ADDIS ABABA : Umma mkubwa wajitokeza katika uchaguzi
15 Mei 2005Wananchi wa Ethiopia leo wamejitokeza kwa wingi katika uchaguzi wa bunge wenye ushindani mkali ambapo unatarajiwa kuiweka nchi hiyo ya Pembe ya Afrika inayojulikana kwa kutopea umaskini na njaa kwenye mkondo wa kuelekea katika demokrasia.
Katika mji wa Addis Ababa umma mkubwa umekuwa katika msururu kwenye vituo vya kupiga kura alfajiri na mapema na Rais wa zamani wa Marekani Jimmy Carter amesema kwamba mbali na suala la kuwepo misururu mirefu kutokana na kujitokeza kwa wapiga kura wengi uchaguzi huo umekuwa ukifanyika kwa utulivu bila ya kuwepo kwa hitilafu kubwa.
Carter ambaye ni mtu mashuhuri kabisa miongoni mwa waangalizi wa uchaguzi wa kigeni 300 hakutowa maoni yake juu ya tathmini ya jumla ya uchaguzi huo na malalamiko ya upinzani ya kuwepo hadaa lakini amesema ukaguzi binafsi aliofanya kwa vituo 12 ya kupigia kura katika mji mkuu huo hakugunduwa matatizo yoyote makubwa.
Meles Zenawi wa chama tawala EPRDF anatazamiwa kushinda kipindi cha tatu cha uwaziri mkuu.Upinzani umeishutumu serikali kwa kujaribu kuhujumu uchaguzi huo na pia umeahidi kususia matokeo venginevyo chama tawala kinakomesha kuwanyanyasa na kuwatia ndani wafuasi wake.
Waethiopia milioni 26 wamejiandikisha kupiga kuta katika uchaguzi huo.