ADDIS ABABA: Vurugu mjini Addis na watu watano wauwawa
1 Novemba 2005Nchini Ethiopia nako polisi wa kuzuia ghasia walilazimika kufyatua risasi hewani leo hii mjini Addis Ababa ili kuwatawanya wafuasi wa upinzani waliokuwa wakirusha mawe na kufanya vurugu kupinga matokeo ya uchaguzi uliofanyika mei 15
Imeripotiwa kwamaba watu watano wameuwawa katika vurugu hizo.
Waandamanaji hao pia waliwasha mioto na kuweka vizuizi barabarani na kuvunja vioo vya magari kadhaa.
Vurugu hizo zimezuka baada ya chama kikuu cha upinzani nchini Ethiopia kuitisha mgomo wa kupinga matokeo ya uchaguzi uliofanyika miezi mitano iliyopita ambao wanadai ulikumbwa na visa vya wizi wa kura.
Chama hicho kikuu cha Upinzani cha CUD kilitoa mwito wa mgomo wa kubaki majumbani kwa wafuasi wake aidha kushiriki katika maandamano ya amani na vile vile kuacha kusikiliza na kuangalia radio na televisheni ya taifa lakini mambo yamekwenda kinyume na ilivyo pangwa.
Hali ya wasiwasi wa kisiasa imejitokeza nchini Ethiopia miezi mitano tangu tume ya uchaguzi nchini humo itangaze kwamba chama cha waziri mkuu wa nchi hiyo Meles Zenawi kimeshinda uchaguzi.