani wamejisikia afueni kidogo kutokana na hali ya utulivu katika uchaguzi huo wa rais, ambao wanamgambo wa Taliban wameshindwa kuuvuruga licha ya kutokea mapigano ya hapa na pale nchini humo.
Barakzai amesema kuwa milolongo miwili ya magari ya wafanyakazi wa uchaguzi ikisafirisha maboksi ya kura imeshambuliwa baada ya upigaji kura. Katika tukio moja katika jimbo la Balkh upande wa kaskazini, mfanyakazi wa tume ya uchaguzi aliuwawa na maboksi ya kura ambayo yamekwisha hesabiwa yalichomwa moto. Pia wapiganaji wamewauwa wafanyakazi 11 wa uchaguzi tangu mwanzo wa matayarisho ya uchaguzi hadi jana.
Mjini Washington , rais Barack Obama amesifu uendeshaji wa uchaguzi na kuahidi kuendelea na mkakati wake, ambao unahusisha kupeleka wanajeshi wengine kadha nchini Afghanistan. Inaonekana uchaguzi umefanikiwa nchini Afghanistan , licha ya juhudi za Taliban kuuvuruga, amesema rais Obama. Tunapaswa sasa kuelekeza nguvu zetu katika kumaliza kazi nchini Afghanistan lakini itachukua muda. Uchaguzi huo ni mtihani kwa mkakati mpya wa Obama wenye lengo ya kuwashinda Taliban. Vifo vya wanajeshi wa Marekani vimeongezeka licha ya ongezeko la majeshi hayo na maoni ya wananchi yanaonesha kupungua katika kuunga mkono vita hivyo.
Mwandishi/ Sekione Kitojo/rtre/afp.
Mhariri:Abdul-Rahman