ADDIS ABABA: Vikosi vya Umoja wa Afrika kubakia Somalia
19 Julai 2007Matangazo
Umoja wa Afrika umeamua kurefusha kwa miezi sita mingine muda wa vikosi vyake kubakia nchini Somalia.Msemaji wa umoja huo amesema,mamlaka ya vikosi hivyo yalimalizika Jumatano jioni na ilitarajiwa kuwa vingepokewa na vikosi vya Umoja wa Mataifa ambavyo kwa hivi sasa bado si tayari. Kwa hivi sasa,kama wanajeshi 1,500 wa Uganda wapo Somalia kwa niaba ya Umoja wa Afrika.Kwa jumla, Umoja wa Afrika unatazamia kuwa na hadi wanajeshi 8,000.Lakini Nigeria,Burundi,Malawi na Ghana zilizoahidi kuchangia vikosi,bado hazijatimiza ahadi hiyo.
Vikosi vya Umoja wa Afrika vinatazamiwa kuchukua nafasi ya majeshi ya Ethiopia ambayo mwaka jana yalisaidia vikosi vya serikali ya Somalia kuwatimua wanamgambo wa Kiislamu.