1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ADDIS ABABA: Wapinzani nchini Ethiopia watoa changa moto kali

16 Mei 2005
https://p.dw.com/p/CFCx

Muungano mkuu wa upinzani nchini Ethiopia umesema kuwa umeshinda viti 20 kutoka jumla ya viti 23 katika mji mkuu Addis Ababa,katika uchaguzi wa bunge uliofanywa siku ya jumapili.Hayo ni kwa mujibu wa matokeo yasio rasmi yaliobandikwa kwenye vituo vya kupigia kura.Muungano wa vyama vya upinzani safari hii,kulinganishwa na chaguzi za nyuma,umetoa changa moto kali kwa waziri mkuu Meles Zenawi.Juu ya hivyo chama tawala cha Zenawi kinatazamiwa kupata ushindi mkubwa katika bunge la shirikisho lenye viti 547.Zaidi ya asili mia 90 ya watu milioni 25.6 walioandikishwa kupiga kura,waliitumia fursa hiyo katika uchaguzi wa siku ya jumapili.Uchaguzi huu unatazamwa kama ni mtihani wa udemokrasia kwa waziri mkuu Meles ambae mwaka 1991 alingoá udikteta wa Kimarxist wa miaka 17.Lakini wadadisi wanasema lile tangazo lililotolewa na Meles siku ya jumapili kupiga marufuku maandamano ni ishara kuwa serikali ina wasi wasi kuhusu wafuasi wa upinzani katika mji mkuu Addis Ababa.Matokeo ya mwanzo ya uchaguzi yanatarajiwa tarehe 21 Mei na matokeo rasmi yatatangazwa Juni 8.