AFCON 2013; Nigeria kutoroka na kombe?
10 Februari 2013Lakini uwezekano kwa Burkina faso kuonyesha maajabu katika fainali hiyo hauwezi kupuuzwa.
Vikosi vyote viwili vilianza kampeni yake kwa matumaini finyu lakini viliweza kusonga mbele hadi fainali katika mashindano ambayo yalikumbwa na maajabu kadha.
Nigeria , licha ya kuwa kigogo katika soka ya Afrika, iliweka wazi kuwa inaona mashindano haya nchini Afrika kusini kama fursa ya kutayarisha kikosi kipya, wakati Burkina Faso ilionekana wakati wote kuwa ni wasindikizaji tu.
Pamoja na hayo timu zote hizo zimeweza kuvuka vikwazo kadha na kufikia fainali , ambapo Burkina faso inakuwa mara yake ya kwanza kufikia kiwango hicho.
Ikiwa katika nafasi ya 92 katika orodha ya timu bora duniani kwa mujibu wa shirikisho la kandanda ulimwenguni FIFA, Burkina Faso imepindukia matarajio ya ndoto yao kwanza kwa kushika nafasi ya kwanza katika kundi lao, na kisha kuipiga mwereka Togo baada ya muda wa nyongeza katika robo fainali na kuiweka kando Ghana kwa mikwaju ya penalti katika mpambano wa kuvutia wa nusu fainali Jumatano iliyopita.
Burkinabe kubadili uwanja
Michezo yao yote mitano , ikiwa ni pamoja na sare ya bao 1-1 dhidi ya Nigeria katika siku ya tatu ya mashindano hayo ilichezwa katika uwanja unaoonekana kuwa na mchanga zaidi ya majani wa Nelspruit, lakini sasa watakabiliana katika mchezo wao wa kwanza katika uwanja ulioko katika eneo la karibu mita 1,750 juu ya usawa wa bahari mjini Johannesburg.
Nigeria ambayo imecheza michezo yake miwili mjini Rustenburg katika eneo la mita 1,100 juu ya usawa wa mahari, inacheza katika fainali yake ya saba ya kombe la mataifa ya Afrika katika muda wa miaka 13.
Licha ya kuwa taifa hilo lenye wakaazi wengi katika bara la Afrika na nchi ambayo mara kwa mara hutoa vijana wenye vipaji vya uchezaji wa soka kwenda kuchezea nje ya nchi hiyo katika vilabu mbali mbali duniani , wameweza kushinda mashindano hayo mwaka 1980 na 1994 tu.
Kocha Stephen Keshi alikuwa nahodha wa Green Eagles, mara ya mwisho walipolinyakua kombe hilo, na iwapo Nigeria itafanikiwa kulitwaa kombe hilo mara hii, atakuwa mtu wa pili kufanya hivyo kama mchezaji na kocha, akifuata nyayo za Mahmoud al-Gohari wa Misri.
Mali yala shaba
Wakati huo huo Mali imerudia kile ilichofanya mwaka jana katika mashindano haya , kwa kutwaa medali ya shaba, baada ya kuishinda Ghana kwa mabao 3-1.
Mwaka jana Mali iliishinda Ghana kwa mabao 2-0 katika mchezo huo wa kutafuta mshindi wa tatu. Wachezaji wa Mali waliingia katika mashindano ya mwaka huu wakisema kuwa wanataka kuleta furaha kwa mashabiki nyumbani kwao ambao wanakabiliwa na msukosuko wa kisiasa na hali isoyokuwa thabiti ya kiusalama.
"Nimefurahi na ninajisikia fahari . Wachezaji wamejituma kwa moyo wao wote na kuleta medali ya shaba", kocha wa Mali Patrice Carteron amesema. " Kwa taifa kama Mali , haya ni matokeo mazuri sana". Kipigo ilichopata Ghana kimeongeza zaidi hali ya kukatisha tamaa, timu ambayo imefikia nusu fainali mara nne zilizopita lakini inaondoka tena bila ya taji.
Ghana iliambulia kushiriki katika kuwania nafasi ya tatu baada ya kushindwa katika mpambano wa nusu fainali na Burkina Faso katika mikwaju ya penalti. Black Stars walishinda mara ya mwisho ubingwa wake wa nne mwaka 1982.
Mwandishi : Sekione Kitojo / ape / rtre
Mhariri: Amina Abubakar