Addis Ababa. Watu kadha wakamatwa , baada ya ghasia zilizosababisha watu 26 kuuwawa nchini Ethiopia.
10 Juni 2005Majeshi ya usalama ya Ethiopia yamewakamata wanachama kadha wa vyama vya upinzani jana, siku moja baada ya polisi na vikosi vya jeshi la ulinzi kuwafyatulia risasi waandamanaji na kuuwa kiasi cha watu 26.
Chama kikuu cha upinzani , Coalition for Unity and Democracy, ambacho serikali inakishutumu kwa kuchochea maandamano, kimesema kuwa wanachama wake 14 wamekamatwa tangu machafuko yaliyotokea siku ya Jumatano, tukio baya kabisa la umwagaji damu kuwahi kutokea katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa katika muda wa miaka minne.
Ghasia hizo zilitokea baada ya wiki kadha za shutuma za wapinzani kuwa chama tawala , Ethiopian Peoples Revolutionary Democratic Front, kimewatisha wapiga kura na kufanya udanganyifu katika uchaguzi ili kuweza kubaki madarakani.
Ikulu ya Marekani imeyaeleza machafuko hayo kuwa ni kitu ambacho hakikubaliki.