ADDIS ABABA: Umoja wa Afrika waendelea na mradi wake wenyewe
5 Agosti 2005
Umoja wa Afrika umelikataa pendekezo lililotolewa na kundi la G4 yaani Ujerumani,Brazil,Japani na India kuhusika na mageuzi katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.Katika mkutano wa kilele mjini Addis Ababa,viongozi wa Kiafrika kutoka nchi 53 walikubaliana kuendelea na mradi wao wenyewe badala ya kuidhinisha ule uliopendekezwa na kundi la G4 kuhusika na kuongezwa kwa idadi ya wanachama wa kudumu katika Baraza la Usalama.Nchi za Kiafrika zinataka kuwa na viti 2 vya kudumu pamoja na kura ya turufu.Uamuzi wa Umoja wa Afrika humaanisha kuwa azimio lake na la G4 huenda yasipate uwingi wa theluthi-mbili,unaohitajiwa katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lenye wanachama 191.Mradi wa G4 unapendekeza kuzidisha idadi ya wanachama kwenye Baraza la Usalama,kuwa 25 badala ya 15 kama ilivyo hivi sasa.Miongoni mwa wanachama hao wapya,6 wapewe viti vya kudumu lakini bila ya kura ya turufu.Marekani na China zinapinga mageuzi yo yote yale katika Umoja wa Mataifa,lakini wanachama wenzao wa kudumu,yaani Ufaransa na Uingereza wanaunga mkono msimamo wa G4.