1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Addis Ababa. Wanajeshi 21 wa jeshi la kulinda amani la Afrika katika jimbo la darfur bado hawajulikani waliko.

2 Oktoba 2007
https://p.dw.com/p/CBKy

Umoja wa Afrika umesema wanajeshi wake 21 wa jeshi la kulinda amani bado hawajulikani waliko katika jimbo lenye machafuko la Darfur , kufuatia shambulio la Jumamosi lililofanywa na watu wenye silaha ambao hawajatambulika dhidi ya kambi ya jeshi la umoja wa Afrika ya Haskanita.

Kiasi cha wanajeshi 10 wa kulinda amani , wengi wao kutoka Nigeria wameuwawa, na kusababisha shutuma kali duniani kote. Senegal na Nigeria , ambazo zote zina wanajeshi wake katika jeshi hilo la Afrika ,zimesema zitaangalia upya uwekaji wa wanajeshi wao. Kamanda wa jeshi hilo la kulinda amani Martin Luther Agwai kutoka Nigeria alisema jana kuwa jeshi hilo halitakubali kitendo kama hicho kuzuwia juhudi za kuleta amani.

Ni mshtuko kwamba katika wakati huu ambapo tulidhani kuwa tutapata amani na mazungumzo ya amani nchini Libya , lakini mambo ya kukatisha tamaa kama haya yanaweza kutokea ambapo maisha ya wanajeshi wasiokuwa na hatia yamepotea. Lakini nataka kumhakikishia kila mtu kuwa jeshi halitakubali tukio hili kuzuwia juhudi zetu za kuleta amani.

Rais wa Senegal Abdoulaye Wade amesema huenda akayaondoa majeshi ya nchi yake iwapo uchunguzi wa umoja wa Afrika utagundua kuwa kambi ya Haskanita ilikuwa na ulinzi hafifu kwa ajili ya kujilinda. Baadaye mwaka huu jeshi la pamoja kati ya umoja wa Afrika na umoja wa mataifa lenye wanajeshi 26,000 linatarajiwa kuwekwa na kuchukua nafasi ya jeshi la umoja wa Afrika baada ya majadiliano ya muda mrefu na serikali ya Sudan. Marekani imesema kuwa inataka jeshi hilo la pamoja kuwekwa haraka iwezekanavyo katika jimbo hilo. Katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki-moon amezitaka pande zinazopigana katika jimbo la Darfur kufikia suluhisho la pamoja na amani katika mazungumzo nchini Libya yatakayofanyika Oktoba 27. Tangu mzozo huo kuanza mwaka 2003 pamoja na njaa katika jimbo la darfur watu 200,000 wameuwawa na kusababisha watu milioni mbili kukimbia makaazi yao.