1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Addis Ababa,Baraza la Amani na Usalama la AU lakutana kuweka vikwazo zaidi kwa Togo.

24 Februari 2005
https://p.dw.com/p/CFbE

Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika-AU,linakutana leo mjini Addis Ababa,Ethiopia kufikiria hatua zaidi za vikwazo dhidi ya serikali ya Togo kutokana na uamuzi wa jeshi la nchi hiyo kumuweka madarakani Faure Gnassingbe kama Rais wa nchi kushika nafasi ya hayati baba yake.

Chombo hicho cha Umoja wa Afrika ambacho majukumu yake yanafanana na yale ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa,kinatarajiwa kuunga mkono hatua zilizokwishachukuliwa na Jumuia ya Uchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi-ECOWAS,ambayo mwishoni mwa wiki iliyopita iliisimamisha uwanachama wa jumuia hiyo nchi ya Togo,ikaiwekea vikwazo vya silaha na kuwarejesha nyumbani mabalozi wote wa nchi hizo waliokuwa mjini Lome.

Nao Umoja wa Ulaya umetishia kuiwekea vikwazo vikali Togo ambavyo havikuelezwa hatua ambayo inafuatiwa na wito wa Marekani wa kuunga mkono hatua zitakazochuliwa na Umoja wa Afrika na zile zilizokwishachukuliwa na ECOWAS.Lengo la hatua zote hizo ni kuishinikiza serikali ya Togo kufuata utawala wa katiba na demokrasi katika kuwaweka madarakani viongozi wake.