ADDIS ABABA: Uingereza yawaonya raia wake kutosafiri kwenda Ethiopia
3 Novemba 2005Uingereza imetoa ilani kwa raia wake wasisafiri kwenda Ethiopia ambako watu 31 wameuwawa na wengine wasiopungua 150 kujeruhiwa katika maandamano ya kuipinga serikali. Wizara ya mambo ya kigeni imeshauri safari zisizo muhimu zisifanywe kutoka Uingereza kwenda mjini Addis Ababa mpaka kutakapokuwa na utulivu mjini humo na kuthibitisha kukamatwa kwa wanasiasa wa upinzani wa nchi hiyo na kuendelea kwa machafuko katika mji huo.
Maelfu ya waislamu walikusanyika kwa maombi ya alfajiri mjini Addis kusherehekea kumalizika kwa mwezi wa ramadhani. Walinda usalama wanashika doria kwenye barabara za mji huku maduka yakiwa yamefungwa kwa sikukuu ya Eid Al-Fitr.
Marekani imezilaani njama za makusudi za kusababisha machafuko mjini Addis. Msemaji wa wizara ya mambo ya ndani nchini Marekani, Sean McCormack ametoa mwito kuwepo utulivu na kuitaka serikali ya Ethiopia kuteua tume huru kuchunguza vurugu hizo na machafuko ya mwezi Juni dhidi ya matokeo ya uchaguzi uliofanyika nchini humo mwezi Mei, ambao upinzani unasema kulikuwa na udandanyifu. Amewataka pia viongozi wa upinzani wasichochee ghasia wakati huu wa hali ya wasiwasi.