1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afcon: Misri yatinga fainali kwa kuibandua Kameruni

Daniel Gakuba
4 Februari 2022

Misri imefuzu kucheza mechi ya fainali ya Kombe la Afrika la Mataifa, Afcon, baada ya kuwabandua wenyeji Kameruni kwa ushindi wa magoli 3-1 uliopatikana kupitia mikwaju ya penalti.

https://p.dw.com/p/46V0b
Afrika Cup I Ägypten vs Kamerun
Wachezaji wa Kameruni wakifurahia ushindi wao dhidi ya KameruniPicha: Sunday Alamba/AP/picture alliance

Dakika 90 za kawaida na 30 za nyongeza zilimalizika timu zote zikiwa sare tasa, na mlinda mlango wa Misri Mohamed Abou Gabal akawa shujaa wa mchezo kwa kuipangua mikwaju miwili ya penalti, zilizopigwa na Harold Moukoudi pamoja na James Lea-Siliki, na baadaye kushuhudia Clinton Njie akiupaisha angani nje ya uwanja penalti ya nne ya Kameruni.

Mechi ya fainali Jumapili inawakutanisha nyota wawili wa Liverpool, Mohamed Salah wa Misri na Sadio Mane wa Senegal, ambapo Mafarao wa Misri watakuwa wakifukuzia kombe la nane la ubingwa wa Afrika huku Senegal wakiwa hawajawahi kuligusa.

''Tunayo fahari kubwa kutokana na mafanikio yetu lakini bado kuna hatua moj inayobaki'' alisema kocha msaidizi wa Misri Diaa al-Sayed amesema kwa niaba ya kocha mkuu Carlos Queiroz ambaye alionyeshwa kadi nyekunu baada ya msuguano wa mara kwa mara na refarii.

Kamerun Ansturm in Yaounde
Watu wanane walifariki katika uwanja wa Olembe tarehe 24.Januari 2022Picha: Thierry Noukeu/AP/picture alliance

Mlolongo wa matatizo kwa Kameruni

Matumaini ya Cameroun ya kulinyanyua kombe kwenye uwanja wa nyumbani yalikatizwa kwa njia ya kuumiza, na bado watalazimika kucheza na Burkina Faso kuwania nafasi ya tatu wikendi hii.

''Tumeumia sana kama timu, na pia Wakameruni wote milioni 27 wameumia na sisi, lakini ndiomambo ya soka,'' amesema kocha wa Kameruni Toni Conceicao.

Ni takribani siku 10 tu tangu janga la mkanyagano lilipotokea kwenye uwanja wa Olembe, lililouwa watu wanane na kujeruhi wapatao 38, kabla ya mechi ya Kameruni dhidi ya Comoro kuwania nafasi katika 16 bora.

Shirikisho la soka Afrika lilikuwa limeufunga uwanja huo kwa muda likisubiri ripoti ya uchunguzi wa mkasa huo, na iliizuia mechi ya robo fainali kuchezwa uwanjani hapo.

Uwanja wa Olembe alikuwa karibu mtupu

Mkasa huo uliwafanya mashabiki wengi wakose hamu ya kurudi katika uwanja huo, na mechi ya jana ilitazamwa na watu 24,371 katika uwanja huo wenye uwezo wa kuwapokea watazamaji 60,000.

Africa Cup of Nations | Kamerun v Ägypten
Nahodha wa Misri Mohamed Salah (jezi nyeupe) hakung'aa sana katika mechi ya nusu finali dhidi ya KameruniPicha: KENZO TRIBOUILLARD/AFP via Getty Images

Uwanja karibu mtupu ulikuwa aibu kwa Kameruni, nchi inayojulikana kuwa na wapenzi wengi wa soka, ikizingatiwa kuwa mechi hii ya nusu fainali iliwakutanisha miamba ya soka Afrika, moja ikiwa timu mwenyeji.

Baada ya kutia kibindoni tiketi ya kucheza fainali, Misri imewataka waandaaji wa mashindano hayo kufikiria kuihamishia mechi hiyo Jumatatu badala ya Jumapili, kwa hoja kwamba, wapinzani wao Senegal wamepata siku ya ziada ya kupumzika na kujiandaa.

''Ninataka kuwaeleza maafisa wote wa shirikisho la soka Afrika, CAF kwamba Senegal wamepata siku ya ziada ya kujianda, kwa hiyo, pengine mechi ya fainali ingehamishiwa Jumatatu,'' amesema koch msaidizi wa Misri Diaa al-Sayed.

Vyanzo: afpe, rtre