1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ADDIS ABABA: Vita vyakaribia kuzuka kati ya Ethiopia na Eritrea

3 Novemba 2005
https://p.dw.com/p/CEM6

Afisa wa ngazi ya juu wa umoja wa mataifa anayeifuatilia hali ya wasiwasi katika mpaka wa Ethiopia na Eritrea amesema ana hofu ya kuzuka vita vipya kati ya mataifa hayo.

Katika kipindi cha siku kumi zilizopita, nchi hizo mbili zimekuwa zikiwapeleka wanajeshi wake pamoja na vifaa vya vita karibu na mpakani. Kamanda wa kikosi cha walinda amani wa umoja wa mataifa nchini Ethiopia na Eritrea, Rajender Singh, ameonya kwamba ikiwa jamii ya kimataifa haitachukua hatua za dharura kuutanzua mzozo huo, huenda vita vikali vikazuka wakati wowote.

Majeshi ya umoja wa mataifa yanalinda eneo linalozitenganisha nchi hizo, lililoundwa baada ya vita vya miaka miwili unusu kumalizika mwaka wa 2000. Hivi karibuni Eritrea imekuwa ikiwawekea vikwazo walinda amani hao wa umoja wa mataifa.

Katibu mkuu wa umoja huo bwana Kofi Annan, ameelezea wasiwasi wake mkubwa kwa hatua hiyo ya Eritrea na Ethiopia kuwapeleka wanajeshi wake katika eneo la mpakani. Amelitolea mwito baraza la usalama la umoja wa mataifa na wanachama wa umoja huo kuchukua hatua muhimu za haraka kuzuia kuzuka kwa vita katika eneo hilo.