1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ADDIS ABABA : Zenawi atangaza Ethiopia iko vitani Somalia

25 Desemba 2006
https://p.dw.com/p/CCgG

Waziri Mkuu wa Ethiopia Meles Zenawi ametangaza katika hotuba iliyoonyeshwa na televisheni kwamba nchi yake inaendesha vita dhidi ya Uongozi wa Kiiislam katika nchi jirani ya Somalia ili kuuhami uhuru wa nchi yake.

Hii ni mara ya kwanza kwa Ethiopia kukiri hadharani kuhusiki kijeshi nchini Somalia ambapo kwa mara ya kwanza imetuma ndege za kivita hapo jana kuwashambulia wapiganaji wa Kiislam wanaoyazingira makao makuu ya serikali yalioko katika mji wa Baidoa.

Meles amesema wanajeshi wao wa ulinzi wataondoka nchini Somalia mara tu baada ya kumaliza shughuli yao na kwamba licha ya mashambulizi hayo ya kijeshi Ethiopia inaunga mkono mazungumzo kati ya Muungano wa Mahkama za Kiislam na serikali ya mpito kuunda serikali ya pamoja.

Wataalamu wa kijeshi wanakadiria kwamba Ethiopia yumkini ikawa na wanajeshi kati ya 15,000 na 20,000 kusaidia serikali dhaifu ya Somalia wakati hasimu yake mkuu Eritrea ina wanajeshi kama 2,00o kuwasaidia waapiganaji wa Kiislam.

Wachambuzi wa mambo wana hofu kwamba mashambulizi hayo ya anga ya Ethiopia huenda yakazidi kuchochea mapambano hayo ambayo hatimae yanaweza kusababisha vita vitakavyolikumba eneo zima la Pembe ya Afrika.